Zitto Kabwe
Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao wanadaiwa kufungamana na viongozi wakuu watatu waliofukuzwa, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na aliyekuwa
Mwenyekiti wa chama hicho Arusha, Samson Mwigamba, jana walifanya maandamano ya kinyemela hadi ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa kutaka viongozi wakuu wa chama hicho waadhibiwe kwa ukiukaji wa katiba ya chama.
Wanachama hao wanadai kuwa, mbali ya uvunjaji wa katiba, viongozi hao wanahusika na ubadhirifu wa fedha za chama zilizotokana na kodi za umma zaidi ya Sh. bilioni 10.038, ingawa Dk. Willibrod Slaa amekuwa akiyapuuza madai hayo kuwa siyo mapya.
Wanachama hao takribani 40 hadi 50 walifika ofisini kwa Msajili saa 7:00 mchana baada ya kushuka katika basi la Uda katika ofisi za Magereza.
Walikuwa wameshika mabango yenye maandishi tofauti, wakilalamikia vitendo vinavyofanywa na viongozi wa Chadema.Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Temeke, Joseph Yohana, alidai kuwa viongozi wakuu wa chama hicho wamekuwa wakitumia mali za chama vibaya, ikiwamo kujilipa mishahara bila kuwalipa makatibu wa mikoa na wilaya.
Pia, alidai kuwa viongozi wamekuwa wakinunua magari kwa fedha za chama na kuyakodisha kwa chama na kuwa yanapochakaa wanakiuzia chama.
Alidai kuwa viongozi hao wamekuwa wakiwakana viongozi wengine wanapothubutu kusema ukweli kuhusiana na mambo mbalimbali ya chama.
Yohana alidai kuwa pamoja na madai hayo pia viongozi hao wamekiingiza chama katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kinyume cha kanuni za chama.
Baada ya kuwasili ofisini hapo walipokelewa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Ntahoza, ambaye alipokea barua yao na kuwataka wawe na subira ya kupatiwa majibu ya madai yao ambayo yatashughulikiwa ndani ya siku 14 na kwamba watapatiwa taarifa kwa njia ya simu ili wayafuate.
“Nimepokea barua yenu ya malalamiko, kama ilivyo ada ofisi hii inapokea barua mbalimbali za watu binafsi na kuzishughulikia ndani ya wiki mbili. Hata hivyo, malalamiko yanaweza kuchukua zaidi ya wiki mbili kutokana na ukubwa wa madai na kama yanahitaji maelezo kutoka kwa mlalamikiwa,” alisema Nyahoza.
Wakizungumza na vyombo vya habari baada ya kukabidhi barua hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, Joram Mbogo, alidai kuwa viongozi wa chama wamekuwa wakitoa matamko ya kuungana na Ukawa yenye lengo la kuachiana majimbo ya uchaguzi.
“Wanakiuka Katiba ya chama kwani Sura ya tisa ibara ya 9.3.1 ya Katiba ya Chadema inasema: ‘Chama kinaweza kuunda mseto na chama au vyama vingine vyenye madhumuni na malengo yanayofanana ili kuimarisha uwezo wa kushinda uchaguzi mkuu au serikali moja ya mtaa kwa lengo la kuunda utawala wa pamoja.”
Aliendelea kudai kuwa, kutokana na kanuni hizo, chama kilitakiwa kukaa kikao cha Baraza Kuu ili kupitisha ajenda zilizojadiliwa na mkutano mkuu, lakini haikufanyika hivyo, badala yake viongozi waliamua wenyewe kujiunga na CUF na NCCR-Mageuzi kinyume cha taratibu.
Hata hivyo, Ukawa siyo muungano wala mseto, isipokuwa ni ushirikiano wa vyama katika masuala mbalimbali.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alikwisha kuzungumzia suala la Ukawa kwa kuwataka wanaolalamikia umoja huo kutambua kuwa siyo chama cha siasa ambacho kimesajiliwa na ofisi yake na kwamba vyama vya siasa vinaruhusiwa kisheria kuwa na ushirikiano almradi hawavunji sheria.
POLISI WAWATAWANYA
Baada ya kutoka Ofisi ya Msajili, wanachama hao waliandamana kuelekea katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya kumpa barua ya kutaka ikague taarifa ya fedha za chama za mapato na matumizi.
Kabla ya kufika kwa CAG, walikutana na polisi waliokuwa katika magari ya Defender mbili na pikipiki kadhaa na wengine wakitembea kwa miguu kuwafuatilia ili wasiingie katika ofisi hizo kutokana na kuandamana bila kibali.
Wakiwa mlangoni kwa CAG, ofisa mmoja wa polisi aliyejitambulisha kwa jina la SSP Andrew Sata, aliwahoji na baada ya kujieleza aliwataka kusitisha shughuli hiyo na kuteua wawakilishi wao kuwasilisha madai yao.
“Nadhani kanuni na taratibu za kupeleka taarifa mnazifahamu, kutembea kwa makundi namna hii hairuhusiwi, mmevunja sheria za nchi, hivyo nawaomba mtawanyike mkajipange upya ili mmoja wenu au wawili ndiyo walete hayo malalamiko yenu,” alisema SSP Sata.
Baada ya kutolewa kwa tamko hilo, wanachama hao walitawanyika kutoka eneo hilo kwa njia tofauti huku askari polisi wakibaki eneo hilo kwa ajili ya ulinzi.
CHADEMA YAWAPUUZA
NIPASHE lilipozungumza na Afisa Habari Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene, kuhusiana na tukio hilo pamoja na madai ya wanachama hao, alisema madai hayo hayana ukweli wowote na siyo mapya kwa kuwa yalishajibiwa na Kamati Kuu ya chama hicho.
Pia alisema madai yao ni yale yaliyokuwa katika waraka wa siri uliotumika kuwafukuzisha uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe; aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Mwigamba baada ya kutimuliwa Chadema alishirikiana na wenzake kuunda chama kipya cha Alliance for Change and Transparency (ACT).
Kadhalika, Makene alisema hizo ni propaganda za masalia wa usaliti na vibaraka wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wanatumika kukwamisha jitihada za Chadema kujadili masuala ya msingi ya kitaifa pamoja na kutaka kuwaondoa katika kazi ya kuibana serikali katika mambo ya msingi.
Alisema hivi sasa Watanzania wanasubiri kwa hamu kujadili masuala mbalimbali ya msingi hususani Katiba mpya, uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani, lakini wao wanatafuta njia nyepesi za kuwaondoa katika mstari.
Makene alisema hata Mbogo alikwisha kufutwa uanachama wa Chadema na aliahidi kuwa chama hicho kitalizungumzia suala hilo kwa upana zaidi leo katika mkutano wa waandishi wa habari.
SOURCE: NIPASHE
0 maoni:
Post a Comment