Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

PAPER’ YA ESTAER WASIR KATIKA KONGOMANO LA MIKA 51 YA UHURU WA TANGANYIKA LILILOFANYIKA UDSM JANA KUHUSU “AMANI NA UTULIVU WA TANZANIA KWA MIAKA 50 IJAYO”


Na Esther Wasira
ester
Mabibi na Mabwana,
Mada yangu imegawanyika katika sehemu kuu nne.
(a) Kwanza nitazungumzia kwa nini Tanzania ni nchi ya amani na utulivu.
(b) Pili kama mambo yaliyoipa Tanzania amani bado yanazingatiwa.
(c) Changamoto mpya za amani ya Tanzania.
(d) Mwelekeo wa amani na utulivu wa Taifa letu kwa miaka 50 ijayo.
Kwa nini Tanzania ni nchi ya amani na utulivu?
Mtafiti mmoja kwa jina Ilana Kessler katika utafiti wake wenye kichwa cha habari “What Went Right in Tanzania: How Nation Building and Political Culture have Produced Forty Four Years of Peace, 2006 (Walsh School of Foreign Service of Georgetown University) katika uk. 2 anasema:
“Pamoja na kuwepo sababu ambazo zingeweza kudhoofisha amani ya Tanzania kama vile umaskini, ukosefu wa kazi hasa kwa vijana, uwepo wa makabila mengi (zaidi ya 120) kuwepo dini kuu mbili (Ukristo na Uislam) na kupakana na nchi zenye vita, bado Tanzania imebaki kuwa nchi ya amani na utulivu”.
Mtafiti huyu anajiuliza, Tanzania ilifanya miujiza gani kuweza kujenga taifa moja lenye amani na utulivu? Kwa hiyo tunakubaliana kuwa amani tuliyonayo Tanzania si kwamba imekuja tu kimiujiza au si kwamba binadamu wanaoishi Tanzania ni tofauti na wale wanaoishi Rwanda, Burundi, DRC, Kenya Uganda, Sudan, Somalia nk. Tanzania tunafanana na nchi nyingine zilizotuzunguka na hata tuna uhusiano wa damu na mataifa hayo. Hivyo ni ukweli kuwa kuna kitu waasisi wa Taifa hili walikifanya kuweza kujenga amani na utulivu.
Wakati naandaa mada hii, ilinibidi kuisoma katiba na itikadi ya TANU, Azimio la Arusha, maandiko mbalimbali ya Mwalimu Nyerere pamoja na tafiti mbalimbali kuhusu amani na utulivu Tanzania pamoja na utamaduni wa kisiasa Tanzania. “Political Culture”. Baada ya kusoma hayo yote pamoja na maoni yangu binafsi, sababu zilizojenga amani ya Tanzania ni kama ifuatavyo:-
Zipo sababu nyingi sana lakini kwa maoni yangu zipo sababu kuu mbili:
(i) Sera safi na itikadi sahihi ya TANU na ASP
(ii) Utekelezaji wa sera na itikadi.
Naomba nisisitize neno ‘utekelezaji’ maana kama tutakavyoona, sera safi na itikadi sahihi hazina maana kama hakuna nia wala uwezo wa kutekeleza sera hizo.
(i) Sera safi na itikadi sahihi ya TANU na ASP
Katiba ya TANU inaeleza wazi kuwa TANU iliamini pamoja na mambo mengine, katika:-
• Binadamu wote ni sawa.
• Kila mtu ana haki ya kuheshimiwa utu wake.
• Kila mtu ana haki ya kumiliki mali asili ya taifa kwa niaba ya vizazi vijavyo.
• TANU iliamini katika serikali kuzuia mtu mmoja kumnyonya mwingine au kikundi fulani cha watu kuwanyonya wengine. Hivyo TANU walipania kujenga jamii yenye usawa na haki.
Malengo ya TANU yalikuwa kama ifuatavyo:-
• Kuzitumia rasilimali za nchi kwa ajili ya kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi.
• Kuhakikisha serikali inaondoa aina zote za unyonyaji, vitisho, ubaguzi, hongo/rushwa na ufisadi.
TANU pia ilikuwa na miiko ya uongozi. Kikubwa katika miiko ya uongozi ni kuwakataza viongozi wa umma kutumia nafasi zao kujilimbikizia mali. Ikumbukwa kuwa Azimio la Arusha lilikuwa ni azimio la kutekeleza sera safi na itikadi sahihi ya TANU.
Azimio la Arusha lilikuwa ni azimio lililoleta haki, usawa, utu, uwezo wa kufanya maamuzi kuhusu rasilimali zetu na lilikuwa ni azimio la ukombozi kutoka katika makucha ya mabeberu na wanyonyaji.
Kwa ujumla, sera za TANU zilijenga jamii yenye usawa, haki, umoja na upendo. Kwa mfano, Watanzania walifanywa kuwa jamii moja na kila mtu alikula jasho lake. Hakuna aliyeruhusiwa kumnyonya au kumdhulumu mwenzake.
Kikubwa zaidi, serikali ilikuwa haina mzaha katika kutekeleza sera na maazimio iliyopitisha. Kwa mfano, serikali ilikuwa haina mzaha katika kupambana na rushwa. Rushwa ilionekena kuwa ni adui wa haki na kila mwanachama wa TANU aliapa kutotoa wala kupokea rushwa. Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba zake alisema serikali ilikuwa haina utani katika kupambana na rushwa. Tumesimuliwa na wazee wetu kuwa hata mtu aliyekuwa anakunywa bia kila siku, kuna watu walikuwa wanahesabu vizibo ili kuangalia kama idadi ya bia alizokuwa anakunywa inalingana na kipato chake. Nyerere hakuwa anawapigia magoti wala rushwa kuwaomba waache kujihusisha na rushwa. Hotuba zenye maneno “wala rushwa tunawafahamu hivyo tunawaomba waache” hazikuwa kwenye kamusi ya viongozi wa serikali.
Chini ya uongozi wa Mwalimu, swala kama kuweka fedha kwenye mabenki ya kigeni, mikataba mibovu, ukwepaji kodi nk. yalikuwa yanashughulikiwa kwa nguvu zote. Vyombo vya upelelezi na usalama vilikuwa na uzalendo na pia vyenye dhamira ya kuchunguza na kuwakamata mafisadi na wahujumu uchumi.
Katika suala la usawa na haki, kila Mtanzania alifanywa kuamini kuwa Tanzania ni nchi yake. Serikali ilitoa elimu bure na kwa usawa, ilitoa huduma za afya bure na ilijitahidi kutoa huduma nyingi za jamii bure. Naambiwa hata watoto wadogo walikuwa wanapewa maziwa bure. Serikali ilikuwa na dhamira ya kujenga jamii moja hivyo pamoja na rasilimali za nchi kuwa chache, bado serikali iliweza kutoa huduma kwa haki.
(ii) Sababu ya pili ni utekelezaji makini wa sera, itakadi na maazimio. Kwa mfano kwa kuwa serikali ilikuwa haina mzaha kwenye vita dhidi ya rushwa, tofauti ya kipato kati ya masikini na matajiri ilikuwa ndogo sana. Kumiliki mali na hasa kama mtu hawezi kueleza amezipataje na kama pia kipato kilichomuwezesha kupata mali hizo amekilipia kodi, ilikuwa ni hatari kubwa kwa mtu huyo.
Kwa hiyo unapokuwa na jamii kama hii inayojali haki za wanyonge, inayopiga vita unyonyaji, inayopiga vita rushwa, isiyowaogopa mafisadi, isiyokuwa na matabaka yanayotokana na baadhi ya watu kuwanyonya watu wengine, inayoongoza kwa maslahi ya wanyonge nk hutegemei kuona fujo au vita zinazuka baina ya watu hawa. Maana fujo au vita vinasababishwa na baadhiya watu kujiona wanatengwa katika uongozi wa nchi na pia katika kufaidi matunda ya uhuru.
Mtafiti Ilana Kessler katika utangulizi wa kazi yake anasema. “Sera zilizoanzishwa baada ya Azimio la Arusha zilijenga utamaduni wa kisiasa ambao ulileta amani. Anasema sera za uchumi zilizingatia usawa, zilipinga migawanyiko ya kijamii, zilizingati ujenzi wa taifa na zilijenga utaifa, uzalendo, utambulisho wa kitaifa na ziliwafanya watanzania wajivunie utaifa wao “national pride”.
Hivyo, kwa ufupi hayo ndio yametujengea taifa letu, taifa ambalo kila siku kwa kujua au kutojua tunaimba kuwa ni taifa la amani na utulivu au kisima cha amani.
Je, mambo yaliyoipa Tanzania amani Tanzania bado yanazingatiwa ?
Kama nilivyosema hapo juu, Azimio la Arusha lilikuwa Azimio la utu, haki, usawa, uzalendo na utaifa. Sote tunajua baada ya kuanguka ukuta wa Berlin, tulilazimika kufuata mfumo mpya wa uchumi. Tunajua kuwa Azimio la Arusha lilifutwa na serikali ya awamu ya pili na badala yake wakapitisha Azimio la Zanzibar. Nimejaribu kulitafuta Azimio la Zanzibar katika maktaba zetu na nakiri sijaliona na wala sijawahi kuliona.
Lakini watu wenye akili hawawezi tu kusema kuwa Azimio la Arusha halifai au limepitwa na wakati. Kuna mwanafalsafa mmoja anasema ‘ukitaka kuvunja uzio, jiulize kwanza ni kwanini uzio huo ulijengwa’.
Baada ya kulisoma na kulitafakari nakiri katika historia ya Tanzania, hatutakaa tupate azimio bora kama Azimio la Arusha. Watu wenye akili wangeweza tu kubadili baadhi ya mambo ili kwenda na wakati ila msingi wa Azimio ungebaki. Kwa mfano, tungeweza kubadili mfumo wa kumiliki mali ili watu binafsi wamiliki mashirika ya umma pamoja na migodi kwa ushirikiano na serikali. Nini kilitushinda kwa mfano kuhakikisha Benki ya NBC inamilikiwa na serikali au watanzania binafsi kwa asilimia 49% ?. Kwa kweli Benki ya Taifa ya Biashara, NBC ya zamani ndio ilikuwa nembo ya kazi alizofanya baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Benki hii ilikuwa na matawi nchi nzima na kwa wakati huo ilikuwa ni moja ya Benki kubwa Barani Afrika. Kuambiwa na Benki ya Dunia kuwa ilikuwa kubwa mno na hivyo igawanywe na iuzwe, ilikuwa ni upuuzi kama alivyowahi kusema Mwalimu. Mbaya zaidi Benki hii iliuzwa kwa bei ya kutupwa, tunaambiwa iliuzwa kwa shilingi bilioni 15, bei ambayo haitoshi kulinunua jengo la makao Makuu ya NBC. Hadi Mwalimu anakumbana na mauti, alikuwa anaililia NBC na inasemekana alienda kuonana na maafisa wa Benki ya Dunia na IMF kulalamikia kitendo cha kulazimisha NBC iuzwe. Cha ajabu maofisa wa Benki ya Dunia walimshangaa Mwalimu kwani walimwambia mapendekezo ya uuzaji wa Benki hiyo yalitolewa na Serikali ya awamu ya tatu na wala sio Benki ya Dunia. Hata katika hotuba zake nyingi, Mwalimu alikuwa anapiga sana kelele kuhusiana na uuzwaji wa NBC.
Mwalimu huko ulipo tunakuahidi, kizazi hiki cha vijana hakitaacha hata jiwe moja kufunuliwa na wale waliohusika kuhujumu jitihada za serikali yako za kuijenga NBC na mashirika mengine ya umma, siku moja wataletwa mbele ya sheria. Mwalimu tunaahidi pia, wale wote waliouziana nyumba za serikali kwa bei ya kutupwa wakati nyumba hizo zilikuwa ni jasho lako na la Watanzania wengine hawataachwa wafaidike kwa hujuma hiyo. Maana ukweli ni kwamba mashirika ya umma na nyumba za serikali zilijengwa kwa jasho la wakulima wa pamba, kahawa, tumbaku, korosho nk. Lilikuwa ni jasho la wafanyakazi wa viwandani, walimu, madaktari nk. Ni kwanini jasho letu sote wagawane wajanja wachache ? Hiyo haikubaliki hata kidogo. Naomba nionyeshwe mkulima wa pamba pale Kijiji cha Manyamanyama Bunda aliyefaidika na uuzaji wa nyumba za serikali na mashirika mengine ya umma.
Ukiachilia mbali umiliki wa mali, ni mwendawazimu pekee atakayesema kuwa misingi ya usawa, haki, uzalendo, utaifa na ujenzi wa taifa zilizojengwa na TANU hazitufai tena. Baada ya kulipuuza Azimio la Arusha, leo hii kuna mambo ambayo yanafanyika na ambayo yasipoangaliwa yatatufanya tuharibu amani yetu.
(i) Rushwa : Rushwa ya Tanzania inatisha. Rushwa katika taasisi za umma na katika chaguzi hasa za Chama Tawala si siri tena. Rushwa pamoja na kwamba ni adui wa haki, inajenga matabaka kwani baadhi ya watu wanawapora masikini na kujilimbikizia utajiri ambao si wa haki. Kwa mfano, kama kuna rushwa katika ukusanyaji wa kodi au katika mikataba ya nchi, ni wazi kwamba hatuwezi kupata fedha za kutosha kuwalipa vizuri walimu, madaktari, mahakimu, polisi, wanajesh nk. Hatuwezi kutoa elimu bora, kutoa huduma za jamii, nk. Sijui nani alisema au ametufundisha kuwa ujasiri na dhamira ya kupambana na rushwa chini ya Azimio la Arusha haina tena maana.
(ii) Maadili ya uongozi. Azimio la Arusha lilijenga maadili ya uongozi. Uongozi ulikuwa ni dhamana na sio njia ya kujitajirisha wewe na familia yako. Viongozi wengi wa wakati huo walistaafu wakiwa watu wa kawaida. Mfano mzuri Mwalimu Nyerere alizikwa masikin pamoja na kuongoza nchi hii kwa zaidi ya miaka 25. Leo mtu akipata uongozi tunasema fulani ameula. Uongozi si dhamana tena, uongozi si mzigo tena na uongozi si utumishi tena. Inashangaza viongozi wanakula meza moja na mafisadi. Kiongozi unakula na kunywa na mafisadi, wewe ni kiongozi wa aina gani ? Fisadi siku zote anawaza namna ya kuendelea kuwafisidi Watanzania. Sasa kama kiongozi wa umma ndie mshirika wao, kama kiongozi wa umma ndie anayechangiwa fedha za kampeni au kutoa misaada kwenye taasisi za dini, kiongozi huyo pian aye ni fisadi. Kama unatuambia pesa unazotoa misaada unachangiwa na rafiki zako, tuna haki pia ya kujua hao rafiki zako ni akina nani na wanachanga kwa nia gani. Sidhani kama marafiki hao wanachanga kwa vile mhusika ana sura nzuri sana. Nadhani kuna kitu kinatafutwa na Watanzania tuna kila sababu ya kuambiwa ukweli. Nani alitudanganya kuwa maadili ya uongozi yaliyojengwa na TANU hayana maana tena ?
(iii) Haki na Utu
Azimio la Arusha lilitangaza na kuzisimamia haki za wanyonge na kuheshimu utu. Je, leo bado tunatetea haki ? Je, tunaweza kuwadhibiti waekezaji ili walipe fidia ya haki kwa ardhi yetu, walipe mshahara wa haki kwa watu wetu, wajiepushe kuchafua mazingira yetu au waheshimu utu wetu ?
(iv) Uzalendo na utaifa.
Je, bado tunaona uzalendo na utaifa ni kitu muhimu ? Je kwa taifa linalonuka rushwa, uonevu nk unaweza kujenga uzalendo ?
Kwa hiyo kwa ufupi, baada ya kulitupa Azimio la Arusha, tumevunja misingi imara iliyojenga utaifa wetu na amani yetu. Ni sawa na kuvunja nyumba iliyojengwa na baba yako halafu akaacha kujenga nyumba nyingine.
Changamoto Mpya za Amani ya Tanzania
Mazingira yaliyokuwepo wakati wa awamu ya kwanza ambayo ndio imejenga amani hii tunayoiona yamebadilika. Kwa mfano, kwa vile Tanzania ilikuwa ni nchi ya chama kimoja na serikali moja, ilikuwa na dhamira moja ya kupiga vita umasikini, maradhi na ujinga. Pia ilikuwa rahisi kuleta umoja wa makabila yote na dini zote na kulikuwa hakuna sababu ya baadhi ya watu kutafuta kutugawa kwa msingi ya udini au ukabila.
