Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Uteuzi wa JK wa Makamishna Uchaguzi wazua Mjadala, Wadau Wahoji Kwanini Sasa!?

Rais Jakaya Kikwete.

Uteuzi wa makamishna wawili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni chini ya siku 40 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu, umeibua hisia tofauti, huku baadhi wakidai kuwa usingepaswa kufanyika kipindi hiki.

Uteuzi huo ambao umefanywa na Rais ikiwa imesalia takribani miezi miwili kabla ya kuondoka kwake madarakani, umepokewa kwa hisia tofauti, huku makundi huru ya kijamii yakiukosoa.

Ingawa uteuzi huo upo ndani ya mamlaka ya Rais, lakini kutokana na muda uliobaki kabla ya kuingia utawala mwingine, wakosoaji wanauelezea kuwa hauna tija kwa ufanisi na uchumi wa nchi.

Rais Kikwete aliwateuwa Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mary Stella Longway na Wakili wa Kujitegemea, Asina Omar kuwa makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wakati Victoria Mwakasege aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.

Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa nafasi moja ya Kamishna wa NEC imejazwa na Rais kutokana na kifo cha aliyekuwa mjumbe wa tume hiyo, Jaji Hillary Mkate aliyefariki mwaka 2013, huku Mary Stella ambaye alikuwa katika tume hiyo akiongezewa muda baada ya muda wake kumalizika.

Katika uteuzi huo, Rais Kikwete pia alimteua Naibu Wazari wa Maji, Amos Makalla kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi ilieleza hatua hiyo ililenga kuziba nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wa Makalla, Leonidas Gama anayewania ubunge mkoani Ruvuma.

Pia Rais Kikwete alimteua Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Jordan Rugimbana kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mwamtumu Mahiza aliyehamishiwa mkoa wa Tanga.

Maeneo mengine ya uteuzi uliofanywa na Rais Kikwete ni Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Muhammed Bakari Kambi, aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Shirikishi cha Muhimbili.

Wengine ni Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), Mlingi Mkucha, ambaye awali alikuwa akikaimu nafasi hiyo na Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Tulia Ackson anayekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

WANAHARAKATI WAKOSOA

Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema uteuzi huo unaibua hisia za shaka kwa kuwa walioteuliwa ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema ingawa Rais anakidhi vigezo vya Katiba na mamlaka zake, lakini nafasi kama ya mkuu wa mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Usalama inapokabidhiwa kwa kada wa CCM, inajenga mazingira kwa watawala kujiimarisha dhidi ya upinzani.

Pia, Olengurumwa alisema uteuzi unapofanyika kwa kiongozi aliyeshika nafasi ya Naibu Waziri katika serikali inayomaliza muda wake kwenda mkoa wenye nguvu kubwa ya upinzani ni moja ya sababu za kutilia shaka (uteuzi).

“Sikuona sababu kwa Rais kufanya hivyo, labda kwa nafasi kama za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambazo zilikuwa wazi, lakini ndani ya tume kuna mabadiliko yalifanyika wakaondolewa wazoefu na kuletwa watumishi wapya, sasa kwa kipindi hiki wanachotakiwa kufanya kazi zao wameondolewa, inatia mashaka,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC), Hellen Kijo Bisimba, alisema uteuzi unaofanyika muda mfupi kabla ya Rais kuondoka madarakani, ni matokeo ya Katiba inayompa madarakani pasipo kuwapo ukomo ama taasisi ya kuthibitisha.

“Siyo muda muafaka kufanya uteuzi huo ikizingatiwa kuwa Rais aliyepo madarakani amebakiza siku chache aondoke na atakayekuja atakuwa na utaratibu wake,” alisema na kuongeza:

“Kwa mfano unampeleka mtu mgeni pale NEC ambayo ilianza kazi siku nyingi ikiwa katikati, akajifunze na kwenda sambamba na waliopo siyo kazi rahisi.”

Bisimba alipendekeza kuwapo mabadiliko ya sheria yatakayotoa ukomo wa muda unastahili Rais kufanya uteuzi anapokuwa madarakani.

MHADHIRI AMTETEA

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini, tawi la Dar es Salaam(Tudarco), Danford Kitwana, alisema uteuzi huo, umefanyika kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo.

“Tukiangalia ni kwamba Rais ana mamlaka makubwa kwa mujibu wa Katiba ilivyoelekeza, hivyo haimzuii kufanya uteuzi kwa kadri inavyofaa,” alisema Kitwana.

Mhadhiri huyo alisema kutokana na uteuzi huo kufanyika muda mfupi kabla ya Rais Kikwete kuondoka madarakani, lazima kutaibua hisia hasi kutoka kwa baadhi ya watu.

WASOMI

Prof. wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi, aliukosoa uteuzi huo na kusema una athari za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Prof. Ngowi, taifa linaweza kuingia katika gharama ambazo `zingeokolewa’ endapo Rais ajaye atawaondoa wateuliwa hao kutoka nafasi walizokabidhiwa.

“Kila Rais ana utawala wake, sasa baada ya miezi miwili atakapokuja Rais mwingine na hakuna hakika kama ataendelea na aliowakuta, isingewezekana kusubiri?,” alihoji.

Hata hivyo, Prof. Ngowi alisema huenda uteuzi huo ukaghubikwa na sababu za kiutalawala au siasa zaidi ya kiuchumi.

CUF: TUNA WASIWASI

Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya, alisema uteuzi huo unaweza kusababisha pamoja na mambo mengine, hofu kwa wananchi ikizingatiwa siku chache zimebaki kuelekea uchaguzi mkuu.

Kambaya alisema miongoni mwa hisia za umma ni kuhusu wateuliwa hao kuhusishwa katika mikakati hasi ya kukinufaisha chama tawala wakati wa uchaguzi huo.

“Sioni sababu ya msingi kufanya uteuzi huo maana kama ni muda alikuwa nao wa kutosha na angeweza kufanya hivyo mapema kuliko alivyofanya sasa,” alisema.

Alisema si jambo jema katika ukuaji wa demokrasia kufanya uteuzi wa nafasi muhimu katika muda wa kampeni za uchaguzi huku mtawala akiwa amebakiza siku chache kuwapo madarakani.

CHADEMA: NI JAMBO LA AJABU

Kwa upande wake, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene, alipoulizwa alijibu kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya kiganjani akisema, ‘uteuzi huo ni jambo la ajabu sana.’

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba, alisema madaraka makubwa ya Rais yanachangia kufanya uteuzi usiokuwa na fursa ya kupingwa.

Alisema athari za madaraka makubwa ya Rais zimezungumzwa na wadau mbalimbali wa haki za binadamu wakiwamo wanaharakati, ikipendekezwa kuwapo ‘vyombo’ vinavyodhibiti uteuzi usiokuwa na tija kwa umma.

“Sina shaka na uteuzi wa Rais kwani haya ni mamlaka aliyonayo ambayo ni makubwa na hakuna anayeweza kuingilia, hata pale unapoona wote hao ni watendaji wa kisiasa,” alisema.Lakini Kibamba alisema kama uteuzi huo ungekuwa wa nafasi za kitaalam, ungekubalika kufanyika wakati wowote bila kujali serikali iliyopo madarakani itamaliza lini muda wake.

*Imeandikwa na Salome Kitomari, Hussein Ndubikile, Theonest Bingora na  Christina Mwakangale

CHANZO: NIPASHE

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr TW

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 maoni:

Anonymous said...

Ni mkesha kwenye kituo cha kupigia kura hadi tupate matokeo ya kura tutakazopiga!!!

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO