Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Bw. Adam Mayingu, (kulia), akipeana mikono na Katibu Tawala Msaidizi (anayeshughulikia masuala ya serikali za mitaa), jijini Dar es Salaam, Bi. Merry Assey, baada ya kufungua semina ya mafunzo kwa watumishi wa Ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Dar es Salaam, iliyoandaliwa na Mfuko huo na kufanyika Januari 3, 2017 kwenye makao makuu ya PSPF Golden Jubilee Towers jijini Dar es Salaam.
NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
MFUKO wa Pensheni wa PSPF, umeendesha semina ya mafunzo kwa watumishi wa Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, ili kuwajengea uwezo wa kushughulikia matatizo ya wananchi ambao ni wanachama wa Mfuko huo.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yameanza leo Januari 3, 2017, na kufunguliwa na Katibu Tawala Msaidizi (sehemu ya serikali za mitaa), Bi. Merry Assey kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa ea Dar es Salaam, Paul Makonda.
“Niipongeze PSPF kwa kuandaa semina hii ambayo inatoa fursa ya watumishi hawa waliohudhuria katika mafunzo haya kuelewa huduma na shughuli zinazofanywa na Mfuko huu na kwa maana hiyo iwe rahisi kwenu kutatua kero za wananchi wanaofika pale Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kutafuta ufumbuzi hususan kwa wanachama wa Mfuko huu,.” Alisema Bi. Assey, wakati akifungua semina hiyo.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Bw. Adam Mayingu, alisema, PSPF ilifikia uamuzi wa kuandaa semina hiyo kufuatia wazo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye alitaka kujengewa uwezo kwa watumishi wa Ofisi yake ili waweze kuwahudumia vema wananchi wakiwemo wanachama wa PSPF.
“Nililipokea wazo hilo na sisi PSPF tukaona ni fursa nzuri kwa kuwaelimisha watumishi hawa ambao, ninahakika baada ya mafunzo haya, watakuwa mabalozi wetu wazuri lakini pia na wao watajiunga na Mfuko huu.” Alisema Bw. Mayingu.
Mada mbalimbali zilitolewa kwa wanasemina hao ikiwa ni pamoja na ile ya shughuli za Mfuko iliyotolewa na Mkurugenzi wa Huduma wa Mfuko huo, Bi. Neema Muro, Kaimu Meneja Mafao, Haji Moshi na Maafisa wengine wa Mfujko huo. PICHA ZAIDI ZA SEMINA HII/>BOFYAHAPA
0 maoni:
Post a Comment