MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, amemshambulia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdurahman Kinana, kuwa ni kiongozi aliyepigwa changa la macho jimboni hapa kiasi cha kujikuta akiingizwa kwenye udhalilishaji na aibu na hivyo kuonekana katika jamii kuwa hafai.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa jana, Lema (Chadema), alisema ziara nyingi za Katibu Mkuu Kinana anazozifanya mikoani zimekuwa ni maigizo na sawa na wachekeshaji katika vipindi vya runinga.
Akizungumzia ‘changa la macho’ alilopigwa, Lema alisema katibu mkuu huyo kwa kutojua aliwapokea wanachama waliofukuzwa Chadema huku akidai bado walikuwa viongozi wa chama hicho.
“Katika mikutano ya ukoo wa CCM ambayo chama hicho hufanya kazi ya ziada kusomba watu kwenye malori kutoka maeneo mbalimbali ili wahudhurie kwa wingi, alikuwa akionekana Kinana akiwapokea wanachama tuliowafukuza uanachama, wakati huo huo akidai kuwa wamewapokea viongozi toka Chadema, haya ni maigizo.
“Ukiona Katibu Mkuu wa CCM anaingia katika udhalilishaji na aibu kama hii maana yake wananchi wanamuona kuwa hafai,” alisema na kuongeza, “jana (juzi) alienda Soko la Kilombero akamkuta mtu anafagia, akaanza kuigiza kwa kufagia kwa lengo vyombo vya habari viweze kumwoshesha.
“Mwenendo wa Kinana unaonyesha CCM kinafanyakazi kama chama kinachoanza leo…ni mambo yasiyoeleweka na sio utawala bora kwa yeye kuwatukana mawaziri wa chama chake hadharani,” alisema.
Alisema Kinana aliyepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya vyama vingi 1995, hana kitu ambacho anaweza kujivunia kwamba alileta maendeleo ya jimbo hili.
Akitoa mifano, Lema alisema Kinana alimpokea aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Monduli aliyefukuzwa, Mchungaji Amani Silanga Mollel, kujiunga na CCM huku akidai kuwa alikuwa bado ni mwenyekiti wa chama hicho.
Alisema ukweli ni kwamba Silanga alifukuzwa uanachama wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema, Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Mkoa wa Arusha Novemba 30, 2013.
Aliongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ngorongoro, Revocatus Palapala, naye alifukuzwa na chama hicho na kuhamia chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT) na baadaye kuhamia CCM na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa wa Kijiji cha Waso, wilayani humo.
Alisema ni ajabu kuona kiongozi mkubwa wa chama akimpokea Palapala kama mwanachama mpya wa CCM aliyeacha wadhifa wa mwenyekiti wa Chadema, wakati ukweli unaonyesha alikuwa ni mwanachama wa CCM.
Aidha alisema aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Chadema, Kata ya Olorien, Godfrey Mfinanga, naye pia alifukuzwa wakati wa uchaguzi wa marudio wa kata nne zilizopo katika jimbo la Arusha Mjini, baada ya kubainika kwamba alikuwa akifanya kazi ya kukisaidia CCM na Cuf katika uchauguzi huo uliofanyika Oktoba 2013.
Lakini alisema alipopokelewa na CCM katika ziara ya Kinana, alitajwa kama mtu aliyetoka Chadema.
Akizungumzia zaidi ziara za Kinana mikoani, Lema alisema mara nyingi amekuwa akiwadhalilisha hadharani mawaziri wa serikali yake pamoja na watendaji wengine huku akijua kwamba anayo fursa ya kuonana na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, na kuyashughulikia masuala hayo kichama na kiserikali.
“Huu ni mwenendo wa Kinana wa maigizo anaoendelea nao nchi nzima, maigizo hayo yameingia Arusha, kitendo chake cha kwenda kwenye mikutano ya hadhara na kuanza kuchambua mienendo ya mawaziri walioteuliwa na mwenyekiti wake kinaonyesha uwezo wake ulivyo…Kinana ni katibu mkuu wa chama, ni mtu mkubwa sana ana fursa zote za kuonana na mwenyekiti wake na hata kuwaita mawaziri katika vikao vya faragha,” alisema.
Akizungumzia madai ya kujimilikisha kiwanja ambacho marehemu Nyage Mawalla, alikitoa kwa ajili ya chama hicho ili kijenge hospitali ya wanawake na watoto, Lema alisema, madai hayo sio ya kweli na upotoshaji.
Alisema kiwanja hicho hajajimilikisha, na utaratibu unaendelea ndani ya chama na wanatarajia kuanza ujenzi kabla ya bunge hili kumaliza muda wake.
“Tumepata wafadhili wa kujenga na makadirio ya awali ya gharama za ujenzi ni dola za Marekani milioni 3.8,” alisema na kuongeza, watajenga pia chuo cha uuguzi.
Kuhusu ujenzi wa Soko la Kilombero, alisema litaboreshwa na kuwa la ghorofa tano hadi nane liwe la kisasa litakaloweza kutosheleza hata wafanyabiashara wa Soko Kuu.
Alisema wamepata kiwanja eneo jirani na Soko la Kilombero hali ambayo itawawezesha sasa kuliboresha soko hilo liwe la kisasa kwa gharama za Sh. Bilioni 25.
“Kinana anakwenda kufanya upotoshaji kwa kudai kuwa sisi tulisema tutavunja soko hilo. Tunataka kuboresha ili wafanyabiashara waweze kufanya shughuli zao katika mazingira bora,” alisema
CREDIT: LIBENEKE LA KASKAZINI
0 maoni:
Post a Comment