Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CCM  YASHINDA UBUNGE DIMANI NA UDIWANI KATA 19  KATI YA 20 UCHAGUZI MDOGO 2017


CHAMA Cha Mapinduzi  (CCM), kimeibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa marudio ya ubunge na udiwani, uliofanyika nchini juzi katika maeneo tofauti.

Katika uchaguzi wa ubunge Jimbo la Dimani, mkoa wa Magharibi, Unguja, CCM ilifanikiwa kushinda nafasi hiyo kwa mgombea wake, Juma Ally Juma, kupata kura 4,860 dhidi ya mpinzani wake, Abdulrazak Khatib Ramadhan wa CUF, aliyepata kura 1,234.

Mbali na ubunge, pia CCM imechukua viti vya udiwani katika maeneo mengi ya Tanzania Bara. Kata 20 zilifanya uchaguzi huku CCM ikishinda kata 19 na CHADEMA moja ya Duru ambayo awali ilikuwa upande wao.

Ushindi wa CCM ulipatikana kutokana na jimbo la Dimani kuwa wazi, baada ya kifo cha mbunge wake, Hafidhi Ali Tahir, kilichotokea Novemba, mwaka jana, mjini Dodoma, alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge.

Kwa upande wa udiwani, katika kata ya Lembeni, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, CCM iliibuka kidedea kwa kuigalagaza UKAWA.

Katika uchaguzi huo, ilishuhudiwa ndoa ya UKAWA, ikiwa na mushikeri baada ya vyama vinavyounda umoja huo, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, kila moja kusimamisha mgombea wake.

Aidha, katika uchaguzi huo, mwitikio wa wananchi kujitokeza kupiga kura ulikuwa mdogo tofauti na ilivyotarajiwa.

Wananchi waliokuwa wamejiandikisha kupiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura katika kata ya Lembeni ni 5,866 huku waliojitokeza ni 2,346.

Akitangaza matokeo hayo juzi, saa 3:17 usiku, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Baihaki Msangi, alimtangaza Godwin Mmbaga (CCM) kuwa mshindi kwa kupata kura 1,668, akifuatiwa na Mchome Kapuya (CHADEMA) kura 637 huku Felix Kidema (NCCR-Mageuzi) akipata kura 11.

Kwa mujibu wa msimamizi huyo, kura 30 ziliharibika hivyo kwa mamlaka aliyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alimtangaza Mmbaga kuwa diwani mpya wa kata ya Lembeni.

Kata hiyo imefanya marudio ya uchaguzi wa udiwani baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, aliyechaguliwa mwaka 2015, Joakim Wangabo (CCM), kupangiwa kazi ya ukuu wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.

UBUNGO-DAR ES SALAAM

Katika Jimbo la Ubungo, CCM imeshinda viti vyote vya wajumbe wa Serikali za Mitaa, wajumbe wa viti maalumu na nafasi ya mwenyekiti katika uchaguzi mdogo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, John Kayombo, alisema katika uchaguzi huo, uliojumuisha kata nne ndani ya wilaya hiyo, ikiwemo Msigani, Makuburi, Manzese na Ubungo, CCM imeshinda zote.

Kayombo alisema katika kata ya Msigani, mtaa wa Malamba Mawili, kulikuwa na nafasi tatu zilizoachwa wazi, ngazi ya uenyekiti, wajumbe wawili na mjumbe wa viti maalumu.

Alisema nafasi ya uenyekiti, Iddi Mgweno (CCM), aliibuka mshindi wa nafasi hiyo kwa kura 871 na kumshinda mgombea wa CHADEMA, Abdulile Mwaisaka, aliyepata kura 486.

Nafasi ya wajumbe walioibuka na ushindi ni Adam Kingu, aliyepata kura 800, Maneno Msukuma kura 663, wote wa CCM. Nafasi ya ujumbe wa viti maalumu ilichukuliwa na Zulfa Mwiru, aliyepata kura 869.

Uchaguzi wa viti maalumu katika kata ya Makuburi, mtaa wa Makoka, Dotto Emmanuel alipata kura 402 na kumbwaga mpinzani wake, Diana Mwalusamba (CHADEMA), aliyepata kura 187.

Katika kata ya Manzese, mtaa wa Mnazimmoja, nafasi ya ujumbe ilienda kwa Isaya Gwalinala (CCM), aliyepata kura 387,  Halima Mpinda (CHADEMA) kura 229 na Said Selemani (CUF) kura 95.

Pia, CCM iliwabawaga wapinzani kwenye uchaguzi wa ujumbe katika kata ya Ubungo, mtaa wa Ubungo Msewe, ambapo Rose Ndunguru (CCM) alipata kura 539 na  Tuntemeke Sanga (CHADEMA) kura 344.

Mgombea wa CCM, Mzee Juma alitangazwa mshindi wa nafasi ya ujumbe katika mtaa wa Kajima, baada ya kupata kura 222 kati ya kura 327 zilizopigwa.


KIJICHI, DAR ES SALAAM

CCM Mkoa wa Dar es Salaam, kimewapongeza wana-CCM wa kata ya Kijichi, wilaya ya Temeke, kwa ushindi wa kumpata diwani mpya wa kata hiyo, Tausi Milanzi, katika uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika juzi.

Tausi, alishinda nafasi ya udiwani, kufuatia aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Underson Charles kufariki dunia.

Katika uchaguzi huo, CCM ilishinda kwa kupata kura 2,572, CUF (1046), CHADEMA (764), ACT wazalendo (670), ADC (56), NRA (17), UDP (70) na AFP (7).


MKOANI MBEYA

Mkoani Mbeya, CCM iliibuka na ushindi kwa kunyakua vijiji saba wakati CHADEMA imeambulia viwili. Kwa upande wa vitongoji, CCM iliibuka na ushindi kwa kuchukua vitongoji 11 huku CHADEMA ikipata saba.

Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Lobe Zongo, akizungumza jana na mwandishi wa habari hizi, alisema kwa upande wa wajumbe, CCM imevuna wajumbe 40 huku CHADEMA ikiambulia sifuri.

Zongo alivitaja vijiji, ambavyo CCM imeshinda na kata zikiwa kwenye mabano kuwa ni Isanga na Itope (Bujonde), Matema na Kisyosyo (Matema), Tenende (Tenende), Fubu (Ikama) na Kajunjumele (Kajunjumele).CHADEMA imeambulia vijiji vya Masebe (Ngusa) na Ipinda (Ipinda).

Aliongeza kuwa kwa upande wa vitongoji, CCM imeshinda vitongoji vya Seko, Kikusya, Mpunguti B, Isimba, Ilopa, Njisi, Mwega, Kasumulu Chini, Kasyunguti, Mbasi na Kilombero huku CHADEMA ikishinda vitongoji vya Mbugujo, Kilambo, Mpunguti, Lugoje, Mbwata, Lyongo na Ilindi.

“Uchaguzi huu umetupa sura na mwanga wa namna gani tunavyotakiwa tujipange, ili kuboresha zaidi huduma za kijamii. Ikumbukwe kwamba jambo lolote lile lina maandalizi yake,” alisema Zongo.

Aliongeza: "Hata shamba huwa linaanza kwa kuandaliwa, kukatua, hatimaye kuchoma, kulima na mvua itakaponyesha ndipo mkulima anapanda mbegu. Lakini kuna kupalilia hadi hatimaye unavuna, hivyo CCM mkoani hapa mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2015, walikuwa wanaendelea kujipanga," alisema.

Kwa mujibu wa Zongo, walikuwa wanaendelea kutengeneza ustawi wa maandalizi ya uchaguzi ujao na ndiyo maana uchaguzi mdogo wa vijiji na vitongoji wilayani Kyela ni mwanzo tu kwani CCM imejiandaa zaidi ya pale.

Hata hivyo, alisema wanaendelea kutengeneza mazingira ili mwaka 2019, kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, Chama kiweze kufanya vizuri zaidi, hivyo alitoa wito kwa wana-CCM mkoani hapa kuanza maandalizi mapema.

MKOANI MWANZA

CCM imeibuka kidedea katika uchaguzi mdogo wa marudio wa udiwani katika kata za Malya wilayani Kwimba na Kahumulo wilaya ya Sengerema.

Katibu Mwenezi wa CCM mkoani Mwanza, Simon Mangelepa, alisema ushindi wa kishindo walioupata ni fundisho kwa CHADEMA na washirika wake wa UKAWA.

Katika kata ya Malya, mgombea wa CCM, Kasmili Kusekwa aliwabwaga wapinzani wake baada ya kupata kura 1,730 (sawa na asilimia 53.3), akifuatiwa kwa mbali na mgombea wa CUF, aliyepata kura 873 huku mgombea wa CHADEMA akivuta mkia kwa kura 604.

Aidha, katika kata ya Kahumulo, Fortunatus Nzwagi (CCM) alizoa kura 1,395 (sawa na asilimia 69.30) na kuwabwaga wagombea wa CHADEMA (kura 581) na CUF kura 35.

Mangelepa alisema Chama kinawashukuru wananchi na wana-CCM wote wa kata hizo kwa kuendelea kukiamini, kukichagua na kuwataka wanachama wengine watakaotaka kugombea nyadhifa kama hizo, waende kwa utashi na sio pesa.

MKOANI ARUSHA

Kwa upande wa Arusha, CCM ilishinda katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata za Mateves na Ngarenanyuki za wilayani Arumeru mkoani hapa.

Uchaguzi huo, ambao ulifanyika juzi, ulikuwa wa marudio kutokana na mgombe wa CCM wa kata ya Ngarenanyuki, Naftali Mbise kufariki dunia mwaka jana.

Katika kata ya Mateves, uchaguzi huo ulirudiwa kwa sababu Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, ilitengua udiwani wa Abel Jereimia (CHADEMA) mwaka jana.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa kata ya Ngerenanyuki, Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo, ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeni, alisema watu waliojiandikisha ni  4,387 na waliopiga kura 2,434.

Kazeni alisema katika kura hizo, zilizopigwa halali zilikuwa 2,394 na zilizokataliwa 40 na kwamba, mgombea wa CCM, Mwalimu Zakaria Nnko aliibuka mshindi kwa kupata kura 1,625, huku mgombe wa CHADEMA, Aminiel Mungure, akipata kura 764 na mgombea wa CUF kura 15.

Kuhusu uchaguzi wa kata ya Mateves, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Dk. Wilson Charles, alisema waliojiandikisha ni 7,677 na waliopiga kura 2,760.

Dk. Charles alisema kura halali zilikuwa 2,731 na zilizokataliwa 29.

Alisema mgombea wa CCM, Julius Savoyo aliibuka mshindi kwa kupata kura 1,322 huku mgombea wa CHADEMA, Abel Jeremia kura 854, mgombea wa NCCR-Mageuzi, Makini Kleruu kura 547 na mgombea wa CUF, Ramadhani Rashid akiambulia kura nane.

SONGEA KUKOJE?

CCM mkoani Ruvuma kimeibuka na ushindi wa kishindo baada ya wagombea wake wa nafasi za udiwani kushinda katika kata mbili za Tanga na Maguu.

Katika kata ya Maguu iliyoko wilayani Mbinga, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Caspar Mahay, alimtangaza Manfred Kahobela kuwa mshindi baada ya kujizolea kura 2,355 na kumbwaga Bahati Mbele wa CHADEMA aliyepata kura 1,717.

Katika kata ya Tanga, iliyoko Manispaa ya Songea, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Tina Sekambo, alimtangaza Agaton Goliyama (CCM), kuwa mshindi baada ya kupata kura 1867, akiwashinda wagombea wa CHADEMA, Vinitan Soko (722), ACT Wazalendo, Swaiba Mapunda(2) na Adolf Ngonyani wa CUF aliyepata kura 15.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Kahobela wa kata ya Maguu, aliwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kukiamini chama.

Naye, Goliyana wa kata ya Tanga, alisema ushindi wa CCM umedhihirisha wazi namna ambavyo Watanzania wanavyoendelea kukiamini Chama kutokana na utekelezaji wa yale, ambayo yaliahidiwa katika Ilani ya CCM.


KUTOKA KAHAMA

Mgombea wa udiwani wa kata ya Isagehe, wilayani Kahama, Charles Mkonge, alifanikiwa kuibuka kidedea baada ya kumshinda Ibrahim Masele wa ACT-Wazalendo.

Katika uchaguzi huo, Mkonge alipata kura 1562 dhidi ya Masele aliyepata kura 578.

Wengine ni Richard Diru (CHADEMA) kura 439, Machelo Juma (CUF) aliyepa kura 30, Toufick Salum (CHAUMA) kura 11 na Joseph Kasubi (NCCR-Mageuzi) aliyepata kura 71.

Akisoma matokeo hayo, Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi huo wa kata ya Isagehe, Jarome Lugome, alisema waliojiandikisha kupiga kura ni 5,470, waliopiga kura ni 2,740, kura halali ni 2,691 na zilizoharibika ni kura 49 kati ya vituo 17 vya kupigia kura.

CHANZO: UHURU
Washirikishe Google Plus

About Unknown

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO