Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Mbowe: Sigombei urais 2015

Imeandikwa na Mtanzania, Jumapili, Desemba 30, 2012 07:26 Na Eliya Mbonea, Karatu

Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe akihutubia Mjini Karatu jana. Picha kwa hisani ya Gazeti la Mwananchi

*Amsafishia njia Dk. Slaa, asema anatosha
*Atangaza kumaliza mgogoro uliofukuta Karatu

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, hatimaye ametegua kitendawili cha mgombea urais wa mwaka 2015, kupitia chama hicho.

Katika mkutano uliofanyika viwanja vya mpira mjini Karatu jana, Mbowe aliwaambia wananchi wa Karatu kwamba, hafikirii kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Badala yake alibainisha kwamba, nguvu na juhudi anazozifanya kwa sasa ndani ya chama hicho, ni kuhakikisha anaijenga Chadema kuwa chama imara kuelekea kuchukua nchi mwaka 2015.

“Sifikirii kugombea urais 2015, siwezi kugombana na Dk. Slaa mimi na yeye tunapambana kuwaondoa hawa mafisadi serikalini. Ndugu zangu urais ndani ya CHADEMA si jambo la mzaha.

“Dk. Slaa anatosha, kazi ya urais si kazi ya majaribio. Mungu akipenda tutampa tena Dk. Slaa nafasi ya kusimama kwa mwaka 2015. Mimi sihitaji cheo ninachoomba Mungu anisaidie kuongoza mapambano ya kuingiza mtu Ikulu kupitia CHADEMA.

“Sina shida na uwaziri wala cheo ndani ya Serikali, nikifanikiwa kuingiza mtu Ikulu mwaka 2015, basi narudi zangu kwenye biashara,” alisema Mbowe.

Tamko hilo la Mbowe linaonekana kuzima ndoto za Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto ambaye alitangaza mapema nia ya kugombea urais kupitia chama hicho

Amaliza mgogoro Karatu

karatu wapatanaPichani kutoka kushoto; Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Mh Lazaro Masai, anafuata Mbunge wa Karatu, Mh Israel Natse (CHADEMA), halafu Mbunge wa Viti Maalumu CHADEMA Mh Cecilia Pareso na Mwenyekiti Darade Moshi wakiwa katika picha ya pamoja wakishikana mikono kuonesha ishara ya mshikamano na umoja baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Mh Freeman Mbowe kuwasuluhisha katika maswala mbalimbali waliyokuwa wanakinzana kiasi cha kutishia kudorora kwa maendeleo Jimboni humo. Picha na Ephata Nanyaro

Akizungumzia kuhusu mgogoro ndani ya chama hicho wilayani Karatu, Mbowe aliyegeuka kuwa mpatanishi wa miamba ya kisiasa wilayani hapa, alisema mgogoro huo umewasikitisha wananchi wa Karatu.

Miamba ya siasa iliyokuwa kwenye mgogoro huo ni Mbunge wa Karatu Israel Natse, Mbunge wa Viti Maalum Secilia Pareso, Mwenyekiti wa Halmashauri Lazaro Maasai na Jubileth Mnyenye, ambao walikumbatiana kama ishara ya kumaliza tofauti zao.

Katika mkutano huo Mbowe aliwaambia miamba hiyo kwamba, kitendo chao cha kutofautiana ndani ya chama kimesababisha wananchi kuendelea kuumia na kukosa imani na chama hicho.

“Leo nimekuja kuzungumzia mustakabali wa kisiasa wa Karatu, ninajua mnahofu sana kuhusu mustakabali wa chama chenu. Naomba niseme leo kwamba, chama ninachokiongoza ni chama cha watu chenye kufanya kazi za watu.

“CHADEMA si mali ya Dk. Slaa, Mbowe wala mtu yeyote hiki ni mali ya Watanzania wenye uchungu na nchi yao. CHADEMA ni chama chenye kujenga matumaini kwa wananchi,” alisema Mbowe na kuongeza:

“CHADEMA hatujengi chama cha kujenga wafalme ndani ya chama, hakuna kiongozi aliyepo juu ya chama, katiba ya chama ndio chombo kinachotuongoza makabila yote ndani ya chama,” alisema.

Akizungumzia uamuzi uliofanywa na Kamati Kuu jijini Dar es Salaam ya kuwasimamisha uongozi kwa muda viongozi wa Karatu, ili kupisha uchunguzi, Mbowe alisema baada ya kukaa na kuzungumza nao sasa ameridhika na kuwarejesha kazini viongozi wote.

Alisema kwa muda mrefu sasa chama hicho kimekuwa kikipigania mambo muhimu na ya msingi kwa wananchi hata hivyo katika utekelezaji huo bado wanaamini kwamba, ndani ya CHADEMA pia hakuna malaika wote ni binadamu.

“Kihistoria Karatu ni ngome ya CHADEMA, naomba niwaambie viongozi hampo juu ya chama, inapotokea mmekiumiza chama basi lazima tule sahani moja na nyinyi.

“Kamati Kuu kule Dar es Salaam tulifanya maamuzi magumu kwamba, hawa wanaume wanaomenyana hapa Karatu hatuwezi kuwavumilia waendelee kukiumiza chama.

“Kiongozi yeyote anayetoka nje ya mstari tuna mchinjia baharini. Naomba viongozi wangu muelewe hivyo ndani ya Chama hakuna aliyepo juu.

“Hawa tungewachinjia baharini, lakini kwa vile wameifanyia CHADEMA mambo mengi ndani ya Karatu na Arusha, hatuwezi kuwachinjia baharini lazima tuthamini mchango wao.

“Tumekaa siku tatu tunazungumza na hawa wanaume kwa kina. Napenda kuwatangazia wananchi wenzangu wa Karatu hawa Tembo waliokuwa wakipigana hapa wamewaumiza mpaka Punda milia na Nyati hapa Karatu.

“Wanachama, kamati mbalimbali na madiwani hapa waligawanyika pande mbili ndani ya chama. Chadema tunaposigana tuna mpa nafasi adui CCM,” alisema Mbowe.

Akiwarushia makombora viongozi hao, Mbowe aliwaambia kwamba kuchaguliwa kwao kuwa viongozi hakumaanishi kwamba Karatu nzima haikuwa na viongozi wanaofaa kuongoza kwa nafasi walizonazo.

“Ndugu wananchi, nimekaa kwa siku tatu hapa Karatu kuzungumzia tofauti hizi, sasa naomba niwaambie kwamba, tumeyamaliza na miamba hii ya kisiasa imekubaliana kufanya kazi pamoja.

“Sasa naomba niwasimamishe hapa wote ili wawaombe msamaha nyinyi wananchi, kwani waliwakosea sana. Juzi na jana tumekesha hapa kwa ajili ya kuhakikisha tunamaliza tofauti hizi.

Sasa kwa mamlaka niliyopewa na Kamati Kuu naomba niwatangazie wananchi kwamba, naurejesha uongozi huu madarakani kama walivyokuwa awali,” alisema.

Hata hivyo kabla ya kuwasimamisha viongozi hao Mbowe aliwataka watambue kwamba nafasi yao ya kuwa kwenye ofisi za umma, ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kujitumikia wao na maisha yao.

“Hawa jamaa wametusumbua sana, hata kama watakuwa na hoja za kweli. Nataka leo wazungumze mbele yenu ujinga wa migogoro basi tena Karatu,” alisema Mbowe.

Akianza kuzungumza mbele ya wananchi hao Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Lazaro Maasai aliwaeleza wananchi wa Karatu kwamba, ana msamehe Mnyenye Saba mara Sabini.

“Kwa yale yote niliyomkosea namsamehe Saba mara Sabini. Lakini pia kwa wananchi wa Karatu nawaomba mnisamehe kwa kuwakosea na kuwaumiza,” alisema Maasai.

Kwa upande wake Mnyenye aliwaambia wananchi kwamba, hakuna tena uhasama ndani ya Chama hicho Karatu kwani sasa ametambua tofauti kidogo zimeleta madhara kwa wananchi wanaokipenda chama hicho.

“Nimewakwaza sana wananchi wa Karatu na viongozi wangu wa Chama pengine kwa kutojua au kufuatana taratibu za Chama. Hakuna tena uhasama kati yangu na Lazaro. Ninawaomba mkiona ninakwenda tofauti msingoje mpaka Mbowe atoke Dar es Salaam, nipo tayari kujishusha au kuondoka kwenye uongozi,” alisema Mnyenye.

Katika hatua nyingine Mbowe alitumia fursa hiyo pia kuwapatanisha katibu wa wilaya ya Karatu na Mwenyekiti wa wilaya ambao nao walikuwa hawaelewani kiutendaji.

Kana kwamba hiyo haikuwa imetosha Mbowe aliwageukia tena Mbunge Natse na Pareso, ambao nao walipandishwa jukwaani kwa ajili ya kuwaomba msamaha wananchi kutokana na tofauti zao.

“Nikiri mbele yenu hapa kwamba, nitamsaidia Mbunge Natse kwanza huyu ni sawa na baba yangu, mchungaji wangu,” alisema Mbunge Pareso.

Kwa upande wake Mchungaji Natse aliwaomba msamaha wananchi waliokuwa wamefurika kwenye viwanja hivyo, kwa kuwaambia kwamba siku zote hupata tabu ya kusimama mbele ya wananchi hao kutokana na kura nyingi walizompatia.

Katika hatua nyingine uwanjani hapo, Mbowe aliongoza harambee ya ujenzi wa ofisi mpya za wilaya za chama hicho kwa kukusanya michango mbalimbali kutoka kwa wananchi pamoja na viongozi wa chama na wabunge.

Kwa upande wake Mbowe alisema kwamba, amesikitishwa na kitendo cha wilaya hiyo kuendelea kupangisha ofisi wakati ndio wilaya yenye mabadiliko makubwa ya mageuzi ndani ya nchi.

“Nimewaambia hawa viongozi waliokuwa kwenye tofauti zao, wao ndio watakuwa wasimamizi wakubwa wa mradi huu na kwa kuanzia mimi nachangia Sh Milioni 10, Dk. Slaa Sh Milioni 5, Nassari ametoa Sh Milioni 2,” alisema Mbowe.

Mara baada ya kumaliza kuzungumza Mbowe, viongozi waliokuwa katika mgogoro walianza kupitisha bakuli kwa wananchi kwa ajili ya kukusanya fedha hizo ili fedha hizo ziweze kuingizwa katika ujenzi.

Nassari amshukia Kinana

MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari, amemshukia Katibu Mkuu wa CCM, Abdluhaman Kinana, akidai ni hatari kwa rasilimali za taifa.

Akizungumza kwenye mkutano wa upatanisho kwa viongozi wa chama hicho, uliofanyika viwaja vya mpira Karatu Nassari aliishangaa CCM kwa uamuzi wake wa kumteua Kinana.

“Kinana amepewa dhamana kukisafisha CCM wakati yeye mwenyewe ni mchafu. Amechaguliwa wiki moja tu rasilimali zetu zikakamatwa huko China, huku Kampuni yake ikihusishwa kwa karibu.

“Kule Meru tumempiga marufuku kwasababu tuna hifadhi ya Taifa pale ya Arusha, sasa nanyinyi huku Karatu kwasababu mpo karibu na Hifadhi ya Taiga, angalieni sana hawo Tembo wenu,” alisema Nassari.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO