Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

RAIS MAGUFULI AFUNGUA DARAJA LA KIGAMBONI NA AMSIMAMISHA KAZI MKURUGENZI WA JIJI LA DAR WILSON KABWE.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akikata utepe huku viongozi wengine wakiushikilia kuashiria uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akipata picha ya kumbukumbu viongozi wengine baada ya  uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiteta jambo na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt Ramadhani Dau wakati wa  uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli na viongozi wengine wakitembea juu ya Daraja la Kigamboni baada ya kulizindua katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.PICHA NA IKULU.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 19 Aprili, 2016 amefungua rasmi Daraja la Kigamboni linalounganisha usafiri wa barabara kati Kigamboni na Kurasini Jiji la Dar es salaam na amependekeza Daraja hilo liitwe Daraja la Nyerere (Nyerere Bridge).

Sherehe za ufunguzi wa daraja hilo kubwa na la kipekee kwa Afrika Mashariki na Kati zimefanyika kando ya daraja hilo upande wa Kigamboni na kuhudhuriwa na viongozi na wageni mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. Lu Youqing, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhandisi Edwin Ngonyani, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Mheshimiwa Antony Mavunde, Wabunge na Mameya wa Jiji na Dar es salaam.

Ujenzi wa daraja hilo umehusisha nguzo mbili za pembezoni na mihimili miwili inayoshikilia nyaya 36, na daraja zima lina urefu wa meta 680, upana wa mita 32, njia sita za magari, njia mbili za watembea kwa miguu na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5.

Daraja hilo limejengwa kwa fedha za ndani na kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 254.12 ambapo kati ya fedha hizo asilimia 60 zimetolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), na asilimia 40 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Kujengwa kwa Daraja hili kutaondoa kero ya msongamano wa magari na usafiri kwa wakazi wa Kigamboni na wakazi wa katikati ya Jiji la Dar es salaam ambao walilazimika kutumia kivuko (Ferry) ili kukatiza eneo la mkondo wa bahari ya Hindi ama kutumia barabara ya kuzunguka kupitia Kongowe lenye urefu wa kilometa 52.

Daraja hilo limefanyiwa majaribio kwa kutumia Malori 44 yenye uzito wa tani 30 na limethibitika kuwa na uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,320 na hivyo linatarajiwa kusaidia usafirishaji wa mizigo ya kutoka na kuingia katika bandari ya Dar es salaam.

Akizungumza katika sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza vyombo husika vianze mchakato wa daraja hilo kupewa jina la "Daraja la Nyerere" (Nyerere Bridge) ikiwa ni kuuenzi mchango mkubwa wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefanya kazi kubwa ya kuijenga Tanzania.

Aidha, Rais Magufuli amewapongeza wadau wote waliohusika kufanikisha ujenzi wa Daraja hilo likiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na wakandalasi kutoka China, na ametaka watanzania wajivunie daraja hilo kubwa na lililojenga heshima kubwa kwa nchi.

Pia Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya habari vya Tanzania kuitangaza vyema Tanzania na kuwa na uzalendo wa kweli kwa nchi yao badala ya kubeza kazi nzuri zinazofanywa ndani ya nchi kwa manufaa ya watanzania.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw. Wilson Kabwe na kuagiza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili za kusaini mikataba iliyosababisha serikali kupoteza mapato.

Dkt. Magufuli ametangaza uamuzi huo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa daraja la Kigamboni, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda kumueleza kuwa amebaini upotevu wa shilingi Bilioni 3 uliotokana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw. Wilson Kabwe kusaini mikataba ya ukusanyaji mapato ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kwa kutumia sheria iliyopitwa na wakati, na pia ukusanyaji wa tozo za uegeshaji wa magari ndani ya Jiji.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
19 Aprili, 2016
Washirikishe Google Plus

About SeriaJr TW

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO