Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MSIMAMO WA CHADEMA KUHUSU RIPOTI YA KAMATI YA PILI YA RAIS YA KUCHUNGUZA MAKINIKIA


CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)



TAARIFA KWA UMMA -KUHUSU MSIMAMO WETU JUU YA RIPOTI YA KAMATI YA PILI YA RAIS YA “MAKANIKIA”.​


Ndugu wanahabari,

Tumeomba kukutana nanyi katika mkutano huu kwa ajili ya masuala mawili juu ya mjadala wa ufisadi katika sekta ya madini na upotevu wa rasilimali zetu, hasa baada ya kuwasilishwa kwa ripoti mbili za Tume zilizoundwa na Rais kuchunguza mchanga wa dhahabu ulioshikiliwa (Kontena 270).

Masuala hayo tutakayoyazungumza leo yatajikita katika;

1. Kuweka kumbukumbu sawa

2. Nini kifanyike (wayfoward)


1. Kuweka kumbukumbu sawa

Ndugu waandishi wa habari, ninyi mtakuwa sehemu ya mamilioni ya Watanzania ambao ni mashahidi kwa namna ambavyo Chama chetu-CHADEMA kwa takriban miaka 20 na zaidi tumekuwa tukiwaongoza Watanzania kupigania na kudai haki, maslahi na matakwa ya taifa letu katika kulinda rasilimali za taifa yakiwemo madini.


Watanzania wote wanajua namna ambavyo wabunge wetu pamoja na uchache wao, walipaza sauti kubwa kupinga Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Fedha ya Mwaka 1997 ambayo ulifuta kodi kwa makampuni ya kigeni hususan yaliyopewa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini nchini.
Mwaka 1998 Serikali ya CCM ilipopeleka mswada Bungeni kwa ajili ya kutungwa Sheria ya Madini, Chama chetu na wabunge wetu tulisimama imara kupinga ‘utaasisishwaji na urasimishwaji’ huo wa uporaji wa rasilimali za Watanzania.
Mwaka 2007, Chama chetu kilifanya ziara nchi nzima kuamsha ari na hamasa ya Watanzania kuhoji usiri wa mikataba na kudai mikataba yote ijadiliwe Bungeni kabla ya kusainiwa. Tulitaka sheria zote za madini zirekebishwe ili zilinde maslahi ya Watanzania na wawekezaji kwa maana ya ‘win-win situation’ (Buzwagi saga –baada ya Mbunge wetu Zitto Kabwe kufukuzwa Bungeni kwa kuhoji mkataba wa Buzwagi -uliosainiwa Hotelini –Magufuli alikuwa Waziri na alikaa kimya)
Wakati huo wa mapambano hayo, Serikali ya CCM pamoja na viongozi wao (wengine wako madarakani bado) na wabunge wao walikuwa wakituzomea na kutubandika majina ya kila aina, wakitetea uporaji wa rasilimali za Watanzania bila huruma .
Agenda ya kutetea rasilimali za nchi, ikiwemo sekta ya madini na nishati, tumeifanya kuwa ni agenda muhimu katika chaguzi zote, hasa kupitia kwa wagombea wetu wa Urais mwaka 2005, 2010 na 2015.
Ndiyo maana hatujashangazwa na mapendekezo ya Kamati ya Pili ya Rais John Magufuli kuhusu makinikia kwa sababu ni kama imehamisha tulichokiandika kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015-2020 (uk 57-59) iliyonadiwa na wagombea wetu wote, kuanzia Mgombea Urais, Wagombea Ubunge na Udiwani .
Hata tukio la hivi karibuni lililotokea Bungeni ambapo wabunge wetu; John Mnyika, Halima Mdee na Esther Bulaya walipewa adhabu kinyume cha kanuni za Bunge na sheria za nchi, ilikuwa inahusu mapambano haya haya ya kulinda rasilimali zetu, lakini CCM walikuwa upande wa kutetea uporaji.

2. NINI KIFANYIKE

Tumemfuatilia kwa makini Rais Magufuli katika hiki anachotaka kuonesha kuwa ameanzisha kitu kipya, tangu wakati wa Ripoti ya Kamati yake ya Kwanza kwenye makinikia na Ripoti ya Kamati ya Pili iliyosomwa juzi;

Tumemsikiliza kwa makini alichokizungumza katika matukio yote mawili ya kukabidhiwa ripoti hizo. Tumefuatilia mijadala mikali inayoendelea na tumesikiliza maoni ya Watanzania mbalimbali katika suala hili.

Kwa sababu CHADEMA tumekuwa viongozi katika suala hili, tukiiongoza na kuielekeza na kuishauri CCM na Serikali yake ambao wamekuja kuuona ukweli baada ya miaka takriban 20 ya machozi, jasho na damu ya Watanzania, tunasema yafuatayo;

2.1 Serikali ya CCM iwaombea radhi Watanzania na iwe tayari kuwajibika kwa kuwaongoza vibaya Watanzania kiasi cha kuporwa rasilimali zao kwa miongo hii yote.CCM kama chama cha siasa kijitafakari kama bado kina uhalali wa kisiasa kuendelea kuwepo madarakani .

2.2 Kila aliyehusika katika kutaasisisha na kurasimisha wizi na uporaji huu awajibike au awajibishwe kwa mujibu wa sheria hata kama ni mkubwa kwa kiwango gani.

2.3 Rais Magufuli hatafaulu vita hii kama Serikali yake itaendelea na utamaduni wa kutubagua na au kutosikiliza sauti za upande wa pili, ni vyema akajua kuwa hata Ilani ya Chama chake uk.26..28 haikuzungumzia kabisa hoja za mikataba na sheria za madini kuhitaji kurekebishwa au kuandikwa upya .

2.4 Tumeshangazwa sana na kitendo cha Rais Magufuli wakati ametoka kuomba taifa liwe pamoja katika vita ya kutetea rasilimali zetu, hapo hapo anajenga na kuimarisha mawazo ya uadui dhidi ya watu wenye maoni tofauti, tena anatoa maagizo kwa mihimili mingine (kinyume na sheria na misingi ya utawala bora) kushughulikia watu ambao mawazo yao mbadala ndiyo yamesimamia vita hii muda wote yeye na wenzake wa CCM walipokuwa wakitetea uwekezaji huu na wawekezaji hawa kwa kuwatungia sheria zinazowasaidia kutupora na kutia mikataba ya siri kupora rasilimali za Watanzania.

2.5 Rais Magufuli kama kweli anataka uwazi katika vita hii ni vyema sasa Bunge likawa Live ili watanzania waweze kuwaona na kuwajua wabunge na vyama vyao ambao ni mawakala wa uporaji wa rasilimali za Taifa letu na waweze kuwahukumu katika chaguzi zijazo.

2.6 Rais asiulize mchawi aliyeturoga wakati inajulikana kuwa chama chake ndicho kimetufikisha hapa kwa kulea na kulinda unyonyaji huu.

2.7 Mabadiliko yoyote yanayotarajiwa kufanyika mbali ya kuweka uwazi katika mikataba na kubadili sheria, yanapaswa pia kulenga kufumua ‘status quo’ ili kuweka mifumo na taasisi imara zitakasosimamia uwajibikaji na maslahi ya taifa dhidi ya mtu au kikundi chochote.

2.8 Dhamira ya kweli ya Rais Magufuli katika mapambano haya , hasa kuweka uwazi mikataba inayoingiwa kwa siri kati ya Serikali ya CCM na wawekezaji isiishie kwenye mikataba ya madini pekee, sasa tunataka mikataba yote iwekwe hadharani ikiwemo ya sekta ya ujenzi, uuzwaji wa nyumba za Serikali, kuuzwa mashirika ya umma nk ili tuweze kunusuru rasilimali za Taifa letu;

2.9 Ni vyema watanzania wakaelezwa ukweli juu ya “haki yetu kwa mujibu wa sheria na mikataba ”ambayo CCM na serikali waliingia na wawekezaji hawa kwani hata kama ni kweli kuwa Makanikia haya yana thamani kubwa kiasi hicho cha Matrilioni yaliyotajwa , sisi kama taifa tunatakiwa kupatiwa asilimia nne (4%) tu na wawekezaji asilimia 96% , japo huu ni ukweli mchungu ambao Rais na serikali yake anatakiwa awaeleze watanzania .


3. HITIMISHO

Sisi kama chama cha siasa tunamtaka rais azitoe hadharani ripoti zote za Makanikia kwani kuna maswali mengi sana ambayo hayana majibu juu ya jinsi ambavyo sampuli zilichukuliwa, utaratibu uliotumika katika maabara kwenye kupima sampuli husika na njia iliyotumika kufikia hitimisho la kiwango cha dhahabu na madini mengineyo yaliyoko kwenye mchanga husika.



Aidha , kama ni kweli kuwa Makanikia yana thamani kubwa kiasi hicho (trilioni 108 kiwango cha chini) , hivi dhahabu ambayo tumeshauza kama taifa tangu mwaka 1998 ina thamani ya kiasi gani ? na sisi kama Taifa tumepata kiasi gani?


CHADEMA , tunaamini kuwa ili kupata suluhisho la kudumu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa , ni vyema sasa tukarejea kwenye hoja ya ‘KATIBA YA WANANCHI’ ambayo iliweka mapendekezo ya jinsi ya kulinda rasilimali za taifa (Rasimu ya Warioba).



Tunataka kuona hatua kwanza na sio pongezi ambazo zinaambatana na kauli tupu zisizokuwa na vitendo , maana tulishapewa maneno mengi sana bila hatua , kama vile aliyepitisha Kontena zaidi ya 2,000 bandarini tulisikia maagizo ila mpaka leo hatujui limeishia wapi,Geji ya mafuta Bandarini hakuna hatua ,watanzania kuficha pesa, hakuna hatua na mengineyo mengi.

Imetolewa leo tarehe 16 ,Juni 2017
Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO