Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI ATAKA KUMTWANGA MGUMI MHE KAFULILA; ALIMUITA TUMBILI NAYE AKAITWA MWIZI WA IPTL

 

Jaji Werema ataka kumtwanga KafulilaKASHFA ya ununuzi wa Kampuni ya IPTL na fedha za Escrow, jana nusura iharibu taswira ya Bunge baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kutaka kumpiga Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi).
Tafrani hiyo ilianza baada ya wawili hao kurushiana maneno ya kejeli ambapo Werema alimuita Kafulila tumbili, huku mbunge huyo akijibu kwa kudai naye ni mwizi.


Chanzo cha sakata hilo kilitokana na mwongozo aliouomba Kafulila kwa Mwenyekiti wa Bunge, Musa Azzan Zungu, akitaka serikali ieleze kwanini ilitoa fedha zake katika akaunti ya Escrow na kuilipa IPTL.


Kafulila alisema serikali, hasa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alilidanganya Bunge kuwa serikali ililipa fedha kutokana na kesi iliyoamuriwa na mahakama ilhali wakijua jambo hilo si kweli.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua kwanini serikali ililipa fedha hizo wakati hakuna hukumu ya mahakama yoyote iliyoamrisha kufanya hivyo…. kutoa fedha hizo katika akaunti hiyo ni ufisadi,” alisema.


Mara baada ya Kafulila kumaliza kuomba muongozo huo, Zungu, alimtaka Jaji Werema atoe ufafanuzi.
Katika ufafanuzi wa Werema, alisema fedha zilizokuwapo kwenye akaunti ya Escrow si za serikali kama inavyodaiwa na Kafulila kwakuwa fedha za serikali hazikai huko.
Alisema kumekuwa na taarifa za kupotosha umma kuwa serikali imetoa fedha kuilipa IPTL wakati ukweli ni kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo kutokana na misuguano baina ya wanahisa wawili ambao ndio wamiliki wa IPTL.


Werema alibainisha kuwa mmoja wa wanahisa hao alikuwa akitaka IPTL, ifilisiwe huku mwingine akipinga juu ya jambo hilo.
Wakati Werema akiendelea na maelezo hayo, Kafulila alikuwa akitaka aeleze maslahi yake katika suala hilo la IPTL kwakuwa naye ni miongoni mwa watuhumiwa.
Pia mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alikuwa akitaka kutoa taarifa juu ya jambo hilo, lakini hakupewa nafasi hali iliyomfanya awe anasimama mara kwa mara kutaka kusema jambo bila kupata fursa hiyo.
Werema alisema Kafulila ni miongoni mwa watu wanaosambaza vipeperushi vya kupotosha watu ndani ya Bunge kuhusu akaunti ya Escrow.
“Kafulila ni miongoni mwa wanaoeneza taarifa potofu…, kama ni tuhuma au kuna rushwa itakuja kujulikana, tusubiri uchunguzi wa vyombo husika. Escrow haikuwa na fedha za serikali, Escrow kulikuwa na ugomvi wa familia,” alisema.


Wakati Werema akiendelea kutoa maelezo hayo, Kafulila alikuwa akipinga mwanasheria huyo mkuu kuzungumzia jambo hilo, ikiwa yeye ni miongoni mwa wanaotajwa kuhusika nalo bila kueleza uhusika wao.
Kitendo hicho kilimfanya Werema kumuambia Kafulila kuwa kama anataka kuleta mambo ya nje ndani ya Bunge asifanye hivyo bali amsubiri nje.
“Wanyankore wanasema tumbili hawezi kuamua kesi ya msitu, hivyo naomba nisikilize, hata kama ni mtuhumiwa nina fursa ya kusikilizwa, hivyo naomba nisikilize  wewe tumbili,” alisema Werema.
Kauli hiyo ilimfanya Kafulila kumuita Werema ni mwizi hatua iliyomfanya mwanasheria huyo mkuu kuhoji “Mimi Mwizi?”


Malumbano hayo yalisababisha Bunge litawaliwe na kelele kutoka kila upande hali iliyomfanya Mwenyekiti wa Bunge, Zungu, kuingilia kati na kuwataka Kafulila na Mnyika kupeleka vielelezo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali pamoja na kutoa nakala kwa spika.
Baada ya kuhairishwa kwa kikao hicho, Werema  alionekana kutoridhishwa na kauli za Kafulila na kuamua kumfuata alipokuwa ameketi kwa lengo la kumuadhibu.
Hata hivyo, dhamira hiyo ilishindwa kutimia baada ya Waziri wa Ushirikiano wa Nchi za Afrika Mashariki, Samwel Sitta na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, kumzuia asitekeleze alilokusudia na kutoka naye nje ya ukumbi wa Bunge.


Nje ya Ukumbi wa Bunge, Wassira, alisema kuwa waliamua kumzuia Werema kwakuwa waliamini alichokuwa akienda kukifanya kingesababisha kuchafuka kwa amani ndani ya Bunge.
“Ni jambo la busara kwa sisi wabunge kutoa kauli zetu kwa staha na kuheshimiana ili kuepuka jazba miongoni mwetu,” alisema Wassira.


Mnyika, Kafulila wanena
Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha Bunge, Mnyika na Kafulila, walisema serikali inalinda ufisadi uliofanywa na baadhi ya watendaji wake.
Huku wakionyesha vielelezo vya sakata hilo, wabunge hao walisema hakuna nyaraka yoyote inayoonyesha mahakama iliamuru PAP ilipwe fedha za IPTL kama ilivyofanya serikali.
Katika moja ya vielelezo hivyo, wabunge hao walibainisha kuwa Tanesco iliifahamisha mahakama iliyokuwa ikishughulikia jambo hilo kuwa wamebadilisha mawakili watakaowawakilisha.
Mnyika na Kafulila, walimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kumuagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo, kufuta kauli yake kuwa fedha hizo zililipwa kwa amri ya mahakama.
“Kauli yake ile ilikuwa ni ya uongo… sisi tunamtaka aifute, asipofanya hivyo baada ya siku mbili tutaanzisha mchakato wa kukusanya saini za wabunge kumng’oa Pinda,” alisema Mnyika.

CHANZO: TANZANIA DAIMA

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO