Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Lowassa: Sina muda wa kujibu matusi ya CCM

MGOMBEA urais wa Tanzania anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa amesema hana muda wa kujibu matusi na kejeli zinazotolewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi yake.

Badala yake amesema anatumia muda uliobaki wa kampeni kutafuta kura kwa wananchi kwa kunadi ilani ya chama chake. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Lowassa aliyeteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameeleza hayo katika mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Mbezi Mwisho, jimbo la Kibamba, jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ameitoa kama mrejesho wa kampeni ya kimkakati inayofanywa na makada wa CCM walioamua kumshambulia wakimtuhumu kuwa hafai urais, ni kapi, fisadi na mgonjwa.

“Sina muda wa kuwajibu. Tukutane kwenye sanduku la kura. Katika siku 48 zijazo, mtaamua juu ya ajira za vijana, afya kama mtaendelea kulala watano watano, mtaamua juu ya elimu yenu ambayo mimi natamani iwe bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu, maslahi ya walimu na viwanda vyenye ajira,” amesema Lowassa ambaye tangu alipoanza kampeni amekuwa akiieleza Ilani ya Uchaguzi iliyopitishwa na UKAWA.

Lowassa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Oktoba 25, na kuzilinda kura kwa sababu tayari anazo taarifa kuwa CCM wamejipanga kuiba kura.

Lowassa alipanda jukwaani

Viongozi walianza kuhutubia saa 11:38 na kumaliza saa 12:10 jioni huku wananchi wakifika viwanjani hapo kuanzia saa 4 asubuhi.

Kulitokea tafrani kidogo pale viongozi wasimamizi wa jukwaa walipoamua kuwaondoa askari tisa wa Jeshi la Polisi waliofika mbele ya jukwaa kabla ya viongozi kwa nia ya kutoa ulinzi. Ilielezwa kuwa viongozi waliona “polisi hawaaminiki.”

Aidha, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyejiunga na Ukawa wiki mbili zilizopita, amesema CCM hawataki kuachia madaraka licha ya kutokubalika kwa wananchi kwa sababu ya kudumaza maendeleo na kukumbatia rushwa na kujikita kumshambulia yeye na Lowassa.

“Nasisitiza watatoka tu, wamebaki na kazi ya kumchafua mgombea wetu na mimi. Lowassa alitoka serikalini miaka minane iliyopita, hata Rais Jakaya Kikwete alisema lililomkuta ni ajali ya kisiasa na kwamba hakuhusika na Richmond. Kwa vile leo ametoka CCM anaonekana ni mbaya,” amesema Sumaye.

Akihutubia jukwaani, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameionya CCM na serikali kuacha kuitumia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhujumu matokeo ya uchaguzi mkuu.

“CCM na serikali wanahofu. Baada ya kumchafua mgombea wetu pia wana mkakati wa kuitumia TRA kuingiza bidhaa mfano mafuta bila kulipa ushuru ili kuyauza na kununulia shahada za kupigia kura,” ametuhumu.

Mgombea ubunge wa jimbo la Kibamba, John Mnyika alitumia fursa hiyo kujinadi akisema Lowassa atakapochaguliwa kuwa rais atahakikisha serikali inapeleka maji jimboni.

Mnyika ambaye alikuwa mbunge wa Ubungo, jimbo linalogombaniwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), Saed Kubenea, alimtaja aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, Dk. Willibrod Slaa kuwa sasa ni adui wa chama hicho.

Amesema Dk. Slaa baada ya kukaa kimya kwa zaidi ya mwezi, tangu Chadema kilipomkaribisha Lowassa kujiunga, ameibuka na kusema chama kimepoteza misingi yake kwa kumpokea Lowassa na kumteua kugombea urais, hatua inayoonekana ni ya makusudi ya kuinua CCM.

“Kuna watu wametoka chooni wameingizwa chumbani… na mwingine ametoka chumba cha Ukawa na Chadema ameenda chooni. Tatizo la msingi adui yetu mkubwa ni CCM. Na sisi tunatangaza atakaeungana na CCM pia ni adui yetu,” amesema Mnyika.

Kubenea amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 25 kumpigia kura Lowassa huku wakikumbuka wanapaswa kuondoa maradhi makuu matatu yaliyotangazwa na Chama cha TANU (Tanganyika African National Union) ambayo ni maradhi, umasikini na ujinga.

“Ili Lowassa aweze kufanya kazi vizuri akiwa rais, lazima tupeleke wabunge wengi wa Ukawa bungeni. Twende tarehe 25 Oktoba kupiga kura huku tukikumbuka maneno ya rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyekaa madarakani kwa miaka 10 bila ya kutuondolea upumbavu na ulofa,” amesema Kubenea.

Mkapa alitoa maneno hayo jukwaani siku CCM ilipozindua kampeni yake kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, alipolenga kumshambulia Sumaye, waziri wake mkuu wakati alipokuwa rais.

Habari kwa hisani ya Mwanahalisi Online

Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO