Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Makala: Wanaosubiri kuiona CCM inashindwa kama PDP Nigeria kwa hakika wanaota

 

Na Charles Charles

KUSHINDWA kwa Rais wa Nigeria katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumamosi Machi 28, mwaka huu, Goodluck Jonathan, kumeanza kuwaotesha pia ndoto za mchana baadhi ya watu kwamba eti Chama Cha Mapinduzi (CCM), nacho kitashindwa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu!

Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha upinzani cha Alliance Progressive Congress (APC), Jenerali Muhammadu Buhari alimng’oa Jonathan aliyekuwa akitetea nafasi hiyo kupitia Chama cha People’s Democratic (PDP) na kuwapa ndoto za alinacha baadhi ya watu hapa nchini!

Jenerali Buhari mwenye umri wa miaka 72 sasa anatarajiwa kuapishwa Mei 29, mwaka huu, kuanza kuiongoza nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu kuliko zote barani Afrika.

Ili kuhalalisha ndoto hizo unatolewa mpaka mfano wa mwaka 1991 huko Zambia, wakati aliyekuwa mgombea urais kutoka chama cha upinzani cha Movement for Maltiparty Democracy (MMD) ambaye sasa ni hayati, Frederick Titus Chiluba alipomshinda Baba wa Taifa hilo na mgombea kutoka chama kilichokuwa madarakani cha United National Independency Party (UNIP), Kenneth Kaunda.

Tunaambiwa mfano wa aliyekuwa Rais wa Benin, Jenerali Mathieu Kerekou aliposhindwa na mgombea kutoka chama cha upinzani nchini humo, Nicephore Soglo.

Tunakumbushwa pia mwaka 2002 wakati aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa vyama vya upinzani vya kundi la National Rainbow Collition (NARC), Emilio Mwai Kibaki alipomshinda mgombea kutoka chama cha Kenya African National Union (KANU), Uhuru Muigai Kenyatta kilichokuwa kimetawala kwa miaka 39 na kuking’oa madarakani.

Tunaelezwa kuhusu ushindi wa aliyekuwa mgombea urais wa chama cha Patriotic Front (PF), Michael Satta alipomwangusha aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mpito ya Zambia, Rupia Banda kutoka chama tawala cha MMD, wakati huo.

Unatolewa mfano wa jinsi aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mpito ya Malawi na kiongozi wa Chama cha United Progressive (UPP), Dk. Joyce Banda alivyoshindwa na aliyekuwa kiongozi wa upinzani kutoka Chama cha Democratic Progressive (DPP), Profesa Peter Mutharika.

Pamoja na ukweli huo wote, lakini hatuelezwi namna kiongozi huyo wa sasa alipoifikisha nchi hiyo katika hali mbaya kabisa kiuchumi ndani ya miezi tisa tu. Imefikia mpaka hatua ya kutokuwa na fedha katika Benki Kuu yake zinazotosha angalau kwa matumizi ya wiki tatu tu!

Tunarudishwa nyuma katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwa kuambiwa kuwa wapinzani walipata zaidi ya wabunge 80 kati ya 340 waliopo katika Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo ambalo hata mimi nakubali.

Tunaelezwa kuhusu ushindi wa CCM wa asilimia 79 katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwaka jana na vyama vyote vya upinzani nchini kugawana asilimia 21 iliyobaki.

Hiyo ndiyo mifano inayohalalisha kushindwa kwa CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu. Hiyo ndiyo mifano inayotumiwa na baadhi ya watu wakiwemo waandishi wa habari wenye mapenzi yaliyopitiliza katika genge linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi, maarufu zaidi kwa kifupi cha Ukawa!

Ili kuwachochea hasira zaidi wapiga kura watarajiwa katika kinyang’anyiro hicho cha urais, ubunge, uwakilishi na udiwani, waandishi hao wa habari wanakwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa “kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Mwaka 2014, Tanzania sasa ni nchi ya 159 kati ya 187 duniani kwa umasikini!”

Nakubaliana pia na takwimu hizo kwa vile ni za kweli, lakini sikubaliani kabisa na jinsi zinavyotumiwa kuwa hoja za kutaka kuhalilishia propaganda na uongo dhidi ya CCM.

Sababu kubwa zilizomng’oa Rais Goodluck Jonathan kule Nigeria ni mbili tu: Ya kwanza ni uwepo wa kundi la kigaidi linaloitwa Boko Haram, na pili ni tatizo sugu la rushwa inayoshinda nchi zote barani Afrika!

Hayo ndiyo mambo makubwa yaliyopelekea ashindwe kutetea nafasi hiyo yeye na chama chake hicho cha PDP, vinginevyo angeshinda na kumalizia muhula wake wa pili hapo Mei 29, 2019.

Lakini pia, ushindi mwembamba alioupata Jenerali Buhari kutoka kwa wapiga kura wanaokaribia idadi ya Watanzania wote waliopo hivi sasa, unatokana na kuwahi kwake kuitawala nchi hiyo akiwa Kiongozi wa Kijeshi kuanzia usiku wa kuamkia Januari Mosi, 1984, alipomwangusha Rais Shehu Shagari aliyetarajiwa kuapishwa kwa muhula wa pili wa utawala wake, siku hiyohiyo.

Buhari aliiongoza Nigeria kwa miezi 19 na siku 26 kamili kuanzia siku hiyo hadi usiku wa kuamkia Agosti 27, 1985, wakati naye alipong’olewa kijeshi na Jenerali Ibrahim Badamasi Babangida.

Katika hali hiyo, wapiga kura wa nchi hiyo wamemchagua rais huyo wa zamani kwa sababu wanaujua uongozi wake, lakini pia wamefikia uamuzi huo baada ya awali kumkataa katika chaguzi tatu za mwaka 2003, 2007 na 2011 na sasa alikuwa akigombea nafasi hiyo kwa mara ya nne mfululizo.

Walichagua kile kinachoitwa kwamba “zimwi likujualo halikuli likakwisha”, lakini Jenerali huyo wa jeshi pia ‘amebebwa’ na utekaji, utesaji na mauaji yanayofanywa mara kwa mara na kundi la kigaidi la Boko Haram likiongozwa na Abubakar Shekau.

‘Amebebwa’ pia na rushwa iliyokithiri nchini humo ambapo wananchi wanaamini kuwa atatumia mpaka uzoefu wa kijeshi, ili kupambana na mtandao wa uhalifu huo ambao umekuwa ni sugu kwa Nigeria kushinda nchi zote barani Afrika. Hizo ndizo sababu kubwa zaidi na mbili zilizompa ushindi huo mwembamba.

Wanigeria hatimaye wamechoka kutekwa, kuteswa ama kuuawa kikatili na kundi hilo la kigaidi kila kunapokucha. Walifika mahali wakaamini kwamba jeshi la nchi hiyo ambalo Rais Goodluck Jonathan anayemaliza muda wake wa kutawala Mei 29, mwaka huu akiwa ni Amiri Jeshi Mkuu wa sasa limeshindwa kabisa kudhibiti vitendo hivyo.

Mbaya zaidi ni habari zinazodai kuwa baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali yake wakiwemo Mawaziri, Magavana wa Majimbo na Majenerali wa Jeshi hilohilo ni sehemu ya kikundi hicho, hivyo mara zote wamekuwa wakivujisha siri muhimu za mashambulizi ya kijeshi yanayopangwa ili kukitokomezea mbali.

Wanafanya kama aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Msumbiji na Naibu Waziri wa Ulinzi, Jenerali Sebastiao Mabote alivyokuwa pia ni sehemu ya kikundi cha waasi cha Resistance Nacional de Mozambique (RENAMO), katika miaka ya 1980 kabla hajagunduliwa na majeshi ya Tanzania yalipokwenda huko kuvisaidia vikosi vya serikali ya nchi hiyo mwaka 1987!

Ndiyo maana ili kuondokana na hali hiyo, wananchi wa Nigeria walimnyima kura za kutosha Rais Jonathan na kumpa Jenerali Buhari.

Walifanya hivyo pia kwa sababu katika hotuba zake zote wakati wote wa kampeni zake, Buhari alikuwa akiahidi kwamba kazi yake kubwa ya kwanza akiapishwa tu itakuwa ni kuweka mikakati madhubuti ya kijeshi ya kuwatokomezea mbali Boko Haram.

Wakiangalia uzoefu alionao kama Kamanda na Kiongozi Mwandamizi wa Kijeshi, wapiga kura walio wengi waliona wamchague kusudi awe tena Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo, lengo likiwa kumkabidhi jukumu la kuokoa maisha yao yanayozidi kunyemelewa kila kunapokucha na genge hilo la kigaidi.

Ndiyo maana ninasema ushindi huo wa Jenerali Muhammadu Buhari kamwe hauwezi ukafananishwa kwa namna yoyote ile na juhudi zinazofanywa iwe na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Civic United Front (CUF), National League for Democracy (NLD), NCCR – Mageuzi ama kwa ‘nguvu’ ya pamoja waliyoipa jina la Ukawa.

Hauwezi ukafananishwa kwa namna yoyote ile na kivuli cha kwamba eti chama kilichopo madarakani kimeshindwa na wapinzani, hivyo CCM nayo ianze kutia maji ‘kichwani’ kwake.

Haiwezi kuwa namna hiyo kwa vile kiuhalisi, uchaguzi huo mkuu wa Nigeria kamwe haukuwa wa kisiasa zaidi isipokuwa wa kutafuta amani ‘iliyoporwa’ na Boko Haram.

Mbali na amani, rushwa iliyopo nchini humo nayo kamwe haiwezi ikafananishwa angalau tu kwa asilimia 15 na ile iliyopo Tanzania, Kenya, Liberia, Ethiopia, Togo, Mauritania au Benin na kadhalika!

Kama taifa tajiri zaidi kwa mafuta Afrika, taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu kushinda nchi zote katika bara hili, mamilioni ya wasomi na kuongoza kwa vitendo vya utapeli duniani; Nigeria ndiyo pia inaongoza kwa uhalifu huo wa jinai unaoitwa rushwa barani Afrika.

Pamoja na kuwepo katika viwango tofauti kwa miaka mingi, rushwa nchini humo ilishamiri kiasi cha kuota mizizi hasa wakati wa utawala wa Jenerali Sani Abacha.

Katika miaka yake mitano ya kuwepo madarakani kuanzia mwaka 1993 hadi 1998 alipokufa ghafla mno, Abacha mwenyewe alikuwa kinara wa rushwa akijilimbikizia mabilioni ya fedha nje na ndani na nchi hiyo. Alikuwa rais ambaye kwake uhalifu huo wa jinai ulikuwa ni ujanja wa maisha!

Aliporudi tena madarakani Mei 29,1999 baada ya awali kuwa Kiongozi wa Kijeshi kuanzia mwaka 1975 hadi Januari Mosi, 1980, Jenerali Olusegun George Obasanjo alijitajidi kupambana na hali hiyo katika miaka yake minane mipya ya utawala wake wa kiraia, lakini kwa vile hali ilishakuwa mbaya mno katika kipindi cha Jenerali Abacha kamwe hakuweza kuitokomeza mara moja.

Kustaafu kwake na hasa katika miaka mitano ya utawala wa Jonathan, kwanza akiwa ni rais wa kurithi na hata alipochaguliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2011, tatizo hilo la rushwa lilirejea tena na hali ikawa mbaya kupindukia pale kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kilichoundwa mwaka 2009 kilipozidi kuimarisha ukatili wake.

Ilifika mahali ambapo rushwa ilikuwa kama sehemu ya maisha ya kila siku nchini humo. Ilifika mahali kuwa vitendo hivyo viligeuzwa na kuwa sehemu ya lazima ya maisha ya watu na kuenea kila sehemu kuanzia mijini mpaka vijijini.

Ndiyo maana ulipofika uchaguzi mkuu wa Machi 28, mwaka huu, wapiga kura wa Nigeria waliona wamchague Jenerali Buhari na kumwangusha Jonathan.

Walifanya hivyo kwa sababu aliahidi kupambana kwa nguvu zake zote na kikundi hicho cha kigaidi, kile ambacho kimeongeza vitendo hivyo vya rushwa huku Rais Jonathan akishindwa kukikabili na kutaka eti achaguliwe tena ili aifanye kazi hiyo, ahadi ambayo hata wendawazimu wa kufikiri wasingeikubali!

Mbali kutoka Nigeria, ushindi wa Chiluba nchini Zambia, Methieu Kerekou (Benin), Kibaki (Kenya), Michael Satta (Zambia) ama Profesa Peter Mutharika kule Malawi mwaka jana pia hauwezi kufananisha kwa namna yoyote ile na nguvu za Chadema, CUF, NCCR – Mageuzi, NLD wala Ukawa hapa nchini.

Chiluba kwa mfano alishinda kwa vile UNIP ilikuwa imeshakufa miaka mingi kama chama cha siasa. Kaunda aliyekuwa madarakani tangu mwaka 1964 alikuwa gizani kuhusu ukweli huo.

UNIP ilikuwa imebaki tu ofisini kwake au makao makuu bila kuwepo tena popote au kwa namna yoyote, lakini yeye alikuwa hafahamu kitu chochote!

Alikuwa hajui kwa sababu alikitumia chama hicho kama alama ya kugombea tu urais ili kukidhi matakwa ya kisheria, lakini siku zote alishiriki kinyang’anyiro hicho kama “KK” akidhani kwamba ni maarufu kuliko taasisi hiyo yenyewe.

Hakujua kabisa kuwa chama hicho hakina mashina popote, hakina matawi wala ofisi za kata ila kipo kwa wastani kwenye majimbo, wilaya pamoja na mikoani tu.

Kilikuwa kimeshakuwa sawa na jinsi vyama kama Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP) au NCCR – Mageuzi vilivyo hapa nchini au Civic United Front ilivyo katika upande wa Tanzania Bara huku yeye akiwa hajui!

Aidha, ushindi wa Satta uliokuja kutokana na kifo cha Rais Levy Mwanawasa au wa Profesa Peter Mutharika dhidi ya Joyce Banda kule Malawi pia una sura zake.

Satta alichaguliwa kutokana na chuki za Wazambia baada ya Mwanawasa kumtia misukosuko Chiluba na kuonekana kutokuwa na shukurani kwake.

Ni Chiluba ambaye alimwibua Levy Mwanawasa na kushinikiza ateuliwe kuwa mgombea urais wa chama cha MMD wakati yeye alipokuwa akistaafu mwaka 2001.

Lakini aliposhika wadhifa huo na hasa kipindi kile cha pili akamshtaki kwa makosa ya rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka huku watu wakiamini kwamba alifanya hivyo ili kutaka umaarufu kwamba ni kiongozi anayetetea maslahi yao.

Ndiyo maana alipokufa chama chake kiliondoshwa madarakani katika uchaguzi mkuu uliokuja kufanyika ili kukidhi matakwa ya Katiba. Kiliadhibiwa kwa vile kilionekana kuwa cha kisasi, kile ambacho pia uwepo wake ulitegemea zaidi nguvu ya rais aliyepo madarakani na siyo wanachama waliopo mijini na vijijini.

Mwanawasa mwenyewe alidhani akimtia gerezani Chiluba angekijenga kwa sababu tu wote wanatoka chama kimoja, jambo ambalo wapiga kura walio wengi waliliona na kuamua vinginevyo bila ya kujali kwamba alishakufa.

Katika kuhitimisha makala hii, sasa ninaomba nigusie angalau kidogo sana kuhusu nafasi ya 159 ya Tanzania kati ya nchi 187 ambazo ni masikini duniani.

Jambo ambalo halieleweki hapa ni je; hivi mtu akiwa ni wa 159 kati ya 187 maana yake ni kutoka chini au kutoka juu?

Hata kwa akili ndogo tu ya kawaida ni kwamba, jumla ya nchi ambazo ni masikini duniani ziko 187, halafu kuna ya kwanza kwa kuwa ni masikini zaidi, ya pili, ya tatu, ya nne, ya tano, ya sita, ya saba…ya 100, ya 150 na kisha Tanzania kuwa ni ya 157.

Hivi ubaya wake hapo uko wapi kama inatanguliwa na nchi masikini 156 huku yenyewe ikiwa mbele ya mataifa 28 tu?

Kama ingekuwa inashika nafasi ya 157 kwa utajiri kati ya nchi hizo 187 hapo wote tungesema iko mbali sana, lakini kuwa kwake ya 29 kutoka mwisho katika orodha ya masikini na kutanguliwa na nchi 156, mtu anayesema vinginevyo huyo ana chuki zake mwenyewe au pengine hafahamu kabisa kanuni za kuhesabu.

Ndiyo maana ninasema bila mashaka yoyote kuwa wote wanaosubiri kuiona CCM nayo inashindwa kama PDP kule Nigeria, UNIP na MMD vya Zambia, KANU ya Kenya ama UPP ya Malawi kwa hakika wanaota!

 

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Upanga jijini Dar es Salaam.

Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

 

CHANZO: CCM BLOG

Washirikishe Google Plus

About Ujenzi Connekt

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO