Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

RAIS KIKWETE AHUDHURIA SHEREHE ZA KUMSIMIKA UASKOFU AKOFU SANGU JIMBO KATOLIKI SHINYANGA

 

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu wakati wa ibada ya kumweka wakfu iliyofanyika katika kanisa kuu la Parokia ya Mama mwenye Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga .

---------------------------------

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Jumapili, Aprili 12, 2015 ameungana na maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Shinyanga, kuhudhuria Ibada rasmi ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu mpya wa Jimbo hilo, Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu.

Rais Kikwete amewasili kwenye Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga kiasi cha saa sita unusu mchana kwa ajili ya Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na maaskofu wakuu, maaskofu na maaskofu wasaidizi 38, akiwamo Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Rais wa Mabaraza ya Kipapa na Katibu Mwambata wa Uenezaji Injili Ulimwenguni Askofu Mkuu Protase Rugambwa kutoka Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican.

Askofu Sangu ambaye amewekwa wakfu na kusimikwa kwenye Siku ya Huruma ya Mungu Duniani anakuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga na anachukua nafasi iliyoachwa wazi tokea Novemba 6, 2012, wakati aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo, Baba Askofu Aloysius Balina alipofariki dunia.

Kwa miaka karibu mitatu, jimbo hilo limekuwa chini ya Usimamizi wa Kitume wa Askofu Mkuu Yuda Tadei R’uaichii wa Jimbo Kuu la Mwanza.

Askofu Sangu mwenye umri wa miaka 52 baada ya kuwa amezaliwa Februari 19, mwaka 1963, katika Kijiji cha Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, alipata daraja la upadrisho Julai 3, mwaka 1994. Wakati anateuliwa na Baba Mtakatifu Francesco kuwa Askofu Februari 2, mwaka huu wa 2015, alikuwa na daraja la Mosinyori.

           Akikabidhi Jimbo hilo kwa Askofu mpya, Askofu Mkuu R’uaichii amesema kuwa Jimbo la Shinyanga ni moja ya majimbo makubwa zaidi ya Kanisa Katoliki nchini, likiwa na kilomita za mraba karibu 30,000 na waumini Wakatoliki wanaokaridiwa kufikia 300,000 katika Mkoa ambao idadi kiasi ya wakazi wake bado wanaamini  imani za jadi.

Amesema kuwa Jimbo hilo lina parokia 29, mapadre wa Jimbo 52, mapadre wa Kitawa 18 na hivyo kulifanya jimbo hilo kuwa na jumla ya mapadre 70 na “jeshi kubwa” la watawa 70.

Kwenye sherehe hizo zilizohudhuriwa na viongozi wengi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Ali Lufunga, Askofu Sangu amepewa zawadi ya sh milioni 18, fimbo ya kiuchungaji na ng’ombe 10 wa maziwa na Wakatoliki wa Jimbo hilo.
Rais Kikwete amerejea Dar es Salaam jioni  baada ya kumalizika kwa Ibada hiyo.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akitoa salamu zake za pongezi muda mfupi baada ya kumalizika kwa ibada ya kumweka wakfu askofu mpya wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu katika Kanisa Kuu Parokia ya Mama Mwenye Huruma Ngokolo Mjini Shinyanga.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na maaskofu wa Katoliki muda mfupi Baada ya ibada ya kumweka wakfu askofu mpya wa jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu(wapili kulia pembeni ya Rais) huko Ngokolo mjini Shinyanga leo.

Picha na Freddy Maro

CREDIT: CCM CHAMA BLOG

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO