Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mwanajeshi anapojitokeza wazi kushabikia upinzani na wale wanaojificha kushabiki CCM

M. M. Mwanakijiji

Lema na Afande

MOJAWAPO ya picha ambazo zimevutia hisia za watu wengi sana siku chache zilizopita ni ya mtu ambaye ameonekana akiwa amevaa fatigi ya kijeshi huku akiwa amesimama na kuzungukwa na wabunge wa CHADEMA Godbless Leman na Joshua Nassari.

Katika picha nyingine ‘askari’ huyo ameonekana akiwa amesimama kama mmoja wa walinzi wa umati tena kikakamavu mbele ya jukwaa.

Kama picha hii ni ya kweli na kuwa mtu aliyepigwa picha hii ni mpiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambayo yuko katika utumishi (active duty), basi siasa zetu zimefikia katika kiwango kingine kabisa.

Naomba kwa ajili ya hoja yangu hii tudhanie tu kuwa picha ni ya mpiganaji wa JWTZ na kuwa amejitokeza wazi kuiunga mkono CHADEMA na sera zake bila kujali matokeo yake katika ajira yake jeshini.

Baadhi ya wachangiaji mbalimbali kwenye mitandao ya jamii wameonyesha kuguswa na kitendo cha askari huyo kujitokeza na hasa pale ilipodaiwa kuwa amedai yeye mwenyewe kuwa hajali wakubwa wake watamfanya nini kwani amekizimia CDM.

Wapo ambao wameona kitendo hiko kuwa ni cha kishujaa na kinahitaji kuungwa mkono.

Wapo wengine ambao wameona kitendo hicho ni zaidi ya kishujaa kwani kinaonesha hali ya wananchi wetu wanavyopigika chini ya utawala wa CCM.

Kwamba hadi wanajeshi wamechoka ‘ile mbaya’ kiasi kwamba hawajali tena kujificha kwenye kivuli cha “jeshi” na sasa kama huyo mmoja alivyoweza kujitokeza basi wengine wataanza kujitokeza vile vile kwani wao nao wanaonekana mitaani wanavyo hangaika na maisha.

Wapo wengine ambao pia ni wengi kidogo kwa maoni yangu ambao wanadai wakati umefika kwa wana jeshi wanaounga mkono upinzani wajitokeze wazi kwani kwa muda mrefu wanajeshi wenye kuunga mkono CCM wamekuwa wakitumia nafasi zao kuitetea CCM bila kukemewa na uongozi wa juu wajeshi.

Mfano mzuri ambao unatolewa mara moja ni jinsi alivyofanya aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi Gen. Abdulrahaman Shimbo wakatit unaelekea uchaguzi mkuu wa 2010.

Gen. Shimbo alijitokeza na kuzungumza na waandishi wa habari na kupiga mkwara ambao ulionekana kuipigia debe serikali na hasa kumlinda Rais Kikwete badala ya kubakia bila upande.

Gen. Shimbo alizungumza maneno ambayo sehemu nyingine yangeonekana kuingilia mchakato wa upigaji kura.

Kwa wanaokumbuka niliandika katika gazeti hili wakati ule kulaani kitendo hicho. Nakumbuka niliandika wakati ule (Octoba 3, 2010) kuhusu jambo hili na kusema kuwa nijukumu la Jeshi kumpigia Saluti Rais anayechaguliwa na wananchi.

Hawawezi kuamua ni rais gani wanamtaka au hawamtaki.

Niliandika katika makala ile ya Kiingereza kulaani kitendo cha Shimbo kutoa vitisho na nikasema kuwa “It is for this reason, I condemn in all possible strongest terms any plan or arrangement that would not let the election process be free, fair and transparent for all to see. I call for an immediate statement from our military leadership to assure the country that they would remain neutral in this political and democratic process and will be willing and ready to ensure that the election will be peaceful and the results will be respected by all parties including the incumbent.” Sikuamini kuwa Shimbo alifanya vile kwa sababu Polisi walishindwa kusimamia uchaguzi.

Lakini siyo hivyo tu wapo wanaotolea mfano kuwa wakati Mwigulu Nchemba amedai kuwa Jeshi limeapa kuilinda CCM mpaka kufa hakuna kauli yoyote iliyotolewa ama na uongozi wa jeshi au na mtu mwingine yeyote serikalini, hivyo kuonesha kuwa ni kweli uongozi wa juu wa jeshi letu uko tayari kufanya lolote kuilinda CCM madarakani.

Haikutolewa kauli yoyote kukanusha wala kujaribu kuuliza jeshi hilo liliahidi hayo lini? Lakini huyu bwana mdogo asiye na nguvu kujitokeza kupiga picha na kiongozi anayemhusudu au wa chama anacho kihusudu imekuwa nongwa?

Lakini wapo wengine kama mimi ambao tunachukulia yote mawili ni makosa. Ni lazima mstari uliochorwa wa wanajeshi kutokuingiza siasa uheshimiwe.

Katika demokrasia jeshi lazima liwe nje ya siasa na mwanajeshi yeyote anayetaka kushabikia siasa au kushabikia chama cha siasa ni lazima ama afanye hivyo nje ya sare zake na kama anataka kushika nafasi ya kisiasa ni lazima atoke jeshini kwanza.

Bahati mbaya sana mstari huu haujaheshimiwa na CCM yenyewe na matokeo yake wameendelea kutenda kana kwamba mstari huu haupo.

Kuna mifano ya watendaji kadhaa ambao wameendelea kuwa katika siasa licha ya kwamba ni wanajeshi na wengine haijawahi kuelezwa vizuri kama walistaafu jeshini rasmi.

Na wengine wameonekana wakifanya utumishi jeshini na mara moja wanapotoka wanapewa nafasi za kisiasa. Kwa mfano aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Adadi Rajabu ambaye baadaya kutoka Polisi akapewa Ubalozi na hayuko peke yake.

Na wengine hatutashangaa kusikia Gen. Shimbo akizawadiwa nafasi fulani. Yote haya ni mambo ya hatari kwa ukuaji wa demokrasia kwani watendaji wa vyombo vya majeshi wanaanza kutenda wakipigia mahesabu kuwa wata kuja kukumbukwa na watawala.

Haya yote yanachangiwa na kukosekana kwa sheria na kanuni wazi inayoweka kikomo kwa watumishi wakuu wa jeshi kushika nafasi za kisiasa. Kwa mfano sheria ikikataza mtu yeyote aliyeshika cheo cha kuanzia Kanali kwenda juu kuteuliwa nafasi yoyote yakisiasa hadi ipite miaka mitano tangu atoke jeshini inaweza kusaidia. Lakini kwa huku chini itakuwaje?

Kama wakubwa wanaweza kujihusisha na siasa baadaya ajira hawa wa chini wafanye nini? Je tuweke utaratibu gani ili wanajeshi wa ngazi za chini wasijisikie wanaonewa.

Naamini hakuna namna isipokuwa kuendelea kuhakikisha huu mstari unaheshimiwa. Wanajeshi wakiwa na sare zao wasishiriki kuunga mkono chama chochote cha siasa kwani hatutaki ilete hisia ya sehemu ya jeshi kugawanyika kisiasa.

Nje ya sare na nje ya muda wakazi wanajeshi waendelee kuruhusiwa kushiriki shughuli mbalimbali za kisiasa isipokuwa kuwa na kadi rasmi ya chama cha siasa.

Lakini kuwakatalia kuwa na kadi ya chama cha siasa nako siyo kuwanyima haki yao?

Hapa basi inabidi wanajeshi nao waruhusiwe kuwa na kadi za vyama vya siasa kitu pekee ambacho labda wasiruhusiwe kushika uongozi wowote ndani ya chama cha siasa hadi anapotoka jeshini.

Kwa kufanya hili la pili itasaidia pia kwa baadhi ya wapiganaji ambao watataka kushika nafasi za uongozi kwenye chama hasa zile zinazohitaji mgombea awe na muda fulani ndani ya chama.

Mtindo huu ndio unatumiwa sana na Marekani labda na baadhi ya nchi nyingine ambapo suala la uanachama linabakia na askari hadi anapotoka japo anajulikana kama ni “registered member” wa chama fulani.

Na wao wenyewe wanaheshimu mipaka hiyo ya kutokuingiza siasa katika utumishi wao na wanapofanya hivyo kuna kanuni kali kabisa – wanapoomba waondolewe jeshini au kuteremshwa vyeo kwa kuwa wana siasa badala ya wapiganaji.

Hivyo, basi wakati JWTZ linaendelea kuchunguza habari za mwanajeshi huyu uongozi wake pia ukae chini na kujiuliza kama kanuni zake zinawafanya watendaji wa juu wa JWTZ kuonekana wanakipendelea chama tawala na kuweka mipaka ya jeshi kujihusisha na siasa au na mambo ya kisiasa.

Kwa mfano, tayari tumeona dalili za jeshi kuingizwa kwenye harakati za kisiasa na kutishia maandamano ya kisiasa.

Ni lazima kanuni ziwekwe wazi ili jeshi libakie na heshima najukumu lake kuu la kulinda uwepo wa nchi yetu. Vinginevyo, itabidi iamuliwe kama jeshi ni la CCM

Source: Tanzania Daima, 26th December, 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO