Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

ICC yabisha hodi Tanzania

Banner

*Jumla ya vifo 200 vya raia vyasababisha

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) yenye makao yake makuu, The Hague, Uholanzi inatafakari uwezekano wa kuiingiza Tanzania katika orodha ya nchi zinazopaswa kuchunguzwa kutokana na makosa ya uhalifu wa kijinai, Mtanzania limebaini.

ICC ambayo bado haijafikia uamuzi wowote kuhusu hatima ya Tanzania, imeeleza msimamo wake huo katika barua yake ya Novemba 27 mwaka huu iliyoituma kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Taasisi hiyo huru ya kimataifa ambayo tayari imeibua mizozo ya kisheria na kisiasa katika mataifa kadhaa ya Kiafrika imeandika barua hiyo ikijibu barua ambayo ilitumwa kwao na LHRC miezi miwili iliyopita.

LHRC ilituma barua ICC Oktoba mwaka huu, ikilalamikia kile ilichokieleza kuwa ni kukithiri kwa matukio ya raia kuuawa na baadhi ya maofisa za taasisi za dola, wakiwamo askari polisi katika kipindi cha kati ya mwaka 2004 na sasa.

Kwa mujibu wa barua hiyo, iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uchunguzi cha Mpelelezi Mkuu wa ICC, M.P. Dillon ambayo MTANZANIA imeiona, uamuzi wa ama kuiingiza Tanzania katika uchunguzi huo wa makosa ya uhalifu wa kijinai au la utafikiwa iwapo mambo kadhaa yatatekelezwa.

Dillon katika barua hiyo anayataja mambo ambayo yanaweza yakasababisha uchunguzi huo kuanza kuwa ni pamoja na iwapo itathibitika kwamba makosa yanayopaswa kufuatiliwa yanaangukia katika kifungu cha 53 cha Mkataba wa Rome, uliosababisha kuundwa kwa ICC yenyewe.

Barua hiyo pia, inayataja masuala mengine katika orodha hiyo kuwa ni pamoja na uzito wa makosa yenyewe na iwapo taasisi za dola zinachunguza na kuchukua hatua zozote za kimashitaka dhidi ya watu wanaohusishwa na makosa husika.

“ICC inatafakari hali ya mambo kutokana na barua mliyoituma kwa kutumia barua na taarifa nyingine zilizopo. Chini ya kifungu cha 53 cha Mkataba wa Rome, Mwendesha Mashitaka (wa ICC) anapaswa kuangalia iwapo kuna sababu za msingi za kuamini kuwa makosa yaliyofanywa yanaangukia katika wigo wa mamlaka ya mahakama hii,” anasema Dillon katika barua yake hiyo.

Ingawa katika barua yake hiyo, Dillon anasema taasisi yake hiyo itachukua hatua ya kuyatafakari masuala hayo kwa haraka, anatahadharisha kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwa kazi hiyo kuchukua muda mrefu kabla ya kukamilika.

Hatua hiyo ya ICC inakuja wakati tayari uchunguzi wa namna hiyo umepata kuleta mitikisiko mikubwa katika katika mataifa mengine ya Kiafrika kama Kenya, Liberia na Ivory Coast.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Hellen Kijo Bisimba alieleza kuridhishwa na hatua hiyo ya ICC.

“Tunashukuru kuona barua yetu imepokelewa, tumeahidiwa kwamba kazi ya kuanza mchakato huu itaanza, baada ya kupitia madai yetu tulioainisha.

“Kama mnakumbuka kumekuwapo na matukio mengi ambayo raia wanauawa na vyombo vya dola kama vile jeshi la polisi, lakini kila tunapopiga kelele hatuoni kama Serikali inachukua hatua, zaidi ya kukaa kimya.

“Tunasubiri wapitie kwa kina madai yetu, tunataka kuona hatua zinachukuliwa ipasavyo, tunasikitika mno kuona hakuna utawala wa sheria,” alisema.

Akizungumzia tukio la kuuawa kwa polisi wawili katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Bisimba alisema kituo hicho kinalaani vikali tukio hilo.

“Tulipokea kwa mshtuko taarifa za kuuawa askari Koplo Paschal na Private Alex, hatupendi kuona wananchi wanajichukulia sheria mkononi.

“Tunapenda kuikumbusha jami na serikali kuwa, hali hii ni ya hatari kubwa kwa jamii na taifa kwa ujuimla, kwa sababu matendo haya ni doa kubwa katika dhana ya polisi jamii iliyoasisiwa na IGP Saidi Mwema.

“Hivyo tunatoa pole kwa jeshi la polisi, lakini tunaitaka serikali ichukue hatua kali dhidi ya wale wote waliohusika katika tukio hilo la kinyama na matukio mengine ya aina hii,” alisema.

Alisema mauaji ya raia wasiokuwa na hatia yamekuwa yakiongezeka, kwani mpaka sasa watu karibu 200 wameuawa.

“Takwimu zinaonyesha, mwaka 2004 watu wanne waliuawa, mwaka 2005 watu 36, mwaka 2006 watu 37, mwaka 2008 watu 14, mwaka 2008 watu watano, mwaka 2009 watu 17, mwaka 2010 watu 52 na mwaka 2011 watu 28.

“Watu hawa, wameuawa katika matukio mbalimbali kama vile kupigwa risasi migodini, kushambuliwa na askari wakidhaniwa ni mtuhumiwa wa ujambazi,

“Haya yote ni mauaji yanayotokana na ukosefu wa uadilifu ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na sababu kuu mbili, kwanza ni kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani jeshi la polisi lenyewe, mahakama na vyombo vingine, nawananchi kukosa imani na vyombo hivyo na kuamua kujichukulia sheria mkononi.

Imechapishwa na Mtanzania, Jumatano, Desemba 19, 2012 06:10 Na Gabriel Mushi, Dar es salaam

MUENDELEO WA STORI HIYO NI HUU HAPA

SERIKALI imesema inasubiri nyaraka za Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), ili kujibu tuhuma ambazo mahakama hiyo imedai inatafakari kuanza kuichunguza Tanzania, kutokana na makosa ya uhalifu wa kijinai.

Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alisema taarifa kuhusu madai ya ICC bado hazijawasilishwa rasmi serikalini.

Alisema ingawa kumekuwapo na taarifa kuhusu mahakama hiyo kuandika barua ya kujibu madai hayo, kwa upande wa Serikali haiwezi kujibu chochote kwa sababu haijapokea taarifa rasmi.

“Tunasubiri documents (nyaraka) kutoka kwenye hiyo mahakama, ili tujue namna ya kujitetea… kwa sasa siwezi kusema chochote, kwa sababu hatujapokea barua yoyote,” alisema.

“Kama mnavyojua Serikali haiwezi kukurupuka tu, bali inakwenda kwa vielelezo,” alisema kwa kifupi na kukata simu.

Juzi MTANZANIA ilipata nakala ya barua kutoka ICC, iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uchunguzi cha Mpelelezi Mkuu wa ICC, M.P.Dillon, ambayo MTANZANIA imeiona, uamuzi wa ama kuiingiza Tanzania katika uchunguzi huo wa makosa ya uhalifu wa kijinai au la, utafikiwa iwapo mambo kadhaa yatatekelezwa.

Dillon katika barua hiyo, anayataja mambo ambayo yanaweza yakasababisha uchunguzi huo kuanza kuwa ni iwapo itathibitika makosa yanayopaswa kufuatiliwa yanaangukia katika kifungu cha 53 cha Mkataba wa Rome uliosababisha kuundwa kwa ICC yenyewe.

Barua hiyo, inayataja masuala mengine kuwa ni pamoja na uzito wa makosa yenyewe na iwapo taasisi za dola zinazochunguza na kuchukua hatua zozote za kimashtaka dhidi ya watu wanaohusishwa na makosa husika.

“ICC inatafakari hali ya mambo kutokana na barua mliyoituma kwa kutumia barua na taarifa nyingine zilizopo, chini ya kifungu cha 53 cha mkataba wa Rome, Mwendesha Mashtaka wa ICC anapaswa kuangalia iwapo kuna sababu za msingi za kuamini kuwa makosa yaliyofanywa yanaangukiwa katika wigo wa mamlaka ya mahakama hii,” anasema Dillon katika barua yake hiyo.

Ingawa katika barua yake, Dillon anasema taasisi yake itachukua hatua ya kutafakari masuala hayo kwa haraka, anatahadharisha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kazi hiyo kuchukua muda mrefu kabla ya kukamilika.

Hatua ya ICC, inakuja wakati tayari uchunguzi wa namna hiyo umepata kuleta mtikisiko mkubwa katika mataifa mengine ya Kiafrika kama Kenya, Liberia na Ivory Coast.

Takwimu zinaonyesha, mwaka 2004 watu wanne waliuawa, mwaka 2005 watu 36, mwaka 2006 watu 37, mwaka 2008 watu 14, mwaka 2009 watu 17, mwaka 2010 watu 52 na mwaka 2011 watu 28.

Watu hao waliuawa katika matukio mbalimbali kwa kupigwa risasi migodini, kushambuliwa na askari wakidhaniwa ni watuhumiwa wa ujambazi.

Huku baadhi ya watumishi wa sekta mbalimbali ikiwamo ya habari, wakishambuliwa na askari na kuuawa.

Mojawapo ya tukio la aina hiyo, lililochafua sura ya Tanzania ni kuuawa kwa mwandishi wa habari wa Kituo cha televisheni cha Chanel ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.

Mwangosi aliuawa kinyama na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakati polisi walipokwenda katika Kijiji cha Nyololo kutawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mwangosi aliuawa majira ya saa 10 jioni, katika ofisi za CHADEMA, huku askari mmoja akijeruhiwa vibaya kwa risasi.

MAUAJI YA MOROGORO
Tukio jingine la mauaji ni lile lilitokea mkoani Morogoro, ambapo polisi walimuua kwakumpiga risasi Ali Zona, aliyekuwa kwenye sehemu ya kufanyia biashara.

LHRC

Oktoba mwaka huu, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kiliandika barua ya kuishtaki Serikali kwa ICC pamoja na Umoja wa Mataifa (UN), kutokana na matukio hayo yaliyokithiri nchini, huku Serikali ikiendelea kukaa kimya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Hellen Kijo Bisimba alisema tayari ICC imejibu barua yao kuhusu madai hayo.

Alisema ICC ilijibu barua hiyo wiki mbili zilizopita na kuahidi kuanza kufanyia uchunguzi madai yaliyoainishwa na kituo hicho.

“Kuhusu suala hili, tayari ICC wametujibu na kutuhakikishia kuwa imeanza kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo.

“Kwa sababu kama mnakumbuka kulikuwapo na matukio mengi ambayo raia waliuawa na vyombo vya dola kama vile jeshi la polisi, lakini kila tulipopiga kelele tukaona Serikali imeendelea kukaa kimya.

“Sasa tunasubiri uchunguzi huo ufanyike, ili hatua zianze kuchukuliwa, lakini pia tunasubiri majibu ya mashirika mbalimbali ya UN, vivyo hivyo kwa sababu tatizo kubwa tunaloliona hapa nchini, hakuna utawala wa sheria,” alisema.

ICC ambayo bado haijafikia uamuzi wowote kuhusu hatima ya Tanzania, imeeleza msimamo wake huo katika barua yake ya Novemba 27 mwaka huu, iliyotumwa kwa kituo hicho.

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uchunguzi cha Mpelelezi Mkuu wa ICC, M.P. Dillon imebainisha kuwa, ICC imeamua kuingiza Tanzania katika uchunguzi huo wa makosa ya uhalifu wa kijinai.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO