Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Lema atoa sababu 18 kutetea ubunge wake

na Happiness Katabazi; Tanzania Daima 5 Des 2012

ALIYEKUWA Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbles Lema, amewasilisha sababu 18, kuiomba Mahakama ya Rufaa nchini, itengue hukumu ya awali iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili mwaka huu ambayo ilifuta ubunge wake.

Ombi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo jana na mawakili wa Lema, Method Kimomogoro na Tundu Lissu ambao walidai kuwa hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalila haina hadhi ya kuitwa hukumu.

Mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa linaloongozwa na Jaji Natharia Salum Massati, wakili Kimomogoro, alieleza mahakama kuwa rufaa ya mteja wake ina jumla ya sababu 18 za kupinga hukumu iliyotolewa na Jaji Rwakibalila.

Katika hukumu yake iliyoibua mjadala mkubwa nchini Aprili mwaka huu, Jaji Rwakibalila alimtia hatiani Lema kwa makosa ya kutoa lugha za kumkashifu mgombea mwenzie, Dk. Batilda Buriani (CCM) na kumfungia kutogombea ubunge kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.

Alidai kuwa, Jaji Rwakibalila alijielekeza vibaya katika hukumu yake alivyosema kuwa kesi za uchaguzi hazitawaliwi na kanuni za sheria za Uingereza kwani kuna maamuzi ya kesi mbalimbali yaliyokwishatolewa na Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu nchini na kuruhusu kesi za uchaguzi ziamuliwe kwa kutumia kanuni na sheria za Uingereza.

Katika hoja ya pili, Kimomogoro alidai kuwa Jaji Rwakibalila alijielekeza vibaya kuruhusu wajibu rufaa, wasitaje maneno kwenye hati ya madai ambayo walidai ni maneno ya udhalilishaji wa kijinsia na dini ambayo yanadaiwa kutolewa na Lema, kwenye mikutano ya kampeni dhidi ya Dk. Burian.

Hoja nyingine ni kwamba hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kwamba wajibu rufaa kama kweli waliandikishwa kupiga kura katika Jimbo la Arusha Mjini mwaka 2010 au la.

Kwa mujibu wa wakili huyo, hoja nyingine ni kwamba Jaji Rwakibalila alikosea kisheria kusema kuwa mtu yeyote akiwemo mpiga kura ana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo ambalo yeye ni mpiga kura na kuongeza kuwa, wao wanaomba Mahakama ya Rufaa itamke kuwa wajibu rufaa (wapiga kura wa Jimbo la Arusha waliofungua kesi ile), hawana haki kisheria kufungua kesi ile ya kupinga ubunge wa Lema kwani mwenye haki ya kufanya hivyo ni Dk. Batilda mwenyewe.

Aliongeza kuwa, mpiga kura yeyote hana haki ya kufungua kesi ya kupinga ubunge wa Arusha Mjini kwani haki zao hazikuvunjwa.

Aidha, katika hoja nyingine alidai kuwa Jaji Rwakibalila hakutumia maamuzi ya kesi za Mahakama ya Rufaa wala vifungu vya sheria ambavyo mawakili wa pande zote mbili waliziwasilisha mbele yake katika majumuisho yao ya mwisho.

Alidai kuwa, maamuzi ya Mahakama ya Rufaa katika kesi zile yalisisitiza kuwa lazima kesi ithibitishwe bila kuacha mashaka yoyote, lakini katika hukumu ya Lema, Jaji Rwakibalila imeacha mashaka mengi, ndiyo maana Lema anadai jaji huyo alikosea.

Baada ya wakili Kimomogoro kuwasilisha hoja hiyo iliyodai Jaji Rwakibalila hakutumia maamuzi ya kesi zilizowasilishwa mbele yake na mawakili wa pande mbili, Jaji Massati alisema si lazima jaji au hakimu atumie kesi zilizowasilishwa mbele yake na mawakili katika kutoa uamuzi.

Hoja nyingine ni kwamba, hukumu ya Lema iliegemea katika ushahidi wa mdomo tu bila kuwepo ushahidi wa kuunga mkono kwani mashahidi wa mjibu rufaa, waliotoa ushahidi walidai walimsikia Lema katika mikutano ya kampeni akitoa maneno ya kumdhalilisha na kumkashfu Dk. Batilda, lakini walishindwa kuleta CD, mikanda ya video kuthibitisha.

“Tulimueleza Jaji Rwakibalila kuwa mashahidi wa wajibu rufaa hawaaminiki na kwamba ushahidi wao ulikuwa wa mazingira, lakini jaji katika hukumu yake hakuna sehemu aliyoonyesha kukubali wala kukataa hoja yetu hii,” alidai wakili Kimomogoro.

Wakili huyo alidai pia Jaji Rwakibalila alikosea alivyosema Lema ana bahati kwani hakukamatwa wala kushitakiwa kwa kutoa lugha za kashfa na udhalilisha katika mikutano ya kampeni za uchaguzi wa mwaka 2010.

Kutokana na madai hayo, alidai kuwa Lema anaiomba Mahakama ya Rufaa itamke kuwa Jaji Rwakibalila alitamka neno hilo kwa bahati mbaya na kutamka kwake neno hilo ndiko kulikomsukuma kufikia uamuzi wa kumfungia Lema asigombee kwa kipindi cha miaka mitano.

“Kwa hoja hizo tulizoziwasilisha hapo juu, tunaiomba Mahakama ya Rufani nchini itengue hukumu ya Jaji Rwakibalila kwani haina vigezo wala hadhi ya kuifanya iwe hukumu, na pia tunaiomba mahakama iwaamuru wajibu rufaa walipe gharama za uendeshaji wa kesi hiyo tangu ilipoanza Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na sasa Mahakama ya Rufaa,” alidai wakili Kimomogoro.

Kwa upande wake wakili wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Uchaguzi, Timon Vitalis, alidai kuwa sheria ya uchaguzi haiwaruhusu wapiga kura kufungua kesi ya kupinga ubunge wala wagombea ubunge, udiwani kwani aliyepaswa kufungua kesi hiyo ni Dk. Batilda na siyo wajibu rufaa ambao ni wapiga kura wa Jimbo la Arusha Mjini.

Hata hivyo hoja hizo zilipanguliwa na mawakili wa wajibu rufaa, Aluthe Mugwai na Modest Akida na Wakili wa Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Vitalis.

Mugwai na Akida walitetea kuwa hukumu ile ni sahihi na haistahili kutenguliwa kwani imekidhi matakwa ya kisheria na kuomba mahakama hiyo itupilie mbali rufaa ya Lema.

Mugwai alisema mawakili wa Lema wanaipotosha mahakama kwa kusema hakukuwa na uthibitisho wowote ulioonyesha wajibu rufaa walikuwa wapiga kura wa Jimbo la Arusha Mjini wakati ukurasa wa 10 katika hukumu inayopingwa, inaonyesha namba za vitambulisho vya wapiga kura ambavyo ni vya wajibu rufaa na wakati vikitolewa mahakamani, mawakili hao wa Lema walikuwepo.

Kuhusu hoja ya jaji kwamba alijielekeza vibaya kusema kuwa sheria za Uingereza hazitakiwi kutumika kuamua katika kesi za uchaguzi, Mugwai alidai Jaji Rwakibalila yupo sahihi kwani hata kifungu cha 1(2) cha sheria ya uchaguzi sura ya 343, kinasema masuala yote ya uchaguzi yatashughulikiwa kwa kutumia sheria ya uchaguzi na kuongeza kuwa mawakili wa Lema wametumia kesi za Mahakama ya Rufaa zilizoamriwa kwa sheria ya zamani ya uchaguzi ya mwaka 1985 wakati sheria hiyo ya uchaguzi imeishafanyiwa marekebisho na marekebisho ya mwisho yalifanyika mwaka 2010 .

“Hata kifungu cha 2 (3) cha sheria ya Judicuture and Application of Law (JALA), inakataza matumuzi ya sheria za nje kutumika kuamua kesi za uchaguzi wakati nchi yetu ina sheria mahususi ya uchaguzi kwa ajili ya kuamua kesi za uchaguzi na kwamba jaji alikuwa sahihi kusema hilo na pia alikuwa sahihi kusema wajibu rufaa walikuwa na haki ya kufungua kesi hiyo na kuongeza kuwa hoja hiyo ni butu,” alidai wakili Mugwai.

Hata hivyo, alipinga hoja ya mawakili wa Lema iliyodai Jaji Rwakibalila katika hukumu yake hakutumia kesi walizoziwasilisha mbele yake, ambapo alidai katika hukumu hiyo alitumia baadhi ya kesi walizoziwasilisha mbele yake na kwamba jaji ana mamlaka ya kuchuja kesi anazotaka kuzitumia kwenye hukumu.

Akijibu hoja kwamba hukumu ya Lema iliegemea kwenye ushahidi wa mazingira tu, wakili Mugwai alikanusha na kusema hakukuwepo ushahidi wa mazingira kwani mashahidi waliomsikia Lema akitoa maneno ya kashfa kwenye mikutano ya hadhara, walifika mahakamani hapo na kutoa ushahidi wao ambapo walisema walimwona na kumsikia akfanya hivyo dhidi ya Batilda.

Hata hivyo wakati wakili Mugwai akiwasilisha hoja zake, baadhi ya watu wanaodaiwa ni wafuasi wa CHADEMA ambao walijazana ndani ya chumba cha mahakama, waliguna na kutoa vicheko hali iliyosababisha wakili huyo awaombe majaji wawadhibiti watu wenye tabia hiyo kwani mawakili wa Lema walipokuwa wakiwasilisha hoja zao walitulia.

Rufaa hiyo inayovuta hisia za wengi ndani na nje ya nchi, ilianza kusikilizwa majira ya saa tatu asubuhi na kumalizika saa tisa alasiri.

Kesi hiyo imeahirishwa na sasa kinachosubiriwa ni tarehe ya hukumu ili kukata mzizi wa fitina.

Kwa mujibu wa jopo hilo la majaji wa Mahakama ya Rufaa, tarehe ya kutolewa uamuzi wa rufaa hiyo itatolewa kwa njia ya maandishi kwa mawakili wa pande zote mbili.

mahakamani-leo1Lema akizungumza na wananchi mara baada ya kesi yake kuahirishwa

mahakamani-leo

mahakamani-leo2

Mmmoja wa mawakili wa Lema, Mh Tundu Lissu akifafanua jambo baada ya kesi. Picha kwa hisani ya Saimon Kailanga

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO