Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga kufuatia vifo vya watu 12 vilivyosababishwa na kuzama kwa boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Tanga kwenda Pemba.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia tarehe 10 Januari, 2017 katika kisiwa cha Jambe kilichopo katika bahari ya Hindi umbali mfupi kutoka Tanga Mjini, ambapo pamoja na vifo vya watu hao watu wengine 33 wamenusurika na 25 kati yao wamelazwa katika Hospitali ya Bombo Mkoani Tanga.
"Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii ya kuzama boti, tumepoteza wapendwa wetu, watoto wetu na watu wazima ambao kwa hakika familia zao ziliwategemea katika maisha ya kila siku, nakuomba Ndg. Mkuu wa Mkoa unifikishie pole nyingi kwa familia za Marehemu wote na jamaa zao" amesema Dkt. Magufuli katika salamu hizo.
Aidha, Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na pia amewataka wote walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki cha huzuni ya kuondokewa na jamaa zao.
Dkt. Magufuli pia amewatakia matibabu mema majeruhi wote walionusurika katika ajali hiyo ili wapone haraka, warejee katika familia zao na waendelee na ujenzi wa Taifa.
"Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe, Amen" Amemalizia Rais Magufuli.
0 maoni:
Post a Comment