Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Siri ya mauaji ya Zanzibar yafichuka

 

*Mkono wake unahusisha taasisi za kimataifa

*Rai lanasa CD ya video ya kulipa kisasi, kuua

*Orodha ya maaskofu wanaosakwa yabainika

untitledTAASISI ya kimataifa ya kidini kwa kushirikiana na makundi mawili ya kigaidi ya nje ya Tanzania yanatajwa kuhusishwa katika matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa viongozi wa kiimani Zanzibar, gazeti la Rai limebaini.

Mbali ya taasisi hizo ambazo tayari uhusiano wake wa kikazi na makundi ya Al Shabaab na Boko Haram umeshaanza kuchunguzwa, matukio hayo ya mauaji yanahusishwa pia na kauli zinazoonekana kuwa za kichochezi zinazotolewa na Sheikh mmoja anayeishi nchini mwenye asili ya Kongo (jina tunalo)

Utafiti uliofanywa na gazeti la Rai umebaini kwamba, mikakati inayohusisha kutekelezwa kwa mauaji hayo na vitendo vingine vya kujeruhi na kuchoma makanisa inahusisha pia vikao vya siri ambavyo kimojawapo kilipata kukaa nchini Nigeria na kujumuisha viongozi wa kundi maarufu nchini humo la Boko Haram.

Vyanzo kadhaa vya habari vilivyozungumza na Rai, vinaeleza kwamba, matukio hayo ya kupangwa yana malengo kadhaa yakiwamo kulazimisha muungano kuvunjwa na kulipiza kisasi dhidi ya matukio ambayo yamepata kutokea nje ya Tanzania.

Hata hivyo, gazeti hili la Rai halikuweza kuthibitisha sababu ambazo zilisababisha kisiwa cha Unguja chenye waumini wengi wa Kiislamu kuwa mlengwa nambari moja wa mikakati hiyo ya kihalifu ambayo tayari imelaaniwa na viongozi na waumini wa Kikristo na Kiislamu.

Habari zaidi za uchunguzi zinaeleza kwamba, wauaji wanaotekeleza mauaji hao na mipango ya namna hiyo ya kihalifu ambayo tayari imesababisha vifo vya mapadri wawili wa Kanisa Katoliki wanatumia njia ya maji kutoroka na kwenda nchi jirani baada ya kufanikisha uhalifu huo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, vijana wa Kizanzibari wanaopanga na kuendesha mauaji hayo wanaelezwa kupata mafunzo mahusisi ya kutumia silaha na kulenga shabaha kutoka nchini Somalia liliko kundi la Al- Shabaab.

Mbali ya hayo, CD ya video ambayo RAI imeiona na inayodaiwa kusambazwa kwa siri kwa watu mahususi inamuonyesha sheikh mmoja anayetajwa kwa jina moja tu la Kapungu akiwahamasisha Waislamu kujihami na kulipa kisasi.

Katika sehemu moja ya kanda hiyo, sheikh huyo ambaye uraia wake unatajwa kuwa ni wa kutoka nchi moja jirani, anasikika akiwataka Waislamu kutokubali kuliacha tukio la sheikh mmoja wa Mombassa kuuawa likapita pasipo kujibiwa.

Sheikh wa Mombassa anayetolewa mfano ni Aboud Rogo ambaye anadai aliuawa ndani ya gari lake, yeye, mkewe na baba yake mzazi.

“Tulipata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba Sheikh Aboud Rogo Mwanaharakati maarufu wa Mombassa, amepigwa risasi ndani ya gari yake, akiwa na familia yake akielekea Nairobi.

“Yeye kapigwa risasi nyingi sana mwilini, mke wake pia na baba yake mzazi kapigwa risasi. Yeye na familia yake wamekufa, aliyenusurika ni mtoto mdogo aliyekuwa naye ndani ya gari yake. Ziko kauli zinasema kwamba amepigwa risasi 16 mwilini, ziko kauli zinasema kapigwa risasi 22.

“Mpigaji alitaka kuhakikisha haponi, na kweli Aboud Rogo alikufa papo hapo. Vyombo vyote vya habari ambavyo vingi ni vya makafiri, vilianza kutangaza Sheikh Aboud Rogo ameuawa na watu wasiojulikana.

“Waislamu wa Mombasa hawakusaka, trafiki waje, hawakutaka polisi wachunguze, polisi wa kwanza aliyefika, hakuweza kukaa pale, ndani ya saa tatu, Waislamu walimzika Sheikh Aboud Rogo.

“Waislamu wa Mombasa walikuwa hawana haja ya polisi kuchunguza kwa sababu wao wanaposema kauawa na watu wasiojulikana, Waislamu wana hakika kauawa na watu wanaojulikana. Waislamu walisema kauawa, hatuna haja.

“Baada ya hapo kukatokea fujo Mombasa magari kuchomwa moto na kuharibiwa, mimi nikiwauliza jamaa zangu Mombasa hali inaendeleaje wanasema hatujatoka ndani siku ya pili sasa. Shughuli zimesimama kwenye mji wa Mombassa.

“Niliwakumbusha Waislamu wa Mombasa warudi kwenye Kuraan, inasema akiuawa Sheikh Aboud Rogo au yeyote, unavunja magari ya watu? Kuraani inasema mlipe kisasi, akiuawa mwislamu huvunji gari ya mtu, unalipa kisasi, jicho kwa jicho, meno kwa meno.

“Kauawa Aboud Rogo, tafuta Askofu mmoja naye muueni, tafuta Kardinali na wewe muue, kauawa mwislamu tafuta padre muue tafuta mchungaji muue, wataacha hawa. Mkiua wanne watashika adabu.

“Kama hamna uwezo huo jipangeni jiratibuni, naanza fikra ngumu. Tafuta kardinali muue kwa kificho au kwa dhahiri,” anasikika akisema sheikh huyo katika mhadhara huo.

Vitisho dhidi ya viongozi wa dini nchini

Wakati CD hiyo ikisambaa, uchunguzi wa RAI unaonyesha kwamba, vitisho dhidi ya viongozi wa dini ya Kikristo wakiwamo, Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Augustine Shao, Askofu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael Hafidh na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa vikabainika.

Mbali ya hao, maaskofu wengine ambao waliwekwa katika orodha hiyo baada ya majina yao kutajwa kwa njia ya vipeperushi ni pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk. Valentine Mokiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo.

Katika orodha hiyo na kwa sababu ambazo bado hazijawekwa hadharani lilitajwa pia jina la Msaidizi wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Mussa Soraga ambaye hivi karibuni alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana mjini Unguja.

Kauli za Maaskofu

Baada ya taarifa kufika ndani ya chumba chetu cha habari kwamba zipo taarifa za viongozi kadhaa kuuawa, tuliwatafuta wahusika wakuu na katika mahojiano nao walikuwa mawazo mbalimbali huku wakikemea vitendo vya aina hiyo.

DK. Valentine Mokiwa:

“Pengine sasa unaongea na marehemu mtarajiwa. Tunatamani sana kukutana na vyombo vya usalama, lakini fursa zilizopo ni ndogo, twende wapi sasa, tukinyamaza tutakufa, tusiponyamaza tutakufa, wakitaka watulinde, wasipoamua wasitulinde, lakini hatuna cha kupoteza,” alisema Askofu Mokiwa.

Dk. Mokiwa alilieleza RAI kwamba, Sheikh Kapungu alitakiwa kuwa wa kwanza kuvisaidia vyombo vya ulinzi nchini juu ya matukio ya mauaji ya viongozi wa dini ya Kikristo yanayoendelea Zanzibar akisisitiza kila alichozungumza katika CD ambayo naye alikiri kuiona ndicho kinachotokea sasa.

“Huyu angekuwa ndio wa kwanza kuhojiwa. Iweje hasira ya tukio la nchi jirani ije Tanzania na yote aliyoyazungumza ndio yameanza kutokea.

“Wakristo sasa angalieni mnachokula, angalieni mapito yenu….hamko salama, lakini kanisa halijamtangaza mtu kuwa adui yake, lindeni wenyewe nyumba zenu za ibada na tusikubali alinde mtu mwingine, sababu hakuna ulinzi, hatulindwi. Kila kichwa cha Mkristo hakipo salama sasa, Mungu alijaalie kanisa katika nchi hii, halitaondolewa na halitafutwa,” alisema Dk. Mokiwa.

Askofu Michael Hafidh:

Katika mahojiano na RAI, Askofu Hafidh anasema; “sasa sio wakati tena wa maombi peke yake. Tunasema tumechoka, haya yanayotokea Zanzibar yamepangwa,” alisema.

Katika mahojiano hayo, Askofu Hafidh anasema mara baada ya kupata taarifa za vitisho vya kuuawa kwa viongozi wa dini ya Kikristo Zanzibar alipeleka taarifa hizo kwa jeshi la Polisi Zanzibar, hata hivyo hakupata ushirikiano.

“Nimezungumza uso kwa uso na Kamishna wa polisi Zanzibar na kumpatia CD hiyo, lakini hakuna alichofanya, nikamweleza asipochukua hatua lazima litatokea jambo kubwa.

“Siogopi najua siku moja nitakufa, nasema wazi sina imani na mfumo mzima wa usalama wa Taifa na jeshi la polisi Zanzibar, wahalifu wamo ndani ya jeshi la polisi.

“Wakristo wa Zanzibar bado tunayo imani kubwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Nchimbi, lakini si kwa sababu yeye ni mkristo mwenzetu, ni kutokana na uwezo wake wa kufuatilia mambo, lakini anaangushwa na polisi Zanzibar,” anasema Askofu Hafidh:

Kardinali Pengo:

“Tukio hili lingeweza kuzuilika, lakini uzembe uliofanywa na vyombo vya usalama kwa kushindwa kufuatilia taarifa zilizofikishwa kwao kupitia, CD na vipeperushi mbalimbali, hasa hasa mara baada ya tukio la siku ya Krismasi la kupigwa risasi, father Ambrose Mkenda,”

“Hili si tukio la dharura, kiasi kwamba watu wetu wa usalama wa Taifa washindwe kuzuia, hili lilijulikana na lingeweza kuzuilika,” anasema Pengo katika mahojiano na RAI.

Askofu Augustine Shao:

“Mara baada tukio la kushambuliwa padri Ambrose na Sheikh Soraga, tulipata ujumbe ukisema, tumewaweza na bado tunaendelea, tunao vijana wa kazi wenye mafunzo waliyoyapata Somalia,” alisema Askofu Shao.

Askofu Shao anasema licha ya kufikisha ujumbe mbalimbali za vitisho kwa jeshi la polisi na uongozi wa juu Ikulu Zanzibar, hakuna kilichofanyika, badala yake walionekana wanataka kueneza chuki za kidini Zanzibar.

“Haturidhishwi na utendaji kazi wa mfumo mzima wa usalama wa taifa na jeshi la polisi Zanzibar kupitia kwa kamishna wake, Mussa Alli Mussa,” alisema Askofu Shao.

Jeshi la Polisi Zanzibar:

Akizungumza na RAI, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Alli Mussa alisema ingawa lawama nyingi zinaelekezwa kwa Jeshi la Polisi, anawalaumu wananchi waishio kwenye eneo alilouawa Padri Evarist Mushi kwamba walifanya uzembe kuchelewa kutoa taarifa za kuwapo watu wasiowafahamu katika eneo lao.

“Unaweza kusikia mengi kwa sasa, lakini licha ya kuwapo vipeperushi vinavyotishia maisha ya viongozi wa dini, wananchi nao wana nafasi yao ya ulinzi miongoni mwao.

“Kwa mfano wauaji wa Padre Mushi walionekana na wananchi wa eneo hilo tangu saa 11 alfajiri wakipitapita, lakini wananchi hawakuwatilia wasiwasi, mpaka tukio lilipotokea,” alisema Kamishna Mussa.

Akizungumzia tuhuma za viongozi wa dini ya Kikristo kwa Jeshi la Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa alisema, baada ya kupokea malalamiko ya viongozi wa dini juu ya tishio la kuuawa, walifuatilia kwa karibu ikiwa ni pamoja na kupekua nyumba za watuhumiwa lakini hawakupata ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.

Kamishna Mussa pia alisema yeye alikuwa hajapata taarifa za kuwapo kwa CD inayohamasisha kuuawa kwa viongozi wa dini ya Kikristo na kusema yeyote aliye na CD hiyo anaweza kuwasilisha polisi.

Kamishna Mussa alisema polisi inaendelea kufanya uchunguzi kubaini iwapo kweli matukio hayo yanahusishwa na ugaidi na kufadhiliwa na baadhi ya jumuiya za nchi za Kiislamu.

“Bado sisi tunasema huu ni uhalifu, Inaweza ikawa ugaidi lakini bado Jeshi la Polisi Zanzibar hatujafikia hatua ya kutoa kauli ya mwisho kuyahusisha matukio ya Zanzibar na ugaidi…ngoja tumalize upelelezi wetu nadhani tutafika pazuri na kutangaza kuwa hili ni tukio la kigaidi, au la,” alisema Kamishna Mussa.

Polisi Makao Makuu

Kama ilivyokuwa kwa Kamishna Mussa, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, ASP Advera Senso naye aliliambia RAI kuwa alikuwa hajapata kuiona au kuisikia CD inayotoa wito wa kuuawa kwa viongozi wa kidini.

“Hatuna taarifa hizo za kuuawa kwa viongozi hao, wamekwambia wewe?, Hebu njoo ofisini tuzungumze kwa undani juu ya hili,” alisema ASP Senso.

Imeandikwa na Rai, Alhamisi, Februari 21, 2013, Na Mwandishi Maalumu

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO