CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeutangaza mwaka 2013 kuwa ni wa kumtegemea mungu katika kufanikisha mikakati yao ya kuwatumikia Watanzania. Kauli ya CCM, imekuja siku chache baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuutangaza mwaka huo kuwa ni mwaka wa kutumia nguvu ya umma, kuisimamia Serikali ili itekeleze hoja za msingi za wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba, alisema mwaka 2013, utakuwa ni kufanyakazi ya kuzisimamia Serikali zake kama njia ya kupima utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.
Alisema sababu ya CCM, kumtegemea Mungu, inatokana na kuwepo kwa mipango mizuri na madhubuti ambayo huwa chini ya uratibu wa Mungu.
“CHADEMA wamekuwa na lugha zenye ndimi mbili katika nchi hii, eti hivi sasa wanasema kuwa mwaka 2013 utakuwa ni mwaka wa vurugu kwa kutumia nguvu ya umma. CCM kwa kuwa tunajua wajibu wetu kwa Watanzania, tunasema tutatumia nguvu ya Mungu kuwatumikia wananchi wetu, ambao wameamini Serikali yetu na kuipa dhamana ya kushika dola.
“Na wakati wao, wanadai kutumia nguvu ya umma na hata kuutangaza ni mwaka wa nchi kutotawalika, sisi kwetu CCM tunasema ni mwaka wa kumtegemea Mungu katika kulinda amani ya nchi yetu.
“Mwaka 2012, ni wazi hakuna asiyejua CCM tulikuwa na uchaguzi wa ndani ya chama na sasa, tunapenda kuutangazia umma kuwa, sasa tunaekelea kufanya kazi.
“Kila siku tumekuwa tukiwasikia na hata kuwaona wakiwahamasisha wananchi kutochangia shughuli za maendeleo, bali wapo tayari kufanya michango kwa ajili ya kuchangia chama chao huku tunawashuhudia wakichangisha fedha wakiwa mahotelini, kwenye mikutano yao na hata katika runinga.
“Fedha hizi, baada ya kuchangishwa haziendi kwa ajili ya kufanya maendeleo ya Watanzania, bali zinakwenda kwenye familia yao. Ukiona fedha hazina bajeti kwa maana ya mapato na matumizi, ujue hizo ni za familia, kwa hali hiyo hakuna anayeweza kwenda kwenye familia hizi, ambapo fedha hupelekwa na kuhoji zimetumika vipi.
“Wakati wakihusika nalo viongozi hawa wa ngazi za chini kwa upande wa Sekretarieti ya Taifa, itagawanyika katika kanda ambapo kuna watakaokwenda kanda ya Kusini, Magharibi na Kanda ya kati,” alisema Nchemba.
Akizungumzia hukumu iliyotolewa na Mahakama ya rufaa iliyompa ushindi Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Nchemba, alisema ni dalili tosha kuwa CCM kuheshimu misingi ya sheria na utawala bora.
“Kilichotokea katika hukumu ya Lema, ni dalili ya wazi kwetu CCM kuwa tunaenzi na kuheshimu misingi ya utawala bora.
“Inashangaza sana eti walidai Ikulu ilikuwa inaingilia kesi hii, CCM haiko hivyo… hoja ilikuwa ni hiyo hukumu iliyotolewa mita chache ilipo Ikulu, sasa jambo hili limedhihirisha kauli za uongo zilizokuwa zinatolewa na CHADEMA.
Chanzo: Mtanzania, 25/12/2012
0 maoni:
Post a Comment