Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

ANDISHI LA JULIUS MTATITO MTANDAONI AKIIBUA MJADALA JUU YA SAKATA LA TANESCO/EWURA NA BEI YA UMEME

Juliua Mtatiro, mchambuzi wa masualaya kisiasa

TUIJADILI TANESCO...
1. TANESCO inajiendesha kwa hasara kubwa kutokana na madeni na mikataba mibovu iliyolizingira shirika hilo. Serikali haijawahi kuchukua hatua madhubuti za kuiimarisha TANESCO ili iwe shirika la mfano katika utendaji na uzalishaji wenye faida na tija kwa taifa. Kwa hiyo TANESCO inawategemea wateja wake ili kujikwamua kwa kila kitu jambo linaloifanya TANESCO kuwa mzigo kwa watumiaji wa umeme na wala si serikali. Kila uamuzi utakaofanywa na serikali juu ya TANESCO, wanaoathirika na uamuzi huo ni wananchi.

2. Napongeza uamuzi wa sasa wa Wizara ya Nishati na madini wa kuzuia bei mpya za umeme zisianze kutumika. Bei hizi zenye ongezeko la asilimia 8.5 zilikuwa mzigo kwa mwananchi wa kawaida na si serikali na kwa kweli kuzuia ongezeko hilo ilipaswa kuwa hatua ya kwanza na muhimu kuliko kitu chochote japokuwa uamuzi huo haujatatua tatizo la msingi la TANESCO ikiwa ni pamoja na uwepo wa mambo ya kushangaza yanayohitaji mjadala.
KWA NINI ZUIO HALIKUFANYWA MAPEMA?
Mchakato wa kuongeza bei ya umeme ili kuboresha huduma ya nishati hiyo ulifanywa na TANECO na EWURA na ulikuwa wazi, ulifuata taratibu zote za kisheria zilizowekwa na serikali. Wadau, wananchi na watumiaji wa umeme walikuwa na taarifa ya mchakato huo uliokwenda hadi mwisho na maamuzi kutolewa hadharani kwa notisi. Kinachoshangaza ni kwa nini zuio la Waziri limekuja dakika za mwisho za utekelezaji wa jambo ambalo limefanywa kwa mchakato wa wazi na ambao umeshuhudiwa na kubarikiwa na serikali yenyewe?
KUNA MTU AMETUMBULIWA!
Huyu aliyetumbuliwa kosa lake ni nini? Ni kufuata mchakato wa kisheria na kikanuni na kupandisha bei ya umeme? Kama serikali ilikuwa na nia njema kwa nini haikuizuia EWURA na TANESCO mapema, visiendelee na hatua za namna hiyo? Kwa nini wasubiriwe wafanye maamuzi ya kisheria ndipo Mkurugenzi wa TANESCO afukuzwe? Hivi kweli jamani, tatizo la TANESCO ni mtu (a person) au ni taasisi (an Institution) tena ikiumizwa zaidi na maamuzi mabovu ya wanasiasa?
YA WAMACHINGA NA WACHIMBAJI WADOGO?
Mnakumbuka ni hivi majuzi tu serikali iliacha amri za kuwabomolea wamachinga Mwanza na kwingineko zitawale? Walifukuzwa, wakabomolewa vibanda vyao na kuharibiwa mali zao. Wapo waliopigwa na kuumizwa. Zoezi la kuwahamisha kuwapeleka mahali pasipokuwepo lilipokamilika Ikulu ikaja na RUNGU zito na kuagiza Wamachinga waachwe na wasiguswe, nani alilipa hasara ile kwa wamachinga hadi? Na je, uamuzi wa kuwaacha wapange bidhaa hadi katikati ya barabara umekuwa na tija yoyote? Kuongoza serikali si jambo dogo na la mchezo. Ni kazi inayohitaji hesabu zinazopigwa hadi mwisho. Kwa nini serikali inafanya michezo kwenye mambo makubwa? Kwa nini haina muunganiko na utendaji wa pamoja? Kwa nini inatoa amri kukataza mambo iliyoshiriki au kuyashuhudia tangu yakianza hadi kukamilika?
TATIZO LA MSINGI LA TANESCO LIMEKWISHA?
Hapana, lipo pale pale. Ni ukosefu wa fedha za kujiendesha kisasa, kutoa huduma imara na iliyoboreshwa. Tatizo hili litaendelea kuwepo na ama litazidi. TANESCO inajiendesha kwa hasara, kwa udi na uvumba inahitaji pesa za ziada haraka. Uamuzi mzuri na wenye utata uliofanywa na Wizara kusimamisha utumikaji wa bei mpya za umeme uende sambamba na serikali ku PUMP mabilioni kwenda TANESCO ili kuziba GAPS za upungufu wa fedha uliopo. Vinginevyo na au kinyume chake, kilio kitarudi kwa wananchi wa kawaida ambao wataanza kukosa umeme wa uhakika kila kukicha, na hata uzalishaji katika viwanda vidogo na vikubwa utadumaa sana na kwa hiyo bidhaa zitapanda bei na vitu vitakuwa ghali na mwananchi wa kawaida ndiye ataisoma namba. Tukumbuke umeme ni maisha katika dunia ya sasa.
HATUA NYINGINE MUHIMU?
Moja ni serikali kupitia upya mikataba ya TANESCO na makampuni mengine ambayo yameigeuza kiwa kitega uchumi chini ya mikataba mibovu na ione hatua za kisheria za kufuata ili kuiokoa TANESCO.
Pili, ni serikali kupitia madeni ya TANESCO kuyachambua na kubaini yapi ni sahihi kuendelea kulipwa na yapi hayafai.
Tatu, ni serikali kuacha mikakati ya KUSAKA UMAARUFU kwa mambo makubwa yasiyohitaji mchezo mchezo. UMEME siyo eneo la kulifanyia mchezo, umeme ni roho ya uchumi, TANESCO isigeuzwe kuwa kilinge cha siasa, michakato ya maamuzi ndani ya TANESCO ifanywe kwa usimamizi mzuri wa serikali, kwa uwazi na ukweli. Wasitolewe watu kafara wakati matatizo ya TANESCO yanajulikana na hayakuanza leo au jana.
Nne, hadi sasa hakuna serikali iliyowahi kuja na ajenda inayoeleweka ya kuihuisha TANESCO, hata hii serikali ya sasa ya viwanda haijawa na mkakati imara na wa muda mrefu. Kunahitajika mjadala na mipango ya wazi juu ya namna ya kuikoa TANESCO.
Tujadili.
#JSM, - Julius Sunday Mtatizo
02 Januari 2017,
Musoma
Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO