Meza kuu katika warsha ya wadau wa ajira kwa vijana iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF. Kutoka kushoto ni Afisa kutoka Wizara ya Kazi na Ajira kitengo cha Ajira, Joseph Nganga, Mkurugenzi wa Kazi katika Wizara ya Kazi na Ajira, Ally M. Ahmed, Mkuu wa utafiti na machapisho Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Fortunata Makene, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel na Mratibu Kazi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Dk. Annmarie Kiaga.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Na Mwandishi wetu
PAMOJA na kuwepo na maendeleo ya kuridhisha katika suala la ajira kwa vijana, serikali imekiri kwamba ukosefu wa ajira bado ni tatizo kubwa duniani na kwa taifa kwa ujumla.
Kutokana na hali hiyo suala la ajira kwa vijana limebaki kuwa ajenda kuu nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kazi katika Wizara ya kazi Ally M. Ahmed wakati akifungua warsha ya siku moja ya wadau wa ajira kwa vijana iliyofanyika hoteli ya Double Tree by Hilton.
Alifanya ufunguzi huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eric Shitindi.
Alisema Tanzania inaendelea kukabiliana na tatizo la ajira kutokana na wigo mdogo wa fursa za ajira, tatizo la utaalamu na ukosefu wa uzoefu .
Alisema hata hivyo vijana wanaoamua kujiajiri wenyewe wamekuwa wakikabiliana na tatizo kubwa la mtaji, maeneo ya kufanyia kazi na utaalamu katika ujasiriamali utakaowawezesha kuendesha miradi wanayoibuni.
Alisema kutokana na uwapo wa sera, mipango na miradi ya maendeleo kuhusu ajira kwa vijana inayoendeshwa kitaifa na kimataifa kumekuwepo na dalili njema za kupungua kwa ukosefu wa ajira.
Alisema utafiti wa mwaka 2014 (ILFS) umeonesha kwamba ukosefu wa ajira umepungua kutoka asilimia 11.7 kwa mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 10.3 ka mwaka 2014 huku kwa vijana (wenye umri wa miaka 15 hadi 35) ukipungua kutoka asilimia 13.2 kwa mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 kwa mwaka 2014.
Mkuu wa Utafiti na mchapishi wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Fortunata Makene akitoa hotuba ya utangulizi katika warsha ya vijana na ajira iliyofanyika hoteli ya Double Tree by Hilton. Katika hotuba yake ya ufunguzi alitoa wito wa washiriki kuangalia kwa undani tatizo la ajira kwa vijana na kutoa mwelekeo utakaosaidia watunga sera kuwa na sera madhubuti kuhusu ajira kwa vijana.
Alisema mafanikio yaliyopatikana hayaondoi ukweli kuwa kuna tatizo kubwa la ajira miongoni mwa vijana na kutokana na mazingira ya sasa ni vyema wadau wa ajira kuangalia kwa undani tatizo la ajira la sasa ili kutoa ushauri wa kukabiliana nalo kwa kipindi kifupi na kirefu.
Shitindi alisema kwamba serikali inafurahishwa na juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali kutafuta majibu ya tatizo la ajira, majibu ambayo alisema yakifanywa vyema yatasaidia sana wataalamu wa serikali kutengeneza sera na kanuni zitakazo kidhi haja.
Alisema ipo haja kwa wachambuzi (watafiti) kuelekeza nguvu zao katika kutafiti soko la ajira ili kusaidia watengeneza sera kuona mahitaji ya soko katika miaka kadhaa ijayo.
Alisema wakati uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 7 kwa mwaka kwa miaka kumi iliyopita ajira zimekuwa haziendi sambamba na ukuaji wa uchumi na hivyo kuleta maswali mengi ya sintofahamu.
Alisema serikali kwa sasa inataka kuhakikisha kwamba inaboresha upatikanaji wa ajira lakini hilo linawezekana kama taasisi zake zinazotengeneza sera na kuweka mipango zinatambua tatizo na kuona namna ya kuliangalia.
Alisema watafiti wana wajibu mkubwa wa kusaidia serikali kuwezesha vijana kuwa na kazi zenye staha kama sera ya ajira ya taifa inavyotaka.
Mkurugenzi wa kazi wizara ya kazi na ajira, Ally Msaki Ahmed, akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira, Eric Shitindi katika warsha ya kitaifa ya ajira kwa vijana iliyofanyika hoteli ya Duble Tree by Hilton. Katika hotuba yake aliwataka washiriki kujadili kwa makini matatizo ya vijana na kutoa suluhu itakayosaidia watendaji kutunga sera na kutoa mwelekeo mpya wa kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema kwa kuangalia ukuaji wa kisekta, sekta ambayo sasa hivi inahitaji watu ndio ambayo haina wataalamu wa kutosha na hivyo ukuaji wa sekta hizo kama za mawasiliano hauendi sanjari na utaalamu uliopo katika soko.
Katibu Mkuu huyo alitoa wito kwa watu binafsi na serikali kuhakikisha kwamba wanakabiliana na vikwazo vya ajira kwa kutoa elimu na taaluma ili fursa zionekane na kutumika ipasavyo.
Alisema tija inaweza kuonekana katika ukubwa wa utaalamu, ubunifu na namna mafunzo yanavyowawezesha wanafunzi kuwa na uhakika na kazi wanazotaka.
Alisema ipo haja kwa wadau mbalimbali kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kwamba vijana wanaingizwa katika soko la ajira na tatizo la ajira linapunguzwa.
Kiongozi Mpango wa ukuaji na ajira wa taasisi hiyo, Shirika la Utafiti ya Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC), Dk. Arjan de Haan akielezea sababu za taasisi hiyo kuunga mkono tafiti kwa ajili ya kusaidia kupatikana ufumbuzi wa tatizo la ajira katika warsha ya ajira na vijana iliyofanyika Double Tree by Hilton hotel.
Katika moja ya maazimio yaliyotolewa na washiriki vijana, walitaka kuwepo na mabadiliko makubwa katika utoaji elimu, ambapo walisema elimu itolewe kwa Kiswahili lakini pia wanafunzi waandaliwe kuwa wabunifu na kujiajiri.
Aidha wametaka kurejeshwa kwa shule za ufundi na shule maalumu kama ilivyokuwa zamani.
Walisema vijana Wanatakiwa kushiriki katika utengenezaji wa sera na kanuni na si kushirikishwa na kutaka matakwa yao yanastahili kuangaliwa na kuzingatiwa ili mtu ajifunze kila anachoona anaweza kukifanya vyema.
Warsha hiyo ya ajira kwa vijana imewezeshwa na IDRC na kuratibiwa na ESRF na mada mbalimbali ziliwasilishwa ambazo zilichambua masuala ya elimu, elimu ya ufundi, changamoto na fursa za vijana katika ajira.
Aidha kulikuwa na mada za majukumu ya serikali na sera katika kuboresha mchakato wa ajira kwa vijana.
Mchumi na Mshauri huru Bi. Mahjabeen Haji akiwasilisha mada kuhusu hali ya ajira kwa vijana nchini katika warsha ya vijana na ajira ilyofanyika hoteli ya Double Tree by Hilton, katika mada yake alielezea mazingira ya ajira ambapo elimu katika sekta zinazokua kwa kasi kama Tehama ni kikwazo kikubwa katika kuwezesha ajira kwa vijana.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akijadiliana jambo na Mkuu wa Utafiti na mchapishi wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Fortunata Makene wakati warsha hiyo ikiendelea.
Mkurugenzi wa Salama Foundation, Shadrack John Msuya akiwasilisha mapendekezo ya vijana juu ya namna ambavyo vipaji, elimu na ubunifu vinavyoweza kutengeneza ajira kwenye maeneo ya Sayansi, Teknolojia, Kilimo na Ufugaji.Moja ya azimio ni kuwa na sera mpya ya vijana yenye mpango mkakati na tafiti zinazotekelezeka katika warsha ya vijana na ajira.
Mshauri mwelekezi katika uanzishwaji na uendelevu wa biashara na maendeleo ya jamii, Gidufana Gafufen akiwasilisha mapendekezo yaliyowasilishwa katika vikundi nini kifanyike ili vijana wapende kilimo katika warsha ya vijana na ajira iliyofanyika katika hoteli ya Double Tree by Hilton.
Pichani juu na chini ni sehemu ya wadau pamoja na makundi ya vijana waliohudhuria warsha ya wadau wa ajira kwa vijana iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF.
Mmoja wa washiriki akitoa maoni kwenye warsha ya wadau wa ajira kwa vijana iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF.
Picha ya pamoja ya washiriki wa warsha ya wadau wa ajira kwa vijana iliyofadhiliwa na Mpango wa Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa kutoka Canada (IDRC) na kuratibiwa na ESRF.
Pichani juu na chini ni wadau kutoka Taasisi mbalimbali walioshiriki warsha hiyo wakibadilishana mawazo.
Mratibu Kazi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Dk. Annmarie Kiaga (kulia) akiteta jambo na baadhi ya washiriki.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifurahi jambo na Mtafiti Mwandamizi ESRF, Dk. Georgina Ole Saibul mara baada ya kumalizika kwa warsha hiyo.
0 maoni:
Post a Comment