Leo hii tuna mfumo wa vyama vingi, uhuru mkubwa wa vyombo vya habari, soko huria na uhuru wa kutoa mawazo. Katika muelekeo wa amani ya Tanzania kwa miaka 50 ijayo, nitazungumzia, pamoja na mambo mengine, changamoto hizi.
Muelekeo wa Amani ya Tanzania kwa Miaka 50 Ijayo.
Nimesema kuwa amani ya Tanzania imetokana na sera safi na itikadi sahihi ya TANU na ASP pamoja na dhamira ya utekelezaji wake. Inawezekana kuwa sera na itikadi ya CCM ya leo haina tofauti sana na ile ya TANU. Lakini tujiulize,je, bado kuna dhamira na uwezo wa kutekelezasera hizo na itikadi hiyo? Mimi sidhani kama tatizo la Tanzania ni sera na wala sikubaliani na wale wanaiomba kila siku kuwa chama chao kina sera nzuri au wao ndio wameleta amani. Swala lililokubwa ni utekelezaji wa hizo sera au kuiishi itikadi ya chama. Kama swala ni sera tu, chama chochote cha siasa kinaweza kuwalipa maprofesa wa vyuo maarufu kama Chuo hiki Kikuu cha Dar es Salaam, au Haward University au Oxford nk. wakatengeneza sera nzuri na zinazovutia. Kwa hiyo, kujivunia sera peke yake bila uwezo au dhamira ya kutekeleza ni sawa na kuwa na gari zuri ambalo halina engine.
Mtafiti niliyemtaja Ilana anasema katika uk wa 1 wa kazi yake kuwa, alijaribu kuwahoji Watanzania wengi. Majibu ya Watanzania wengi ni kuwa Tanzania ni masikini ; maana hakuna kazi, elimu ni duni, maji na umeme ni shida, hawawezi hata kumudu milo miwili kwa siku, lakini wanajivunia kuwa Watanzania maana angalao wana amani. Kwa maana nyingine, kitu pekee Watanzania wanachojivunia ni amani.
Mtafiti huyu anasema baada ya kuivunja misingi ya Azimio la Arusha, lazima Tanzania ijenge utamaduni mpya wa kisiasa ‘political culture’ la sivyo, nchi hii haina siku nyingi itakuwa sawa na Burundi, Rwanda, DRC nk.
Tutajengaje utamaduni mpya wa kisiasa ? Kwa maoni yangu, tunapaswa kufanya yafuatayo ili kujenga utamaduni mpya wa kisiasa na kujenga misingi ya amani kwa miaka 50.
(a) Lazima Tanzania Tuwe na Serikali Yenye Nguvu
Mwalimu Nyerere katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Tume ya Kusini ‘South Commission’ mwaka 1998 kuhusu utawala bora (J.K Nyerere 1998, Good Governance for Africa) anasema yafuatayo/=
Afrika lazima iwe na viongozi wenye nguvu ili waweze, pamoja na mambo mengine, kufanya kazi kwa niaba ya watu wake kutokana na matakwa yao. Anasema katika soko huria ambalo limetawaliwa na unyonyaji, ufedhuli, ufisadi na madhila mengine mengi, lazima tuwe na serikali inayoweza kuwatetea wanyonge.
Anaendelea kusema hakuna serikali yenye nguvu ambayo haina uungwaji mkono wa raia walio wengi na haoni itawezekanaje kuwa na serikali yenye nguvu ambayo haijatokana na uchaguzi huru na haki.
Mwalimu kwa maana nyingine anasema serikali yenye nguvu si lazima iwe ya kidikteta na tena anasema udikteta ni udhaifu maana kuwa dikteta maana yake ni kushindwa kutafuta ridhaa ya watu. Dhana hii inapingana na kauli za baadhi ya watu wanaosema eti Tanzania tunahitaji rais dikteta. Hi ni dhana potofu sana. Hatuhitaji Idd Amini, Mabutu au Bokasa wa Tanzania ili tufanye yafuatayo :-
(i) Kupambana na rushwa. Watu wanaotutesa kwa rushwa naamini ni chini ya asilimia kumi (10%). Kama rais unaungwa mkono na zaidi ya asilimia 90% ya watu katika vita ya rushwa unaopa nini ? Kwa nini uwabembeleze mafisadi na kuwaomba waache ufisadi au warudishe fedha walizotuibia ili wasishtakiwe? Hivyo lazima tuchague serikali inayoweza kuwatafuna wala rushwa bila huruma. Tunataka Watanzania mwaka 2015 mtuchagulie Nyerere mpya, Sokoine mpya, Kawawa a.k.a Simba wa Vita mpya nk. Tunataka wakati anaapishwa Nyerere mpya Mwezi November, 2015 kama Rais ambaye nae atamwapisha Sokoine mpya kama Waziri Mkuu, mafisadi wawe wanahaha kutafuta tiketi za ndege kuikimbia nchi.
Tunamtaka Nyerere atakayesaidiwa na Sokoine , ahoji wenye vijisenti kule Uswisi wamevipaje? Wenye magorofa na fedha zisizoelezeka wamezipataje na kama wametulipa kodi.
Wataalamu wa kodi wanajua kuwa kama mtu anajenga ghorofa, anatumia mapato au amekopa. Lazima tujue amezipataje hizo hela ili tujiridhishe kama ametulipa kodi. Kama hawezi kutuambia amepataje basi alipe kodi yetu na kama hawezi basi jengo hilo ni halali yetu.
(ii) Ulinzi wa rasilimali. Huhitaji kuwa na Bokasa wa Tanzania ili alinde mbuga zetu, madini yetu, ardhi yetu, misitu yetu nk. Ili kulinda amani ya nchi lazima rasilimali ziwanufaishe wananchi wote. Tanasikia malalamiko kila siku kuwa ardhi inachukuliwa bila fidia ya kutosha, watu na mifugo wanaathiriwa na kemikali, maliasili kama wanyama hai wanatoroshwa nk. Tunataka serikali inayoweza kumpa mwekezaji masaa 24 awe amefunga mitambo yake na kuondoka baada ya kuwadhuru watu wetu kwa kemikali. Nyerere anavyosema lazima tuwe na serikali yenye nguvu ana maanisha tunapaswa kuwa na serikali inayoweza kumuamrisha mwekezaji aliyechafua maji yetu kwa kemikali atulipe fidia. BP imelipa mabilioni ya fedha kwa Wamarekeani kama fidia baada ya kuchafua mazingira. BP walimwaga mafuta baharini na hivyo kuwaathiri wakazi wa maeneo jirani hasa wavuvi hivyo waliamriwa na serikali yenye nguvu ya Marekani kuwalipa fidia kubwa waathirika. Tumeambiwa hapa kuna mgodi ulimwaga kemikali watu watu na wanyama wao pamoja na mazingira viliathirika sana. Niliona picha ya watu ambao ngozi zao zilibadilika zikawa kama za nyoka kutokana na kuathirika kwa kemikali lakini sijasikia hatua madhubuti za kumtetea mnyonge huyu zilizochukuliwa. Sisi tunashindwaje kuwatetea watu wetu? Kwani mwekezaji ni shangazi au mjomba wetu?
(iii) Haki za wafanyakazi ; Mabeberu na mabepari wana sifa moja kuu nayo ni kulinda maslahi yao pekee. Serikali yenye nguvu ambayo Mwalimu anaizungumzia ni ile inayoweza kumwamuru mwekezaji awalipe watu wetu mshahara wa kutosha au afunge biashara yake aondoke. Bila kusimamia na kutetea haki hizi za wanyonge, watu wetu wataendelea kunyonywa. Nimefanya utafiti kidogo nikagundua kuwa walinzi wa makampuni ya ulinzi wanalipwa wastani wa shilingi 80,000/= kwa mwezi nk. na wengine wanafanya kazi kwa masaa 24 mfululizo. Tume wakweli, mlinzi huyu ambaye ana mke/mume, watoto, ndugu, anapaswa kulipa maji, umeme, kusomesha watoto, analipa nauli, anakula wakati akiwa kazini nk, kumpa Tsh. 80,000/= ni matusi. Where is the government?
Mwanafalsafa Lenin katika kitabu chake (Lenin, V.I., Imperialism, the Highest Stage of Capitalism, Moscow, pp. 58-59) anasema:-
‘As long as capitalism remains what it is, surplus capital will be utilized not for the purpose of raising the standard of living of the masses in a given country, for this would mean a decline in profit for the capitalists, but for the purpose of increasing profits by exporting capital abroad to the backward countries. In these backward countries, profits are usually high, for capital is scarce, the price of land is relatively low, and raw materials and labour are cheap’.
Kwa maneno haya ya Lenin, tusidhani kuwa wawekezaji wanatupenda sana wanapokuja kuwekeza hapa. Wanakuja ili wachukue ardhi yetu kwa bei chee, wawalipe watu wetu mshahara mdogo sana, wafanye biashara bila kulipa kodi, na wanunue mali zetu kwa bei ya kutupwa ili watengeneze faida kubwa waendelee kuwa matajiri na sisi tuendelee kuwa masikini na ombaomba. Ni lazima uwe na serikali inayoweza kusimama upande wa wananchi na kuwa tayari kuwatetea wanyonge. Kuna watu wanacheka eti ni kwanini TANU iliweka miiko ya uongozi kwa mfano kuwakataza viongozi wa umma kuwa na nyumba za kupangisha. Busara ya viongozi wa TANU ni kwamba kwa vile wananchi wengi wakati huo walikuwa masikini, ukimweka kiongozi mwenye nyumba za kupangisha, hisa kwenye makampuni binafsi nk, atasimama upande wa wanyonyaji walio wachache dhidi ya wananchi walio wengi. Kwa mfano, serikali ya awamu ya kwanza ilipitisha sheria inaitwa ‘Rent Restrictions Act ambayo ilitetea sana na kulinda maslahi ya wapangaji. Baada ya viongozi wa sasa kumiliki nyumba wamebadilisha sheria sasa mpangaji hana ulinzi tena maana viongozi wamesimama upande wa wenye nyumba dhidi ya wananchi masikini. Hebu tujiulize; kama Rais aliye madarakani anafanya biashara ikulu, anajimegea mashirika ya umma nk, je atasimama upande wa wawekezaji au wananchi? Ndio maana tunasema lazima turudishe maadili ya uongozi.
Tunavyozungumzia amani tunazungumzia haki. Kama hawa watanzania wataendelea kunyonywa na serikali yao ikaamua kufunga nira na mabeberu basi kuna siku hawa wananchi wanyonge watakataa.
Lakini haki za wafanyakazi si za wafanyakazi wa sekta binafsi tu. Hata wafanyakazi wa sekta ya umma hawatendewi haki. Kima cha chini ni kidogo sana na kinawafanya wafanyakazi hawa wanakata tama.
Mwalimu Nyerere katika hotuba niliyonukuu hapo juu anasema mshahara wa kutosha hauwezi kuwazuia watu wabaya kula rushwa lakini mshahara mdogo na usiokidhi mahitaji ya mfanyakazi utawachochea hata wale wazuri nao wale rushwa. Anaendelea kusema unapokuwa na viongozi wa siasa wala rushwa au wanaohisiwa kuwa ni wala rushwa unaifanya hali ya nchi kuwa mbaya zaidi. Ili kulinda amani ya Tanzania lazima tuwajali wafanyakazi badala ya kuwahujumu watetezi wao. Na hapa napenda kuzungumzia tukio la kutekwa na kufanyiwa unyama kiongozi wa Chama cha Madaktari, Dr Ulimboka.
Pamoja na kwamba swala hili lipo mahakamani, mazungumzo yangu hayaingilii hata kidogo uhuru wa mahakama. Watanzania wote tumeshuhudia unyama huo, na mhusika alijaribu kutaja wale waliohusika kumtesa. Serikali inakanusha kuhusika lakini haichukui hatua muafaka kuchunguza swala hili ili kuwaleta mbele ya sheria wale wanaohusika. Serikali ambayo imesimama upande wa umma haiwezi kukaa kimya pale watu wake wanapoonewa. Kama serikali haihusiki au imeshindwa kuwajua wanaohusika, ingewaleta wapelelezi wenye uwezo mkubwa kama ‘Scotland Yard’ ili uchunguzi ufanyike na wanaohusika wachukuliwe hatua. Serikali kukaa kimya “inatafsiriwa” kama ni njia ya kuwatisha wale wanaotetea maslahi ya wanyonge. Hata hivyo, katika historia ya dunia, hakuna kipigo wala risasi iliyoweza kunyamazisha sauti za wale watetezi wa wanyonge.
(iv) Amani ya Tanzania ya miaka 50 ijayo itajengwa na haki ya demokrasia. Tumeruhusu mfumo wa vyama vingi, lazima pia turuhusu vyama hivi vifanye kazi za siasa. TANU ilihamasisha Watanzania kuunga mkono maazimio na sera mbalimbali kwa kuitisha maandamano. Tumeambiwa wakati Azimio la Arusha lilivyotangazwa Mwalimu Nyerere alitembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Musoma kuunga mkono Azimio. Sasa leo kama chama cha siasa kina sera zake na kinataka ziungwe mkono au kinapinga sera zilizopo kikaamua kuitisha maandamano kuna tatizo gani? Kuzuia demokrasia ni kupandikiza mbegu ya vita na machafuko.
Ni ukweli kuwa siku za hivi karibuni jeshi la polisi limekuwa linatumiwa na baadhi ya wanasiasa wasiotutakia mema kuharibu amani ya nchi kwa kuuwa watu bila sababu. Naomba ninukuu muhtasari wa taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi kilichotokea September, 2, 2012.
Katika kifungu cha 2, taarifa inasema ‘kutokana na hayo yote, Tume imejiridhisha kuwa tukio lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Kifungu cha 2.1 kinasema ‘CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kina usajili wa kudumu. Chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa (Cap 258 R.E 2002) vyama vya siasa vyenye usajili vimeruhusiwa kufanya maandamano na kuitisha mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa afisa wa polisi katika eneo husika. Baada ya kutoa taarifa, kazi ya jeshi la polisi ni kutoa ulinzi.
Hitimisho la taarifa ya Tume ni muhimu sana Watanzania na hasa jeshi la polisi kulizingatia.
Hitimisho lipo katika kifungu cha 4.0.
‘Jukumu la kulinda amani na utulivu ni wajibu wa kila Mtanzania… Tume inatoa wito kwa Watanzania wote kuheshimu haki za binadamu na kutekeleza kwa vitendo misingi ya utawala bora. Kwa kufanya hivi taifa letu litaendelea kuwa na amani na utulivu. Tume inatoa rai kwa jeshi la polisi kutekeleza wajibu wake mkuu wa ulinzi na usalama wa raia bila kutumia juzba. Kuwepo kwa vyama vya siasa ionekane kuwa ni kukua kwa demokrasia na sio kuwa ni upinzani kwa chama tawala’.
Pia magazeti hivi karibuni yalimnukuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akihutubia vikao vya Chama huko Dodoma akiwaonya wana CCM kuacha kulitegemea jeshi la polisi na badala yake wajibu hoja za wapinzani majukwaani. Hadi Rais ambaye ni Amiri jeshi Mkuu kufikia hatua ya kusema maneno haya hadharani, inaondoa shaka kuwa vitendo vinavyofanywa na jeshi la polisi vya kuzuia demokrasia kuchukua mkondo wake vinachochewa na viongozi wa CCM wanaoogopa hoja na kudhani kuwa wataokolewa na jeshi la polisi. Hata hivyo, historia inatufundisha kuwa hakuna jeshi la polisi popote duniani lililoweza kuzuia milele uhuru wa watu.
Kwa kumalizia kipengele hiki, ili amani idumu, taasisi za serikali kama polisi, jeshi, mahakama, ofisi ya msajili wa vyama, Tume ya Uchaguzi na nyingine lazima ziwe huru na zitende haki kwa Watanzania wote bila kujali dini, vyama vya siasa au eneo alilotoka mtu. Mfano mdogo tu ni kwamba kama Kenya katika uchaguzi wa mwaka 2007 ingekuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, mauaji ya raia wasiokuwa na hatia yasingetokea. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wakati huo alinukuliwa akisema hajui ni nani alishinda kiti cha urais. Sasa alitangazaje matokeo kama alikuwa hamjui mshindi? Huku ni kukosa uhuru wa kiutendaji na mawazo.
(v) Ajira kwa Vijana
Serikali kwa sasa haina njia mbadala. Kuendelea kwa amani ya Tanzania ni ndoto kama vijana hawatasaidiwa kwa dhati kupata ajira. Vijana wengi wa Tanzania wamekata tamaa. Wanasiasa hasa wa Chama Tawala wamekuwa wanatoa majibu mepesi kuwa vijana waende vijijini wakalime. Haya majibu hayasaidii kutatua tatizo.
Ikumbukwe kuwa kilimo ni uwekezaji. Kilimo kinahitaji mtaji mkubwa, ardhi, soko la mazao, utaalam wa kilimo nk. Kijana ambaye hana chochote ni matusi kumwambia aende kijijini akalime. Cha kushangaza zaidi hawa wanasiasa wanaosema vijana wakalime wao watoto wao wako kwenye viyoyozi mijini. Kama kilimo ndio ukombozi kwa vijana, basi watoto wa wanasiasa hawa ndio wangepaswa kuwa wa kwanza kwenda vijijini.
Tujifunze kutoka ‘Arab Spring’. Kuna kijana mmoja Mtunisia anaitwa Mohammed Bouazizi ambaye alisoma hadi chuo kikuu. Kwa vile alikosa kazi na serikali yao haikuona sababu ya kuwahangaikia vijana wapate ajira, kijana huyu aliamua kufanya biashara ya kimachinga ya kuuza matunda. Askari wa Jiji waliamua kumnyanganya matunda yake. Kijana kuona hana namna nyingine ya maisha aliamua kujimwagia petrol na kujichoma moto. Kitendo hicho kiliwasikitisha wengi matokeo yake watu waliandamana wakaiangusha serikali ya Tunisia. Mambo haya yaliendelea yakamtafuna Gadafi, Mubarak yakaenea Yemen, Bakhrain, Algeria na sasa mnaona yanayoendelea Syria. Nchi za kibepari zilitambua hilo mapema wakaamua kuwalipa vijana wao ‘unemployment benefit’ ndio maana mapinduzi ya kijamaa hayakutokea Ulaya magharibi. Tulizingatie sana hili la vijana maana pamoja na kwamba nguvu za vijana zinapotelea vijiweni bure, vijana hawa ni bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote.
(vi) Lazima turudi kwenye misingi ya Azimio la Arusha kuhakikisha Watanzania wanapata haki ya elimu, huduma za jamii nk. Kuna wanasiasa wanasema huko ni kuturudisha kwenye ujamaa. Cha kushangaza, wanasiasa haohao wanasema Tanzania ni nchi ya ujamaa na kujitegemea. Nani alikuambia elimu bora na ya bure hasa kwa wasiojiweza ni siasa ya kijamaa? Nani alikuambia huduma za afya bure ni siasa ya kijamaa? Misingi ya Azimio la Arusha ni dhahabu, Watanzania tuna dhahabu ila hatujijui. Wenzetu wamekuwa wanaiga misingi ya Azimio hili na kulitekeleza kwao.
(a) Rais Bush Jr wa Marekani aliiga Azimio la Arusha akaanzisha kitu kinaitwa ‘No child shall be left behind’ program. Mpango huu ulihakikisha kila mtoto wa Mmarekani anapata elimu bora hata kama hana fedha.
(b) Rais Obama ame copy msingi wa Azimio la Arusha kwa mpango wake wa bima ya afya ambao unalenga kumpa kila Mmarekani nafasi ya kupata huduma bora ya afya hata kama hana fedha.
(c) Kenya wame copy misingi ya Azimio kwa katiba yao kutamka kuwa elimu bora ni haki ya kila mtu. Sheria imepitishwa Kenya, the Education Act, 2012 ku-guarantee haki ya kusoma hadi chuo kikuu hata kama mtu hana fedha.
Tukirudia misingi yetu, tukizingatia haki ya elimu na huduma nyingine za jamii, amani yetu itaendelea kunawiri.
(vii) Tuzuie uchochezi wa dini na ukabila
Hivi karibuni tumeshuhudia chokochoko za dini hapa Tanzania ambazo zinatishia amani yetu. Utafiti uliofanywa na REDET mwaka 2000 ulionyesha kuwa asilimia 78% ya Watanzania wanaamini uhusiano kati ya wakristo na Waislam wa Tanzania ni mzuri sana. Hivyo tunasema kwa hakika hakuna ugomvi wala chuki kati ya wakristo na waislamu wa Tanzania.
Tatizo lipo kwa wanasiasa waliofilisika na wenye udogo wa mawazo wanaodhani kuwa wanaweza kutumia tiketi ya udini au ukabila/ukanda kuendelea kubaki madarakani. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 unadhihirisha hili. Hata uchaguzi mdogo wa Igunga-Mahakama Kuu imesema wazi kuwa uligubikwa na udini.
Tufanye nini?
Nilidhani wazee wetu wastaafu kama akina Mh. Ally Hassan Mwinyi, Salim A.Salim, John Malecela, Kingunge Ngombale Mwiru, Joseph Warioba, Mzee Joseph Butiku nk. wangesimama kidete kukemea kwa nguvu zote chuki za kidini, kikabila na rangi zinazopandikizwa na baadhi ya watu lakini hawajafanya hivyo. Hata kama wamefanya, si kwa kiwango cha kutosha.
Watanzania mtakumbuka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na 2005 kulitolewa shutuma kuwa CUF ni chama cha kidini.
Mwaka 1995 NCCR-Mageuzi kilisemwa kuwa kilikuwa chama cha Wachaga.
Mwaka 2005 Dr. Salim Ahmed Salim alisakamwa kuwa ni mwarabu hivyo asingefaa kuwa Rais.
Mwaka 2010 Chadema kilisakamwa kuwa ni chama cha kaskazini na ni chama cha wakristo. Haya mambo yanasemwa bila haya majukwaani.
Dr. Salim anaheshimika sana Tanzania. Ameshawahi kushika nyadhifa nyingi sana nchi hii. Kusema leo kuwa yeye ni mwarabu eti kwa vile alitaka kugombea urais ni kosa kubwa na ilipaswa likemewe kwa nguvu zote na Watanzania wanaopenda amani. Kufumbia macho mambo haya yataendelea kukua na yatahatarisha amani yetu. Na kweli yanakua maana tumeambiwa kuwa Rais hawezi kutoka Kaskazini hata kama ni kwa tiketi ya CCM. Kesho tutaambiwa Rais hawezi kutoka Musoma maana hawa watu wa Musoma kama akina Esther wana damu ya Unyerere hivyo wakishika nchi watakuwa wakali kutetea haki za mnyonge kama alivyofanya Mwalimu.
Hatujaambiwa CUF kimeacha kuwa chama cha udini lini wala NCCR kuwa chama cha wachaga lini.
Kwamba Chadema ni chama cha kaskazini wakati kina wabunge na madiwani nchi nzima ni kichekesho. Basi hawa wanaopiga kelele watuambie kuwa mikoa ya Rukwa, Iringa, Katavi, Mbeya, Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dar es Salaam nk iliyotoa wabunge wa Chadema kwamba siku hizi inaitwa Mikoa ya Kaskazini.
Kwamba Chadema ni chama cha kidini ni matusi na kebehi kubwa. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya viongozi wakuu sita wa juu wa Chadema, wanne ni waislam. Lakini watu hawa wanaosemasema mambo haya hawatuambii pia kuwa chama chao ni chama cha familia maana kuna familia moja ambapo baba, mama na watoto ni wajumbe wa kikao cha juu cha chama hicho.
Napendekeza itungwe sheria kali ambayo itaunda chombo cha kufuatilia kauli za wanasiasa na Watanzania wengine. Chombo hiki kipewe mamlaka ya kuwahoji na kuwashtaki wale wanaohubiri udini, ukanda au rangi. Sheria iweke adhabu ya kifungo pamoja na faini kubwa ikiambatana na kufungiwa kujihusisha na siasa kwa miaka mingi au maisha. Chombo hicho pia kipewe mamlaka ya kumhoji Rais na kumshtaki bungeni ili aondolewe madarakani kama yeye ndie atakuwa ametoa hotuba ya uchochezi au kujihusisha na vitendo vya kuwagawa wananchi.
Rwanda waliwavumilia walioleta uchochezi bila kuchukua hatua, madhara yake mmeyaona, Tanzania tusifanye kosa hilo.
(viii) Mwisho katika kulinda amani kwa muda mrefu tuhimize muungano wa chi zetu. Matatizo mengi ya amani Afrika yanatokana na umasikini na uhaba wa rasilimali. Mfano nchi kama Burundi, kutokana na uhaba wa ardhi, watusi au wahutu wanajaribu kutumia karata ya ukabila ili kuwaondoa wenzao. Hebu fikiria tungeunda muungano wa Sudan Kusini, Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na DRC. Tungekuwa na uchumi mkubwa kuliko India na Brazil. Watu wa nchi hii kubwa na tajiri wangehangaika na uchumi zaidi kuliko kuangalia ukabila na udini. Tanzania tunaweza kuongoza tena jitihada za muungano maana awali Kenya ndio walikuwa wanaogopa muungano wakati Tanzania ilikuwa tayari muda wowote kuungana. Mwalimu alishawahi kusema, kama Kenyata akikubali leo tuungane, kesho mimi nipo tayari, tena nakubali yeye awe Rais. Huu utashi wa Muungano umeenda wapi? Au kuna watu wanadhani ukiwa na muungano itakuwa ngumu wao kuendelea kujineemesha? Tusiwe waoga maana hata Mwalimu alisema…’africa bila muungano haina future’. Tuweke maslahi binafsi nyuma, tuwajengee watoto wetu taifa lenye nguvu ili wawe na nafasi yao duniani. Nina ndoto, Tanzania tutachukua tena nafasi yetu ya uongozi. Tutahimiza tena muungano na hata tutakuwa tayari kukubali kiongozi wa juu atoke nchi nyingine ili mradi tu maslahi ya watu wetu yalindwe.
Mwisho namalizia kwa kunukuu maneno ya mtafiti Ilana Kessler na naomba myatafakari. (uk 103 wa kazi yake).
‘Watanzania wengi hasa wenye umri mkubwa wanaichagua CCM pamoja na kwamba hawaziamini tena sera zake na wala hawawaamini tena viongozi wake. Sababu pekee inayowafanya waichague CCM ni kwa vile wanaamini kuwa CCM italinda amani. Kama vyama vya upinzani Tanzania vikiweza kuwashawishi hawa Watanzania kuwa nao wanaamini katika amani na wanalengo hilohilo la kulinda amani ya Tanzania, basi wataweza kuzipata kwa urahisi kura za watu hawa na hakika wataiangusha CCM kwa urahisi sana’
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza, Mungu Ibariki Tanzania.

seria signature

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO