Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mawaziri wawili CUF watupwa kura za maoni; Wabunge wengi na wawakilishi wametupwa katika hatua hiyo ya awali ya uteuzi

 Mawaziri wawili wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutoka CUF na wabunge wengine wakongwe wa chama hicho wamepigwa mwereka kwenye kura za maoni za kutafuta wagombea wa nafasi za uwakilishi na ubunge kwa majimbo 50 ya Zanzibar.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa uchaguzi wa CUF, Omary Ali Shehe alisema matokeo hayo ni ya awali.

Walioangushwa ni waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Haji Faki Shaali ambaye ameangushwa katika Jimbo la Mkanyageni, sambamba na mbunge wa jimbo hilo, Mohamed Habib Mnyaa na Naibu Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Haji Mwadini Makame katika nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Nungwi.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali, kura hizo zimewatupa waandishi wa habari waliokuwa wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali akiwamo mtangazaji mkongwe wa BBC, Ally Saleh ‘Alberto’ ambaye ameangushwa na mbunge wa sasa wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ibrahim Mohamed Sanya.

Wengine ni Talib Ussi Hamad wa Mwananchi aliyepata kura 31 katika nafasi ya ubunge Jimbo la Magogoni na kutanguliwa na Juma Kombo Hamad aliyepata kura 106 huku mbunge anayemaliza muda wake Kombo Khamis Kombo akiambulia kura 61.

Mwandishi wa Majira, Mwajuma Juma alishika nafasi ya pili, baada ya kupata kura 11 akiwania nafasi ya uwakilishi jimbo la Amani, ambapo Khamis Rashid Abeid aliibuka kidedea kwa kura 22, huku mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Maua Mohamed Mussa akishika mkia katika nafasi aliyokuwa akiwania ya ubunge wa viti maalumu, Wilaya ya Mjini.

Mtangazaji wa zamani wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), Najma Khalfan Juma alipata pigo mara mbili baada ya kuanguka katika kura za maoni nafasi ya uwakilishi jimbo la Ziwani na nafasi ya ubunge viti maalumu kupitia Wilaya ya Chakechake, Pemba.

Kwa upande wa uwakilishi wa viti maalumu Wilaya ya Mjini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej amepenya kwenye tundu la sindano kwa ushindi wa kura moja, baada ya kupata kura 91, akifuatiwa na Nunuu Salim Rashid aliyepata kura 90 na mtoto wa mbunge wa Mji Mkongwe, Rahma Ibrahim Sanya aliyepata kura 30 huku kura nne zikiharibika.

Mbunge wa Mtambile, Mohamed Abdallah Salim naye ameanguka katika kura za maoni sambamba na mwakilishi anayemaliza muda wake, Mohamed Haji Khalid huku Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Dk Alley Soud Nassor akijitoa kabla ya uchaguzi na nafasi hiyo ya uwakilishi kunyakuliwa na Abdallah Bakar Hassan.

Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi wa CUF kutoka Jimbo la Chonga, Abdallah Juma Abdallah ameanguka katika kura hizo pamoja na mbunge wa jimbo hilo, Haroub Mohamed Khamis huku Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC), Omar Ali Shehe akishinda kwa kura tisa baada ya kumwangusha Mhasibu wa Kampuni ya simu ya Zantel, Ali Bakari aliyepata kura 97.

Kwa upande wa ubunge Jimbo la Chakechake, Yusuph Kaiza Makame ameibuka kidedea kwa kura 84 baada ya kumuangusha Fatma Omar Juma aliyepata kura 83, huku Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Juma Duni Haji akishinda kwa kupigiwa kura za ndiyo baada ya mpinzani wake Ali Juma Khamis kujitoa dakika za mwisho na kupata kura 60 kati ya 61 katika nafasi ya uwakilishi jimbo la Bububu.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui amepita katika kura za maoni nafasi ya uwakilishi jimbo la Mtoni, lakini mbunge, Faki Haji Makame ameanguka.

 

HABARI ZAIDI HAPA

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr TW

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO