MARAIS wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) watafanya mkutano maalum mjini hapa kesho kutathmini shughuli za kiuchumi kwa wanachama wa jumuiya hiyo.
Miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele katika mkutano huo ni pamoja na kutathmini hatua iliyofikiwa kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja lililoanza Novemba 2009.
Itifaki ya Soko la Pamoja inaruhusu uhuru wa bidhaa, watu, ajira, huduma pamoja na mitaji kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine au kuishi au kufanya shughuli pasipo vikwazo.
Soko la Pamoja ni hatua ya pili katika ushirikiano wa kiuchumi ndani ya EAC, ikiwa imetanguliwa na Umoja wa Forodha,uliotiwa saini 2005. Hatua ya tatu ni Umoja wa Fedha, uliotiwa saini Kampala, Uganda, Novemba, mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Sekretarieti ya EAC, marais wa EAC pia watapokea marekebisho ya muundo wa kufikia hatua ya Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki, hatua ambayo ni ya mwisho katika lengo kuu la mtangamano wa EAC.
Mkutano huo pia utapitia maombi ya nchi za Sudan Kusini na Somalia kujiunga na EAC. Hata hivyo vyanzo vya habari vinadai kwamba hali ya sasa ya vita katika nchi hizo mbili inaweza kuwa ni kikwazo kwa nchi hizo kukubaliwa maombi yao kwa wakati huu ambao pia maelewano baina ya baadhi ya nchi wanachama yako katika kiwango cha chini.
Lingine ambalo pia mkutano huo unatarajiwa kuwa moja ya agenda zake katika kikao hicho cha siku moja ni hali ya usalama katika kanda hiyo.
CHANZO: MAJIRA
0 maoni:
Post a Comment