Kamanda Charles Mkumbo, RPC Arusha |
Madiwani wawili wa Halmashauri ya Karatu mkoani Arusha, Lazaro Gege wa Kata ya Mang’ola Barazani (CCM) na Moshi Darabe wa Kata ya Baray (CHADEMA) wanaendelea kushikiliwana Jeshi la Polisi kufuatia sakata la kuchomwa moto mashine za maji Wilayani Karatu.
Awali watu 11 wakiwemo madiwani hao wawili wa CCM na CHADEMA, walikamatwa na polisi wilayani Karatu wakituhumiwa kuharibu mali, zikiwemo mashine zaidi ya 10, za kunyonya maji kwa kuzipondaponda na kuzichoma moto kwa madai zimewekwa kwenye vyanzo vya maji.
Mbali na hilo, watu hao wakiwemo madiwani, wanadaiwa kuteketeza kwa moto kibanda umiza kimoja.
Hadi sasa mashine zilizothibitika kuchomwa moto ni tano, tatu zikiwa za Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Wilaya ya Karatu, Daniel Awakii na mbili za Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Karatu, Mustafa Mbwambo.
Nyingine ni mashine za wakulima, ambao wote waliitwa polisi kwa ajili ya kuandikisha maelezo.
Aidha, Mbunge wa Karatu, Willium Qumbalo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jubilet Mnyenye, waliitwa Kituo cha Polisi Karatu kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na sakata hilo.
Tukio hilo linatokea siku chache baada ya kumalizika kwa ziara ya Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, ambaye alipokea kilio cha wananchi wa vijiji vinavyotumia maji hayo vikiwemo Qamndet, Barazani, Dumbechan, Maleckchand na Laghangareri, ambapo aliagiza uongozi wa serikali ya mkoa na wilaya, kuhakikisha ndani ya siku moja mashine zote zilizoko katika vyanzo vya maji zinaondolewe na kuwekwa umbali ya mita 500.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo amenukuliwa na gazeti la Mzalendo la Januari moja 2017 akieleza kuwa hajatoa amri ya mtuhumiwa yeyote kupewa dhamana labda tu kama itakwenda kutokea mahakamani siku ya Jumatatu.
Kujua sakata hilo zaidi soma hapa na hapa
0 maoni:
Post a Comment