Mshehereshaji wa kongamano la siku moja lililofanyika jijini Dar kuzungumzia ukarabati na uendeshaji wa bwawa la Kalemawe lililopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro, Mtaalamu wa masuala ya fedha wa UNCDF, Bw. Imanuel Muro akisherehesha kongamano hilo. Katikati ni mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Same, Herman Kapufi akifuatiwa na Mkuu wa ushauri wa ufundi wa Mfuko wa Umoja wa mataifa wa Ukuzaji Mitaji (UNCDF), Bw. Peter Malika.(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)
Na Mwandishi Wetu
ZAIDI ya watu 10,000 wanaozunguka bwawa la Kalemawe wilayani Same mkoani Kilimanjaro watanufaika na ukarabati wa bwawa hilo na kuwekewa muundo mpya wa kiutawala na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Ukuzaji wa Mitaji (UNCDF).
Bwawa hilo ambalo lipo katika kata za Kalemawe na Ndungu lilijengwa na watawala wa Kiingereza mwaka 1952-1959 kwa ajili ya kusaidia shughuli za kilimo na ufugaji baada ya kuanzishwa kwa hifadhi ya Mkomazi na hivyo wakazi kuzuiwa kwenda katika hifadhi hiyo kwa shughuli mbalimbali.
Taarifa ya kuwepo kwa mradi huo mkubwa, imetolewa na Mkuu wa ushauri wa ufundi wa Mfuko wa Umoja wa mataifa wa Ukuzaji Mitaji (UNCDF) nchini, Bw. Peter Malika wakati akiwakaribisha madiwani wa kata hizo ambao wameitwa katika kongamano la siku moja Dar es salaam kuzungumzia ukarabati na uendeshaji wa bwawa hilo.
Pichani juu na chini ni Mkuu wa ushauri wa ufundi wa Mfuko wa Umoja wa mataifa wa Ukuzaji Mitaji (UNCDF), Bw. Peter Malika (kulia) akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Same, Herman Kapufi kufungua rasmi kongamano hilo.
Malika amesema Mfuko huo wa ukuzaji wa mitaji unasaidia ukarabati wa bwawa hilo kupitia mpango wake wa uendelezaji rasilimali kwa kutumia fedha za ndani (LFI) .
Amesema baada ya ukarabati huo, mradi utaendeshwa kwa pamoja kati ya serikali na watu binafsi.
Malika alisema ukarabati huo unakidhi lengo la mfuko ambalo ni kuwezesha miundombini inayoleta maendeleo.
“Ukarabati na hatimaye uendeshaji wa bwawa hilo kutasaidia kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo ya mitaji kwa watu binafsi na umma.” alisema
Kongamano hilo lililofunguliwa na Mkuu wa wilaya ya Same, Herman Kapufi lilizungumzia masuala ya umiliki, masuala ya kisheria ya taasisi, utawala bora, masuala ya kiufundi ya ukarabati,uvuvi wa samaki wa kibiashara, matumizi ya maji kwa ajili ya umwagiliaji, ufugaji, mabadiliko ya tabia nchi na mazingira, uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake, mfumo wa utoaji wa huduma za fedha na masuala mengi mengine ya mipango ya maendeleo endelevu.
Kapufi alisema kwamba pamoja na kushukuru Mfuko wa Mitaji kukubali kuwasaidia, amesema bwawa hilo ni muhimu sana katika kuondoa migogoro na migongano ndani ya jamii pia na mamlaka ya hifadhi ya Mkomazi.
Alisema kurejeshwa kwa hali yake ya zamani kutasaidia wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa bawawa hilo kama wavuvi wa samaki kila mmoja kuwa na nafasi katika matumizi ya bwawa.
Mkuu wa wilaya ya Same, Herman Kapufi akizungumza kwenye kongamano la siku moja lililofanyika jijini Dar kuzungumzia ukarabati na uendeshaji wa bwawa la Kalemawe lililopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro lililoandaliwa na UNCDF.
Aidha alisema ukarabati utakaofanywa na muundo wa uendeshaji wa bwawa hilo utasaidia wilaya pia kufikiria namna ya kutengeneza bwawa jingine katika Mto Ruvu kwa sababu kama hizo za kuwapa uwezo zaidi wananchi katika maendeleo yao kwa kutumia rasilimali maji.
Toka kujengwa kwake katika miaka ya 1950, bwawa hilo lenye urefu wa takaribani kilomita tatu na upana wa mita 200 limepungua ukubwa wake kwa karibu nusu ya uwezo wa awali kwa sababu za kujaa tope, matumizi mabaya, kukosa ukarabati na usimamizi.
Aidha limeota magugu maji ambayo inaua kizazi cha samaki na kuvuruga uvuvi.
Mkuu wa wilaya ya Same, Herman Kapufi akisisitiza jambo kwenye kongamano hilo lililowakutanisha madiwani wa kata za halmshauri ya wilaya ya Same na wataalam kutoka UNCDF kujadili pamoja kabla ya utekelezaji.
Pichani juu na chini ni washiriki wa kongamano hilo la siku moja ambao ni madiwani wa kata za Same, mainjinia na wakandarasi kutoka halmashauri ya wilaya ya Same pamoja na wataalam kutoka UNDCF.
Washiriki wakitamaza video ya bwawa la Kalemawe lililopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro kujionea hali halisi ya bwawa hilo linalohitaji ukarabati.
Pichani juu na chini ni muonekano wa bwawa la Kalemawe lililopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro wakati UNCDF walipotembelea eneo hilo.
PICHA NA STORI: ZAINUL MZIGE
0 maoni:
Post a Comment