Mkakati wa kutokomeza unyanyapaa na mauaji ya watu wenye ualbino nchini, uitwao IMETOSHA, jana ulianza rasmi kujitokeza kimataifa baada ya kushiriki katika pambano la kimataifa la kirafiki kati ya nyota wa zamani wa Barcelona na Veterani wa Afrika Mashariki.
Katika mpambano huo wa kimataifa uliochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mkangara, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Said Meck Sadick na maafisa kutoka katika mkakati huo walipata nafasi ya kuongea na wachezaji hao nyota wa Barcelona kuhusiana na dhana iliyoko katika nchi za nje ambako inaaminika Tanzania wanauana wenyewe kwa wenyewe kutokana na imani za kishirikina.
Akiongea baada ya mpambano huo ambapo Barcelona waliibuka washindi, Balozi na muasisi wa mkakati huo unaoelekea na sura ya kizalendo na kitaifa, Bw. Henry Mdimu alisema kulikuwa na haja wachezaji hawa warudi na ujumbe kwao wenye majibu ya maswali wanayojiuliza kuhusiana na mauaji ya albino na kukosa majibu.
"Maneno haya ya kwamba sisi tunauana kwa imani za kishirikina, ingawa matukio mengi yapo kanda ya Ziwa lakini nchi nzima inachafuka kwa hiyo haja ya kusafisha jina la nchi kwa mataifa ya nje ipo na sisi IMETOSHA tumeamua kuchukua jukumu", alisema Balozi huyo ambaye pia ana ualbino.
Mdimu alibainisha kwamba katika mkakati wa kimataifa wameanza kwa kuanzisha tovuti (imetosha.or.tz) ambayo itakuwa ikionesha matukio mbali mbali yanayopinga mauaji na unyanyapaa ili wanaoamini vingine waone kwamba unyanyapaa na mauaji kwa watu wenye ualbino si kitu ambacho watanzania kama taifa wanakifurahia.
Balozi huyo pia alitoa wito kwa kila mtanzania kuuunga mkono mkakati wa IMETOSHA ili katika miaka 20 ijayo kizazi kijacho kiwe na jamii yenye watu wenye ualbino wanaoishi kwa amani katika nchi yao.
Wachezaji wa zamani wa timu ya Barcelona ya Hispania wakiongozwa na Patrick Kluivert (aliebeba mtoto) wakiingia uwanjani tayari kwa kukipiga na timu ya Tanzania Veterans katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa, Jijini Dar es salaam. hadi mwisho wa mchezo, Barcelona ya Hispania ilishinda bao 2-1.
Mchezaji wa zamani wa timu ya Barcelona ya Hispania, Patrick Kluivert akifurahia jambo na Mtoto Sharifa mwenye Ualbino kabla ya kuanza kwa mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Tanzania Veterans uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mkangara (wa pili kulia) akizungumza jambo na Mchezaji wa zamani wa timu ya Barcelona ya Hispania, Patrick Kluivert wakati akiwasalimia wachezaji hao kabla ya kuanza kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Tanzania Veterans, uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam jana.Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Said Meck Sadick.
Sehemu ya Wachezaji wa timu ya Tanzania Veterans na Barcelona wakiwa kwenye picha ya pamoja na Watoto wenye Ualbino mbele ya Bango la Mkakati wa kutokomeza unyanyapaa na mauaji ya watu wenye ualbino nchini, uitwao IMETOSHA.Habari/Picha na Othman Michuzi
0 maoni:
Post a Comment