Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MBOWE:2013 HAKUNA KULALA

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mh Freeman Mbowe
*************

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema mwaka 2013 utakuwa mwaka wa chama hicho kutumia nguvu ya umma, itakayolenga kuishinikiza Serikali kuyafanyia kazi mambo ya msingi ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele tangu mwaka 2010.

Amesema kutokana na hali hiyo kuanzia Januari mwakani hakuna kulala wala mtu kupumua, kwamba chama hicho kitafanya harakati za kisiasa za aina yake ikiwa ni pamoja na kuifanyia maboresho Operesheni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).

Akisoma maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutaka kwa siku mbili Dar es Salaam jana, Mbowe alisema tangu 2010 wamekuwa wakiitaka Serikali kutekeleza masuala mbambali lakini imekuwa haifanyi hivyo.

“Kama CCM wakitumia polisi sisi tutapambana kwa njia nyingine ambayo sio vurugu wala kugombana na vyombo vya dola” alisema Mbowe.

Alifafanua, “Septemba 9, mwaka huu tulifanya kikao cha Kamati Kuu baada ya mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Televisheni ya Channel Ten, Daudi Mwangosi na kumwandikia barua Rais Jakaya Kikwete tukimtaka aunde tume huru ya kimahakama ya uchunguzi wa jambo hili, ila mpaka leo kimya.”

Mbowe ambaye alikuwa ameambatana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbroad Slaa alisema, “Pia nimewahi kukutana na Rais Kikwete na kumsisitiza suala hili, lakini mpaka leo hii umepita zaidi ya mwezi mmoja hakuna jibu lolote.”

Alisema kwa muda wa miezi mitatu chama hicho kilisitisha mikutano yake ya M4C iliyokuwa ikifanyika mikoa mbalimbali nchini, ili kusubiri hatua zitakazochukuliwa na Rais Kikwete baada ya kumwandikia barua hiyo, ambayo pamoja na mambo mengine ilitaka kuchukuliwa hatua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, maofisa wa juu wa Jeshi la polisi pamoja na Makamanda wa polisi wa Mkoa wa Morogoro na Iringa.

Alisema katika kikao hicho mambo yaliyojadiliwa na ambayo watakayowasilisha bungeni ni pamoja na kutofanyika kwa chaguzi za marudio katika kata 13 nchini, licha ya kuwa umeshapita zaidi ya mwaka mmoja.

“Katika hili inaonekana wazi kuwa CCM ina hofu ya kushindwa, zipo kata 13 nchini ambazo zipo wazi kwa zaidi ya mwaka sasa na uchaguzi haujafanyika, hii ni kinyume na sheria za uchaguzi zinazoeleza kuwa uchaguzi unatakiwa kufanyika ndani ya siku 90 baada jimbo au kata kutokuwa na mwakilishi” alisema Mbowe.

Alisema jambo jingine lililojadiliwa ni kuboreshwa kwa daftari la kudumu la wapiga kura ili kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura awe na haki ya kufanya hivyo.

“Jambo jingine ni Katiba, kamati kuu imetoa mapendekezo yake kwamba wakati mchakato wa kupata Katiba Mpya ukiendelea, tunataka ufanywe utaratibu wa kubadili sheria mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi ya mwaka 1985,” alisema Mbowe.

Alifafanua zaidi, “Sheria hii ikibadilishwa italifanya taifa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi isiyofungamana na upande wowote pamoja na kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.”
Alisema kuwa ni ngumu kwa vyama vya upinzani kujiandaa na uchaguzi wa 2015 wakati mfumo wa uchaguzi ujao haujulikani na kusisitiza, “Mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma kwa sababu mwaka 2011 na 2012 tumezungumza mengi na hayajafanyiwa kazi.”

Chanzo:Mwananchi

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO