Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

UTARATIBU WA UTEUZI WA WAGOMBEA NDANI YA CHADEMA KWA UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA 2015

DSC_9839

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza utaratibu wa uteuzi wa wagombea wake watakaokiwakilisha chama hicho katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka huu.

Aidha, kupitia mkutano na waandishi wa habari, Chadema pia imetangaza namna watia nia wa nafasi mbalimbali watakavyochukua na kurejesha fomu huku pia kikiweka wazi gharama za fomu kwa kila ngazi ya uteuzi yaani udiwani, uwakilishi, ubunge na urais

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Salum Mwalim amesema kuwa utaratibu huo wa uteuzi katika ngazi ya ubunge na uwakilishi utahusisha hatua tatu katika ngazi ya jimbo/wilaya husika na hatua moja katika ngazi ya kitaifa huku ule wa udiwani ukiwa na sehemu mbili katika kata na moja wilayani/jimboni.

“Kupitia mkutano wetu nanyi ndugu wanahabari, tunapenda kuutarifu umma wa Watanzania hususan wanachama wetu, wapenzi na wafuasi wote wenye sifa za kuwania uteuzi kupitia CHADEMA kuwa kwa kuzingatia matakwa ya katiba ya chama na kukuza demokrasia tukilenga kuhakikisha tunapata wagombea waadilifu, wenye uwezo wa kuwatumikia watu na wanaokubalika na wapiga kura, chama kimepanua wigo wa kupata maoni ya uteuzi,”alisema Mwalim.

Akirejea maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya Chama kilichoketi Mei 3 na 4 jijini Dar es salaam, NKMZ Mwalim amesema kuwa chama kimepitisha utaratibu huo utakaotumika kupata maoni na hatimaye kufanya uteuzi wa wagombea watakaosimama kugombea nafasi hizo tajwa kupitia CHADEMA katika ushirikano wa vyama vinavyounda UKAWA.

Mwalim ameutaja utaratibu huo utakaotumika katika nafasi za ubunge/uwakilishi na udiwani, kuwa ni:

Ubunge/Uwakilishi

1. Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo

Mkutano huu utafanyika kwenye kila jimbo la uchaguzi na utafanyika siku moja kwenye eneo moja ambalo ni makao makuu jimbo au eneo ambalo litaamuliwa na vikao vya chama.

Washiriki watatakiwa kuwapigia kura moja wagombea ambao wamejitokeza ndani ya chama na kura hiyo itakuwa ya siri .

NKMZ amesema kuwa wasimamizi wa mikutano hiyo maalum ya kura ya maoni watatakiwa kuwa watu ambao hawana ‘maslahi’ kwenye uchaguzi huo yaani wasiwe wagombea au wasiwe na mgombea ambaye wanamuunga mkono kati ya wanaogombea nafasi hiyo.

Kila mgombea atapewa fursa ya kujieleza mbele ya wapiga kura kwa dakika tano (5) na ataulizwa maswali yasiyozidi matatu kutoka kwa washiriki.

Kura zitapigwa mwishoni baada ya wagombea wote kumaliza kujieleza mbele ya Mkutano Maalum wa Kura ya Maoni , na kila mgombea atakuwa na haki ya kuweka wakala wa kuhesabu kura zake.

Matokeo ya kura hizi yatawasilishwa kwenye Kikao Cha Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya kabla ya kufanya kikao chake cha uteuzi.

Wajumbe wa Mkutano Maalum wa Kura ya Maoni Jimbo/Wilaya :

(i) Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Jimbo

(ii) Wenyeviti wote wa kata za wilaya /jimbo

(iii) Makatibu wote wa kata za wilaya/jimbo

(iv) Makatibu waenezi wote wa kata za jimbo/wilaya

(v) Wenyeviti na makatibu wa Mabaraza yote ya Chama Jimbo/Wilaya

(vi) Wenyeviti wa Mabaraza yote katika Kata za wilaya/jimbo

(vii) Makatibu wa mabaraza yote ya kata katika jimbo/wilaya

(viii) Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji watokanao na Chama kwenye Jimbo.

2. Wagombea kujipigia kura wenyewe

Wagombea wote wapewe fursa ndani ya Mkutano Maalum ya kujipigia kura wenyewe na kila mmoja apige kura tatu, kura moja iwe yake binafsi na kura nyingine mbili atakiwe kuwapigia wagombea wengine waliopo.

Matokeo ya kura hizi pia yatawasilishwa Kamati ya Utendaji na pia Ofisi ya Katibu Mkuu.

3. Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya

Kamati ya Utendaji ya Wilaya /Jimbo itafanya uteuzi wa awali kwa mujibu wa Katiba ya Chama Ibara ya 7.4.10 (q).

Kamati ya Utendaji itatakiwa kupiga kura za awali na kuwasilisha taarifa yake pamoja na Mapendekezo yake kwa Kamati Kuu kwa mujibu wa Katiba ya Chama kwa ajili ya uteuzi mwisho.

Utaratibu wa kuendesha vikao vya Kamati ya Utendaji Jimbo/Wilaya utazingatia Katiba na Kanuni za Chama.

Udiwani

Katika nafasi ya udiwani Mwalim amesema kuwa kuwa utaratibu utakaotumika ni ule ule kama ilivyo katika nafasi ya ubunge isipokuwa hapa itakuwa katika ngazi ya kata kama ifuatavyo;

1. Mkutano Mkuu Maalum wa Kata/Wadi

Wajumbe wa Mkutano Maalum wa Kura ya Maoni kata/wadi:

(i) Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Kata

(ii) Wenyeviti wote wa matawi katika kata

(iii) Makatibu wote wa matawi katika kata

(iv) Wenyeviti wote wa mabaraza ya wazee, wanawake na vijana katika kata

(v) Diwani wa Chama wa Kata/Wadi, Diwani wa Viti Maalum, Mbunge/Mwakilishi anayeishi katika kata husika.

(vi) Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Wenyeviti wa Kamati za Mitaa au Shehiya wanaotokana na Chama katika kata.

(vii) Wenyeviti wa Serikali za Vitongoji, Mitaa na wajumbe wa serikali hizo katika kata wanaotokana na CHADEMA.

2. Wagombea kujipigia kura wenyewe

3. Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya

Mwalim ameongeza kuwa tofauti na kwenye nafasi ya ubunge na uwakilishi ambayo uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Kamati Kuu ya Chama, kwenye ngazi ya udiwani uteuzi utafanywa na Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA.

“Lakini pia hapa kwenye udiwani, mkutano mkuu maalum wa kata ambao utawapigia kura za maoni wanaowania uteuzi wa udiwani, mbali ya kujumuisha wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa, utahusisha pia wajumbe wote wa serikali katika vitongoji, vijiji na mitaa wanaotokana na CHADEMA katika kata husika. Unaweza kuona tunavyopanua wigo wa demokrasia.

“Jambo jingine ambalo tungependa kusisitiza kwa wote watakaojitokeza kuchukua fomu ni kuhakikisha wanazingatia utaratibu wa katiba ya chama, kanuni za uendeshaji chama na miongozo yetu na nyaraka mbalimbali za kiutendaji. Watambue kabisa kuwa kati ya mambo ambayo hatutakubali yatokee kwenye chama hiki ni vitendo vya rushwa kusaka nafasi.

“Tumeshasema na tunarudia tena kusisitiza kuwa watoa rushwa na wapokea rushwa hawana nafasi ndani ya CHADEMA. Tumekuwa wakali katika hili. Yeyote atakayebainika kuvunja kanuni za chama katika zoezi hili ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa hatutakuwa na msalie mtume katika kuchukua hatua stahiki ndani ya chama pamoja na vyombo husika vya kiserikali kuchukua hatua za kisheria,”amesisitiza Mwalim.

Gharama za fomu, utaratibu wa kuzichukua na kuzirejesha

Kuhusu gharama za kuchukua fomu za uteuzi huo, Mwalim alisema kuwa baada ya Kamati Kuu kuamua tarehe za kuchukua na kurejesha fomu za uteuzi wa ndani ya Chama na mfumo mzima wa kuwapata wagombea ilikasimisha mamlaka kwa sekretarieti ya chama kufanya maamuzi na kuidhinisha kutolewa kwa fomu pamoja na gharama zake.

Amesema kuwa sekretarieti ya chama taifa imeelekeza kuwa fomu zitaweza kuchukuliwa eneo lolote lile yaani kwenye ngazi zifuatazo; Taifa, Mkoa, Wilaya na Jimbo kwa upande wa fomu za ubunge na kwa upande wa udiwani fomu zitaweza kuchukuliwa kwenye ngazi ya wilaya, jimbo na kata.

Aidha ameongeza kuwa fomu hizo pia zitapatikana mitandaoni kupitia website ya chama; www.chadema.or.tz, kwa ajili ya wale wote ambao kwa sababu moja ama nyingine wanaweza kushindwa kufika katika ofisi za chama.

Amesisitiza kuwa kuwa fomu hizo ni lazima zirejeshwe kwenye Ofisi ya Jimbo au Kata ambayo mgombea anagombea na ndipo atapaswa kulipia gharama za fomu husika.

Kwa upande wa Ubunge wa Viti Maalum, NKMZ amesema kuwa fomu zao zitalipiwa moja kwa moja kwenye Akaunti ya BAWACHA Taifa ambayo ipo kwenye fomu husika, hivyo wagombea wa nafasi hiyo watalazimika kuambatanisha fomu zao na risiti ya kibenki (Pay Slip) ambayo inaonyesha kuwa wamelipia fomu hizo.

Gharama za fomu hizo ni kama ifuatavyo;

· Urais ni Tsh. 1,000,000/=

· Ubunge/Uwakilishi wa Jimbo ni Tsh. 250,000/=

· Ubunge Viti Maalum ni Tsh. 250,000/=

· Udiwani wa Kata ni Tsh. 50,000/=

· Udiwani wa Viti Maalum Tsh. 50,000/=

Imetolewa leo Alhamis, Mei 14, 2015 na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

CHADEMA

Washirikishe Google Plus

About Ujenzi Connekt

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO