Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA Wazindua Programu ya “MOVEMENT FOR CHANGE” Mjini Arusha

M4C logo CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezindua rasmi programu mpya ya chama hicho inayolenga kuwashirikisha wananchi kuchangia ujenzi wa chama ili kukiwezesha kufikia mabadiliko ambayo chama hicho kinapigania katika siasa zake nchini.

Programu hiyo mpya, “Movement for Change” au M4C kwa kifupi, ilizinduliwa juzi Machi 23, 2012 katika hafla maalumu ya kukichagia fedha chama hicho iliyofanyika katika hotel ya Naura Springs mjini Arusha na kuwakutanisha wapenzi, wanachama, wabunge na viongozi mbalimbali wa chama wakiwemo Mwenyekiti wa Chama Mh Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dr Wilbroad Peter Slaa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbowe alisema kuwa Kamati Kuu ya chama hicho iliketi mwezi uliopita walipokutana Arumeru kupitisha jina la mwanachama wa kupeperusha bendera ya chama hicho, na kuafikiana kukirudisha chama kwa wananchi ili kufanikisha mkakati wa kusitisha utegemezi wa ruzuku toka serikalini, jambo ambalo limekuwa kama karoti ya kuviweka vyama vya upinzani nchini katika utegemezi kwa chama tawala, CCM.

Akisisitiza zaidi, Mbowe alisema, CHADEMA ni chama cha watu, kitasimamiwa na watu na kitaendeshwa na viongozi waliochaguliwa na watu.

“CHADEMA inajengwa na wananchama wake wenye moyo na mapenzi ya nchi yao, ilikuwa hivyo wakati inaanzishwa na itakuwa hivyo (siku zote)’’

Akimzungumzia mgombea wa chama chake katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, Mbowe alisema chama chake kinaamini kiongozi mzuri atatokana na watu na kwamba chama hicho huwa kinachagua viongozi na kuwapima na kuwaandaa kupigania haki na utu wa mtanzania, na kusimamia rasilimali za taifa.

Mh Mbowe alidai kuwa watanzania wamekuwa katika maisha ya woga na uongo kwa muda mrefu ili kuwafurahisha watawala.

“Serikali imekuwa ikiwanyanyasa (watu wanaoonekana kuunga mkono upinzani) kimyakimya. Mpango wa kutishana umepitwa na wakati. Tutaheshimu serikali, tutaheshimu sheria lakini hatutaogopa kupigania haki yetu kwa kuwa Mungu atakuwa upande wetu” alisema.

Akisisitiza zaidi, aliwataka wafanyabiashara waoga waige ujasiri wa Mh Philemon Ndesamburo, mfanya biashara wa Moshi, na mbunge wa Moshi Mjini, na akasema kuwa wao wanatangulia (kupigania haki bila woga) na watakutana mbele ya safari.

Aidha, Mh Mbowe alivishutumu vyombo vya habari nchini hasa vituo vya umma, akitaja kwa majina Daily News, Habari Leo, TBC na Sunday News kuwa vimekuwa vikiwagawa watanzania badala ya kuwaunganisha. Alisema vyombo hivyo vya habari ni mali ya watanzania wote lakini anashangaa kuona watendaji wake wakijiona kama wanawajibu wa kuimarisha chama tawala na kuvinyanyasa vyama vya upinzani.

Uchangishaji

Kwa mujibu wa taarifa za kamati ya maandalizi ya hafla hiyo, iliyokuwa chini ya Uenyekiti wa Susan Lyimo (mb), jumla ya shilingi milioni 150 zilitarajiwa kukusanywa usiku huo kwa wastani wa sh 3.5 mil kwa kila meza ukumbini, kwa watu kutoa fedha taslimu ama ahadi.

Aidha, jumla ya sh 8,684,500/=  zilipatikana kwa njia ya mitandao ya simu (M-PESA, tiGO PESA, na Airtel Money) kutoka kwa watu waliokuwa wakifuatilia hafla hiyo moja kwa moja kupitia Star Tv.

Akizungumza kabla ya zoezi la ukusanyaji michango, Mbunge wa Moshi Mjini na mfanyabiashara, Mh Philemon Ndesamburo ambae kwa yeye binafsi alichangia sh milioni 20, aliwakumbusha watu kuwa wakati wakipigania uhuru (wa Tanganyika) walichanga sumni na kuikomboa nchi kutoka kwa wakoloni.

“Leo tuko huru lakini tunahitaji mabadiliko kwasababu yaliyopo hatuyataki…ili tusisikitike kwanini tumepata uhuru, (badala yake) tufurahie kwanini tumepata uhuru” alieleza Ndesamburo.

Mbunge wa Arusha Mjini nae alipewa nafasi ya kuzungumza na kusema kwa ufupi tu kuwa Arusha itakuwa kitovu cha mabadiliko nchini kama ilivyokuwa kwa Azimio la Arusha.

Uchaguzi wa Arumeru Mashariki

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dr Wilbroad Slaa alishusha tuhuma nzito kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhusika na mbinu chafu za kuhujumu uchaguzi, ambapo alisema chama chake kimekamata mbinu za hujuma kwa mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari na zoezi zima la upigaji kura Arumeru Mashariki linalotarajiwa kufanyika April 1 mwaka huu.

“Tumejipanga kushinda Arumeru. Kwa mara ya kwanza tumekamata mbinu za hujuma na sasa hivi NEC wanagongana wenyewe kwa wenyewe” alisema.

Alisema waligundua kuwepo vituo 55 vya kupigia kura vilivyoongezwa kinyemela, bila maelezo na hakuna vyama vilivyoshirikishwa.

Pamoja na tuhuma kupingwa vikali na Mkurugenzi wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva,  bado kumekuwa na taarifa zinazopishana kutoka kwa maofisa wa tume hiyo.

Akinukuu habari iliyoandikwa na Gazeti la Serikali, Uhuru yenye kicha cha habari “Lubuva amshukia Dr Slaa” kwa madai kwamba tuhuma za vituo hewa 55 ni uongo, alihoji kama tuhuma hizo ni za uongo na yaya si mkweli basi NEC isingetuma maofisa wake kwenda Arumeru kufuatilia.

Dr Slaa alisema kuwa mwanzoni Mkurugenzi wa Uchaguzi huo, (Trasias Kagenzi) alitangaza kuwa hawataweka majina ya wapigakura na kwamba yatawekwa siku ya uchaguzi, jambo ambalo CHADEMA walilipigia kelele na Mkurugenzi huyo kukiri walikosea na kuahidi kurekebisha kasoro hiyo. (tayari majina hayo yakianza kubandikwa tangu juzi)

Alilalamika kuwa kumekuwepo na manyanyaso kwa viongozi wa CHADEMA na kukakamtwa kwa vile wana daftari la wapigakura.

Hata hivyo, Dr Slaa alisema kuwa wamepata barua ambayo inawaruhusu kuwa na hilo daftari kwasababu ni haki yao kisheria, na kuahidi kwamba unyanyasaji wowote hautavumiliwa.

Akihitimisha hotuba yake, Dr Slaa aliwakumbusha askari polisi wajibu wao wa kulinda na kusimamia amani wakati wote wa uchaguzi na kuwataka waache kufanya kazi ya siasa kwa kukipendelea Chama Cha Mapainduzi.

Alitoa angalizo kuwa kama sheria hazitafuatwa katika uchaguzi huo, Arumeru patakuwa katika hali tete  na ndio utakuwa mwanzo wa ukombozi wa Tanzania.

Angalizo hilo lilifuatia taarifa za siri alizodai amezipata kutoka vikao vya ndani vya CCM zikimnukuu mmoja wa marais wastaafu nchini, Bwa Benjamin W. Mkapa akiagiza lazima atangazwe mshindi wa chama chake kwa hali yeyote, na CHADEMA itaenda kudai haki yake Mahakamani.

Hizi ni tuhuma ambazo zinaukabili upande mmoja wa washindani katika uchaguzi huo ilhali uchaguzi wenyewe bado haujafanyika na mshindi kujulikana.

Viongozi na watu wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mbunge wa Iringa Mjini-Mch Peter Msigwa, Mbunge wa Mbeya Mjini- Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana - John Heche, Makamu Mwenyekiti Baraza la Wanawake, Mkurugenzi wa Rasilimali na Mbunge wa Viti Maalumu - Susan Lyimo.

Wegnine ni Mkurugenzi Kampeni na Uchaguzi, Msafiri Mtemelwa, Mkurugenzi Ulinzi na Usalama –Wilfred Lwakatare, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri – John Mrema, Mkurugenzi Fedha na Utawala – Antony Komu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar – Hamad M. Yusuph na Mkurugenzi wa kampeni Arumeru – Mwikabwe Mwita Waitara na Mgombea wa cha hicho Arumeru Mashariki  Joshua Nassari.

Washereheshaji wa hafla hiyo walikuwa ni Ndg Godwin Gondwe, Ndg Salim Mwalimu sambamba na mtangazaji mwenyeji wa Star Tv, Angelo Mwaleko

Pichani: hafla ya chakula cha jioni kwa marafiki wa CHADEMA Kibo Place mapema mwezi huu.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 maoni:

immanuel saro said...

UTI BILA UHURU NI UTUMWA
Ndugu zangu watanzania wote najuwa wengi wenu mnajuwa nini kinacho endelea Arumeru Mashariki nimekuwa nashiriki kikamilifu mwanzo na hadi mwisho nimeona mengi nimejifunza mengi na kwa muda wote bila upendeleo wowote chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA kimefanya kazi kubwa na kitaibuka na ushindi mkubwa kwenye kura hofo yangu kubwa ni kama ifuatavyo
Je sisiemu wako tayari kumwaga damu
je sisiemu mko tayari chadema kuingia ikulu
mimi naamini ndio muda mwafaka kwa watanzani kuwa huru kiukweli hukuna atakee ipingia sisiemu kura na wao wanal;ijuwa hilo nawaomba sisiemu msijaribu kuiba kura kwani tuko tayari kwa kufa na tuko tayari kwa lolote hata tuwe vilema lakini haki ioneka na sio kuonekana tu ionekana ikitendwa
BILA KIFO HAKUNA UHURU

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO