Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Jeshi la Polisi lajeruhi mwandishi kwa risasi; Wajikanganya wakidai wanasaka majambazi

JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, limeingia kwenye kashfa baada ya askari wake kumjeruhi kwa risasi mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Shabani Matutu, akiwa nyumbani kwake.

Matutu alizingirwa na baadhi ya askari nyumbani kwake eneo la Kunduchi Machimbo jana majira ya saa 3:30 usiku katika kile kilichodaiwa ni operesheni ya kupambana na majambazi, na akiwa kwenye hekeheka za kujitetea, alijikuta akipigwa risasi kwenye bega la kushoto.

Tukio la kujeruhiwa kwa Matutu, linakuja wakati tasnia ya habari ikiwa bado na kumbukumbu ya kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi mwenzao wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, aliyelipuliwa kwa bomu na askari polisi kijijini Nyololo akiwa kazini.

Matutu ambaye alijeruhiwa pia kiganjani

kwa risasi hiyo, alilazimika kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili huku akiwa na risasi mwilini, hadi jana asubuhi alipofanyiwa upasuaji wa kuiondoa.

Katika hatua ya kushangaza, jana Jeshi la Polisi lilitoa taarifa huku likishindwa kueleza mazingira halisi ya tukio hilo, na badala yake kujaribu kumkingia kifua askari wake aliyefyatua risasi hiyo kwa madai kwamba alishambuliwa kwa panga na Matutu.

Akisimulia tukio hilo, Matutu alisema kuwa akiwa amelala chumbani na mkewe, walisikia sauti ya mtu nje akimwita mkewe kwa jina la Mama J ambapo alimuamsha mkewe na kumueleza aende akamsikilize aliyekuwa akimuita.

Alisema wakati mkewe akiwa anaelekea mlangoni kufungua, alimtaka mtu aliyekuwa akimuita ajitambulishe ni nani, lakini hakufanya hivyo.

“Wakati mke wangu anajiandaa kwenda kufungua mlango, nikasikia sauti za watu wengi wakiongea nje ya mlango na sauti zilikuwa za wanaume, ikanibidi nimzuie asiende,” alisema.

Matutu aliongeza kuwa, wakati akimzuia mkewe asiende kufungua mlango, aliamka na kuchukua panga lake kwa ajili ya kujihadhari na watu hao, kisha akafungua mlango, lakini kabla hajamaliza kuufungua, alishtuka kuona mlango ukisukumwa kwa nguvu ndipo naye akajitahidi kuzuia hali hiyo.

Alibainisha kuwa wakati akiwa katika jitihada za kuzuia mlango usifunguliwe, alimulikwa na tochi yenye mwanga mkali usoni na kisha kusikia kishindo cha bunduki jambo lililomfanya aamini kuwa mkewe ameuawa na mlipuko wa kishindo hicho.

“Sikujua kuwa ni mimi ndiye niliyejeruhiwa, nilipomuona mke wangu yupo salama nami damu zikiwa zinanitoka ndipo nikabaini kuwa aliyejeruhiwa ni mimi,” alisema.

Matutu aliongeza kuwa, baada ya kubaini amejeruhiwa yeye, aliwauliza askari wale sababu ya kufanya ukatili huo dhidi yake, ndipo wakamwambia wanamtafuta Mama Juma.

Alisema kuwa aliwauliza kama aliyenaye ndiye wanamtafuta, wakasema hapana huku wakitaka kumtoa risasi iliyokuwa mwilini mwake, lakini akawakatalia.

Matutu alidai kuwa baada ya kuwakatalia kumtoa risasi hiyo mwilini, aliwaomba wampeleke kupata matibabu huku akitumia fursa hiyo kuwasiliana na baadhi ya ndugu na jamaa zake kuwapa taarifa ya kilichompata.

Hali ilivyokuwa Mwananyamala

Katika Hospitali ya Mwananyamala, askari waliomfikisha Matutu hapo, walionekana wakifanya jitihada za kila namna kutaka waandishi waliofika hapo wasiweze kupata taarifa za kina kwa kuwaeleza kuwa wamuache mgonjwa ashughulikiwe na daktari.

Wakati mgonjwa alipopewa uhamisho wa kwenda Hospitali ya Muhimbili, askari hao walitaka litumike gari lao ambalo halikuwepo, hali iliyomfanya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda kupinga na kutaka litumike la kwake.

Lakini polisi hao walikataa wakieleza kuwa usalama wao utakuwa mdogo kutokana na silaha walizobeba na lilipofika gari lao, lilimchukua Matutu hadi Muhimbili na kumuacha pasipo kutoa maelezo ya namna atakavyopata matibabu.

Kauli ya Kamanda wa Polisi

Hata hivyo, katika hali ya kutia shaka, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alizungumzia tukio hilo akisema Matutu alijeruhiwa baada ya kuanza kumshambulia askari kwa panga.

Alimtaja askari huyo aliyemjeruhi Matutu kuwa ni mwenye namba F. 8991 D/C Idrisa, na kueleza kuwa akiwa na wenzake walifika nyumabni kwa mwandishi huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuwa, kuna majambazi sugu waliojificha humo.

“Askari huyo aliyekuwa na wenzake wanne, baada ya kujeruhiwa alirukiwa na huyo aliyemkata panga na katika purukushani hizo, risasi moja ilifyatuka kutoka kwenye silaha aina ya bastola aliyokuwa nayo na kumjeruhi Matutu bega la kushoto,” alisema Kenyela.

Mashuhuda

Taarifa ya Kamanda Kenyela ilipingwa na baadhi ya mashuhuda wa eneo la tukio, akiwemo msamaria mwema aliyetoa taarifa polisi za kuwepo kwa hisia za uhalifu eneo hilo.

Mashuhuda hao walidai kuwa askari hao walielekezwa chumba cha mwanamke waliyemtaja kwa jina la Mama J ambaye ndiye walikuwa na wasiwasi juu ya mwenendo wake.

Walisema hata baada ya kuelekezwa, askari hao hawakufuata maelezo hayo na badala yake wakaenda kugonga chumba cha Matutu pasipo kuwa na kiongozi yeyote wa eneo hilo.

“Tunachojua sisi katika mazingira kama yale, wangeenda kwa mjumbe, lakini hawakufanya hivyo na hata chumba walichokwenda si kile tulichowaambia,” alisema mmoja wa mashuhuda.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, alisema baada ya tukio la mwandishi kupigwa risasi, mtuhumiwa Mama J alijitokeza, lakini askari hao wala hawakumgusa.

Wahariri wanena

Nalo Jukwaa la Wahariri kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Neville Meena, lilisema kuwa tukio hilo ni baya na linaleta ukakasi hata kulisikiliza, hasa kwa namna Jeshi la Polisi linavyojitetea.

Alisema mara kwa mara walipokuwa wanapiga kelele juu ya utendaji wa jeshi hilo, baadhi ya wananchi walifikiri kuwa walikuwa wanawaonea na hawakustahili kusemwa kuwa, hawana weledi wa kazi yao.

Aliongeza kuwa, ni vigumu kuamini kama askari waliotekeleza unyama huo walikuwa na nia nzuri ya kutaka kumkamata mtu wanayemdhania kuwa ni muhalifu akiwa mzima.

“Mimi ninapenda watu watambue kuwa hao ndio polisi wetu, na huo ndio weledi wao wa kufanya kazi ulipofikia, hakuna faraja yoyote ya kukutana na polisi na ukawa unajiamini kama upo salama,” alisema Meena.

Stori na Abdallah Khamis, Tanzania Daima

 Mwandishi wa habari wa Kampuni ya Free Media inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Shaaban Matutu akionesha jeraha lililotokana na kupigwa risasi na Polisi katika tukio lililotokea usiku wa kuamkia leo - baada ya polisi kuvamia nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es Salaam kwa madai ya kumtafuta mtuhumiwa waliyekuwa wakimsaka. Matutu kwa sasa amelazwa Hospitali ya Muhimbili katika Kitengo cha Mifupa (MOI) kwa ajili ya matibabu zaidi.

 Shabaan Matutu akionesha sehemu ya mkono wake wa kulia ambao ulipata majeraha wakati polisi walipotumia nguvu kuingia chumbani kwake na kumtwanga risasi iliyompiga upange wa kushoto wa kifua chake.

Daktari aliyekuwa zamu katika Hospitali ya Mwananyamala akiangali picha ya X-Ray ya Matutu mara baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo na kufanyiwa kipimo hicho, kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Wafanyakazi wa Free Media, Khadija Kalili (kushoto) na Maria Kayala (kulia) ambao walifika Hospitali ya Mwananyamala baada ya kupata taarifa za tukio hilo wakiwa na Matutu.

(Picha / Maelezo na Dande Francis kwa msaada wa Global Publishers Ltd)

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO