Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Serikali yadhamiria kukamilisha Miradi ya Kitaifa ya Kimkakati

Na Saidi Mkabakuli

Serikali imesema kuwa ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha miradi ya kitaifa ya kimkakati iliyoibuliwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo unaofikia kikomo mwaka ujao wa fedha wa serikali.
Hayo yalisemwa na Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Nagu alisema kuwa mpaka kufikia mwezi machi mwaka huu, serikali imefanikiwa kutandika reli za uzito wa ratili 56.12 kwa yadi kwa umbali wa km 9 kati ya stesheni za Lumbe, Mto Ugalla na Katumba; kukamilisha malipo ya ununuzi wa mabehewa 274 ya mizigo ambapo mabehewa yameshaanza kupokelewa Novemba 2014; kukamilika kwa matengenezo ya njia ya reli iliyoharibiwa na mafuriko katika maeneo ya Ruvu – njia panda ya Mruazi.
Waziri Nagu aliongeza kuwa kwa upande wa Barabara hatua iliyofikiwa ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa kilometa 502.6 za barabara kuu kwa kiwango cha lami dhidi ya lengo la kilomita 560, na ukarabati wa kilomita 78.8 za barabara kuu kwa kiwango cha lami dhidi ya lengo la kukarabati kilomita 131.5. Kwa upande wa madaraja hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na ujenzi wa madaraja ambapo daraja la Kigamboni limefikia asilimia 75, Sibiti asilimia 22, Kilombero asilimia 26, Mbutu asilimia 99, Lukuledi II asilimia 25 na Kavuu asilimia 36.
Katika sekta ya Uchukuzi, Dkt. Nagu aliyataja mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa shehena iliyohudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam kufikia tani milioni 14.3 Machi 2015 dhidi ya lengo la tani milioni 13.0 kwa mwaka 2014/15; kuongezeka kwa ufanisi wa bandari katika kupakua magari kwa kila shifti moja ya saa 8 kufikia magari 886 kwa shifti kufikia Machi 2015 ikilinganishwa na lengo la magari 600 kwa shifti katika mwaka 2014/15; kupungua kwa muda wa meli kupakia na kupakua mizigo bandarini kutoka lengo la wastani wa siku 5 mwaka 2013/14 hadi wastani wa siku 3.7 kufikia Machi 2015; kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa malipo kwa njia ya mtandao mwezi Julai, 2014; na kuanza  kutoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam kwa masaa 24 kwa siku zote za juma. Aidha, kwa upande wa bandari ya Bagamoyo, hatua iliyofikiwa ni kusainiwa kwa makubaliano ya ujenzi wa bandari; na kutangazwa kwa zabuni kwa ajili ya kupata wawekezaji katika bandari za Mtwara na Mwambani -Tanga.
“Katika sekta ya nishati, hatua iliyofikiwa ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam (km 542) Machi 2015, na ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi Madimba (Mtwara) na Songosongo (Lindi) umefikia asilimia 86.9 ambapo unatarajiwa kukamilika Juni 2015. Kwa upande wa usambazaji wa umeme vijijini, wateja wapya 2,602 wameunganishiwa umeme katika mikoa ya Simiyu, Singida, Kagera, Tanga, Ruvuma, na Iringa,” alisema Dkt. Nagu.
Kwa mujibu wa Waziri Nagu, shughuli nyingine zilizotekelezwa nia katika sekta ya nishati, ni pamoja na kukamilika kwa usimikaji wa mitambo 4 ya kufua umeme yenye uwezo wa jumla ya MW 150, kuendelea na ujenzi  wa vituo vya kupoza na njia za kusafirisha umeme, na kuendelea na ujenzi wa  karakana, majengo ya utawala, na barabara za ndani katika mradi wa Kinyerezi I; kukamilisha ulipaji fidia kwa eneo la Makambako katika mradi wa usafirishaji umeme wa Makambako - Songea;  na kuanza ujenzi wa nguzo za njia ya umeme katika mradi wa msongo wa kV 400 wa Iringa – Shinyanga.
Akiwasilisha kazi zilizotekelezwa katika sekta  ya Maji, Dkt. Nagu alisema kuwa ulazaji wa mabomba katika mradi wa maji Ruvu Chini kutoka Bagamoyo hadi Dar es Salaam kazi ambayo imekamilika kwa kilomita 52.43 kati ya kilomita 55.93 za mradi sawa na asilimia 93.8; kwa upande wa mradi wa maji Ruvu Juu: mkandarasi amekamilisha utafiti wa udongo na uchunguzi wa awali wa mahali yatakapojengwa matanki Kibamba na Kimara; na kwa upande wa mradi wa Bwawa la Kidunda,  wananchi wamelipwa fidia ya shilingi bilioni 7 kupisha ujenzi wa barabara na eneo litakapojengwa bwawa.
“Kwa upande wa miradi ya maji vijijini, jumla ya miradi 123 ya maji ilijengwa na kukamilika. Idadi hii imenufaisha wananchi wapatao 463,750 na kuongezeka kwa ufanisi katika masuala ya ununuzi wa huduma katika mikataba kutoka siku 265 hadi siku 90. Aidha, Serikali imeendelea na ujenzi wa mabwawa ambapo bwawa la Iguluba (Iringa) na Wegero (Mara) yamekamilika. Vile vile, ujenzi wa bwawa la Kawa (Rukwa) umefikia asilimia 95, bwawa la Sasajila (Dodoma) asilimia 66.09 na Mwanjoro (Shinyanga) asilimia 45.4,” aliongeza Waziri Nagu.
Katika sekta ya kilimo, Dkt. Nagu aliyataja mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kupatikana kwa hati za mashamba mawili ya Bagamoyo na Mkulazi; maghala 30 yamekarabatiwa na kupatiwa watoa huduma binafsi katika Wilaya za Mbozi na Momba.  Vile vile, skimu 30 za umwagiliaji zimepatiwa watoa huduma binafsi katika Wilaya za Mbarali, Kyela na Iringa; na mafunzo juu ya kubaini na kudhibiti visumbufu, matumizi bora ya maji, utunzaji na matengenezo ya miundombinu ya umwagiliaji na kutumia mwongozo wa uendeshaji skimu za umwagiliaji yametolewa.  Aidha, ujenzi wa maghala 2 katika Wilaya ya Mlele umekamilika.
Vile vile katika sekta ya viwanda, Waziri Nagu alizitaja kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilika kwa ukarabati wa barabara ya Itoni - Mkiu - Liganga na Mchuchuma kwa kiwango cha changarawe ili kuwezesha mitambo kufika maeneo ya Mchuchuma na Liganga; na kuanza uthamini wa mali za wananchi watakaohama eneo la Mchuchuma. Vile vile, fidia shilingi bilioni 53 imelipwa katika eneo la kujenga kituo cha Biashara na Huduma Kurasini; na fidia ya shilingi bilioni 7 imelipwa katika eneo la uwekezaji Bagamoyo na Serikali imesaini mkataba na kampuni ya China Mechants Holding International kwa ajili ya kujenga bandari na eneo la viwanda. Aidha, katika kiwanda cha kuzalisha dawa ya kuua viluwiluwi wa mbu, Kibaha, kazi ya ufungaji wa mitambo na ujenzi wa miundombinu inaendelea na inatarajiwa kukamilika kabla ya Julai, 2015.
Akizungumzia upande wa maendeleo ya rasilimali watu, Dkt. Nagu alisema kuwa kazi zilizofanyika ni pamoja na kuendelea kugharamia wanafunzi 159 wanaoendelea na mafunzo katika fani za mafuta na gesi kwa ngazi mbalimbali za mafunzo ndani na nje ya nchi ambapo wanafunzi 124 wanagharamiwa na Serikali na wanafunzi 35 wanagharamiwa na nchi wahisani; na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vikuu na vyuo vya ualimu, ufundi na ustawi wa jamii.
Kwa upande wa utafutaji wa rasilimali fedha, Waziri Nagu alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania inatumia kanzidata bora inayohifadhi taarifa inayoweza kuthaminisha bidhaa na hivyo kutoa makadirio bora zaidi ya viwango vya kodi. Vilevile, alisema kuwa tozo kwa ajili ya uwekezaji katika elimu umeanza Julai 2013 ikiwa asilimia 2.5 ya mapato ghafi ya kampuni za simu.
“Katika sekta ya fedha, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuongezea Benki ya Maendeleo ya Kilimo mtaji wa shilingi bilioni 60; kuendelea kuongeza mtaji wa Benki ya Rasilimali kufikia shilingi bilioni 212 ambapo mtaji kutoka Serikalini ni shilingi bilioni 152.2 na shilingi bilioni 59.8 zimetokana na malimbikizo ya faida; na  mali za Benki ya Maendeleo ya Wanawake Tanzania ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 26.5 mwaka 2013 hadi shilingi bilioni 34.8 mwaka 2014,” alisema Dk. Nagu.
Kuhusu eneo la huduma za utalii, Dkt. Nagu aliongeza kuwa kazi zilizofanyika ni pamoja na usanifu wa ujenzi wa Utalii House awamu ya pili na kuboreshwa kwa mfumo wa ukusanyaji mapato (utalii, uwindaji na upigaji picha). Aidha, idadi ya watalii kutoka nje iliongezeka kutoka watalii 1,090,905 mwaka 2013 hadi watalii 1,102,026 mwaka 2014. Vile vile mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.81 mwaka 2013 hadi dola za Marekani bilioni 1.98 mwaka 2014.
“Kwa upande wa Biashara, hatua iliyofikiwa ni kurekebisha sheria ya mfumo wa stakabadhi ghalani na kutoa  elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu mfumo huo; kuanzishwa kwa kampuni ijulikanayo kama Tanzania Mechantile Exchange plc kusimamia na kuendesha soko la mazao ya bidhaa na kuhamasisha matumizi ya fursa za masoko ya mipakani, Kikanda na Kimataifa,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Dkt. Nagu maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2015/16 yamezingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16). Aidha, Mpango huu umezingatia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini – MKUKUTA II (2010/11 – 2014/15), Malengo ya Milenia, Mwongozo wa Mpango na Bajeti  kwa mwaka 2014/15; Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2014/15 yaliyojadiliwa na Bunge Novemba, 2014; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2010 – 2015); na sera na mikakati ya kisekta.

Naibu Katibu Mtendaji (Sekta za Uzalishaji) kutoka  Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bw. Maduka Kessy (Kulia) akimpongeza Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Kushoto) mara baada ya kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima.

Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.


Baadhi ya Wabunge wakifuatilia kwa makini hotuba ya  uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima

Baadhi ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16.

















Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO