HABARI NA MAGAZETI
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharifu Hamad jana alisema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ambaye yupo mahabusu tangu mwishoni mwa mwaka jana bado ana ujasiri ule ule.
Aidha, Maalim Seif ambaye alimtembelea Lema jana katika Gereza Kuu la Arusha la Kisongo, alisema amemkuta Mbunge huyo akiwa mwenye furaha kubwa.
Aidha, akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa kwenye uwanja wa ndege wa Arusha, Maalum Seif alisema Lema ameonyesha ujasiri mkubwa.
"Dhamira kuu iliyonileta hapa ni kimuona Lema, ambaye amewekwa mahabusu kwa zaidi ya miezi miwili, baada ya Mahakama mkoani hapa kumnyima dhamana," alisema.
Lema yupo mahabusu baada ya kushtakiwa tuhuma za kutoa taarifa za uchochezi na kumkashifu Rais Dk. John Magufuli.
"Dhamira kuu iliyonileta hapa ni kumtembelea Mbunge Lema, nimeweza kumuona na kuzungumza naye. Bado yupo na ujasiri ule ule na furaha kubwa."
Alisema jambo linalomtia moyo ni kumkuta Lema akiwa salama na bado hajavunjika moyo wa mapambano ya kutafuta haki na kuwa kwake gerezani kumempa nafasi zaidi ya kutafakari.
"Kama kuwekwa gerezani ndio njia pekee ya kumnyamazisha kuzungumza atakapotoka, basi wamekosea," alisema Maalim Seif ambaye aliwahi kukaa kizuizini.
"Tumaini languni atakuwa shujaa na jasiri (kuliko) hata kabla ya kukamatwa."
Lema alisafirishwa na polisi usiku kutoka Dodoma alipokuwa akihudhuria vikao vya Bunge mwishoni mwa mwaka jana mpaka hapa Arusha baada ya kukamatwa, na tangu Novemba 2 amekuwa ama mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi Arusha au Kisongo.
Awali kabla ya kumtembelea Lema, Maalim alikuwa amefanya mazungumzo na kituo cha televisheni cha Azam na kudai kuwa tangu kumalizika kwa muda wake katika nafasi ya Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, hakuwahi kulipiwa na serikali gharama za safari zote alizokwenda nje ya nchi ingawa ana haki ya kulipiwa.
Maalim Seif, akizungumza jana katika kipindi cha Funguka, alisema kuwa licha ya kutambua kwamba ana haki ya kulipiwa na serikali gharama za matibabu, ameamua kujilipia mwenyewe.
“Nilisema hapana nitajipiga mwenyewe kwa kifua (changu). Na nina haki kikatiba kulipiwa na serikali," Maalim Seif alisema. "Kwa sababu nina haki kama viongozi wengine wastaafu (kupewa huduma) kama vile matibabu, walinzi, posho ya kila mwezi, matumizi ya VIP maeneo mbalimbali."
Alisema kuwa kwa sasa afya yake iko vizuri na kwamba safari zake za India zilikuwa kwa ajili ya kuangalia kama ana matatizo ya kiafya.
“Nipo ngangari kinoma, nilienda India kwa kucheki afya yangu, mara moja nilikwenda kwenye upasuaji na baada ya hapo nilikaa wiki moja nikarudi nchini na nikashauriwa kupumzika kidogo na baadaye nikarejea kazini," alisema.
"Kwa hiyo, mtu kuumwa ni jambo la kawaida hata angekuwa mtoto au kijana anaweza kuumwa," aliongeza na kukiri kuwa serikali bado inampatia baadhi ya huduma licha ya tishio la hivi karibuni la kumnyima msaada wa serikali kutokana na kitendo chake cha kumnyima mkono Rais wa Zanzibar.
"Ninaishi vizuri na familia yangu, nilipata marupurupu yangu baada ya kustaafu, lakini pia haki za viongozi wastaafu kama posho, walinzi matibabu napata, na wala serikali isidhani inafanya hisani bali ni haki yangu,” alisema.
UCHEPUSHAJI WA RUZUKU
Maalim Seif pia alisema wanashauriana na mawakili wao ili kuangalia uwezekano wa kulipeleka mahakamani sakata la ruzuku ya mamia ya milioni ya shilingi ya ruzuku ya CUF yanayodaiwa kuchepushwa na kuliwa na watu wachache.
“Kwanza sisi hatua tulizochukua tumemuandikia barua Msajili wa (Vyama vya Siasa), Gavana wa Benki Kuu na nakala tumempa kiongozi wa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. "Hatujui watachukua hatua gani, lakini sisi tunashauriana na mawakili wetu ili kuangalia uwezekano wa kuipeleka kesi hii mahakamani," alisema.
Alisema ameshangazwa na hatua ya Msajili kutoa fedha za ruzuku na kumpa Prof. Lipumba wakati awali alimuandikia barua kumuuliza sababu za kutokipatia ruzuku chama chao na kuelezwa kuwa amezuia kutokana na chama hicho kuwa na mgogoro wa kiungozi.
“Fedha zimekwenda kwenye akaunti ambayo bodi ya wadhamini wa CUF hawaijui na wala Katibu Mkuu, fedha za ruzuku ni za serikali na za walipa kodi na halafu zitakaguliwa na CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali). Sasa hizi milioni 290 ambazo msajili kampa (Prof. Ibrahim) Lipumba zitakaguliwaje wakati hazijaingizwa akaunti ya chama?" Alihoji.
Alisema pamoja na Msajili kudai kumtambua Prof. Lipumba, alipaswa kutambua pia kwamba katiba ya CUF inabainisha kuwa Katibu Mkuu ndio mwangalizi wa fedha na mali zote za chama na si Mwenyekiti wa chama hicho.
“Kwanini apewe fedha Mwenyekiti ambaye hahusiki na uangalizi wa fedha za chama, zile fedha ndio zimeshapotea, nani atazikagua?
Katibu huyo aliongeza: "Mimi - Katibu Mkuu bado natambulika na hajaniletea barua yoyote ya kwamba mimi si Katibu Mkuu tena.
Mimi ni Katibu Mkuu na najua dhamana ya ukatibu mkuu kumpelekea fedha mtu yeyote mwingine ni kinyume cha katiba.
“Msajili alikuwa na sababu gani kupeleka fedha kwenye akaunti ambayo bodi ya wadhamini na katibu mkuu hawaijui, hivyo hajui katiba ya chama inasema nini? Fedha hizi zilipelekwa kwenye akaunti mpya ambayo ni ya wilaya ya Temeke, sasa wilaya ya temeke hakuna watia saini. Msajili anajua mchezo alioucheza."
MGAWANYIKO CUF
Maalif Seif alidai kuwa yote yanayotokea ndani ya chama hicho kwa sasa yanaonyesha Prof. Lipumba anasaidiwa na nguvu ya dola.
“Profesa anasaidiwa na dola kama mkoa wa Lindi na Mtwara, taarifa ilitolewa polisi juu ya kuomba kibali cha kufanya mkutano wa ndani na polisi walikubali, lakini baadaye polisi hao hao alikuja OCD na kudai barua aliyotupa na akasema kikao hamna eti kuna Katibu kakataa, ni nani huyo wakati katibu ni mimi?” Alihoji.
KUGOMBEA 2020
Maalif Seif alisema anatarajia kuwa rais wa Zanzibar muda mfupi ujao huku akisema atafanya uamuzi wa kuwania au kutowania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 baada ya kuangalia hali halisi ya kisiasa.
“Hilo suala tusubiri wakati wake tuonaje, tunafanikiwa au hatufanikiwi halafu baada ya hapo ndio tutafanya uamuzi, lakini kugombea 2020 tusubiri muda ufike na kuangalia hali halisi ya kisiasa,”alisema Katibu huyo.
SULUHU MGOGORO ZENJI
Katibu Mkuu huyo alisema hakuna dawa nyingine yoyote ya kumaliza mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar isipokuwa vyama vya siasa kushirikiana katika kujenga visiwa hivyo.
“Kama kila upande utakubali kwamba Zanzibar kuna tatizo, kila upande ukubali kwamba kuna haja kila kiongozi kupata ufumbuzi au uamuzi wa matatizo hayo na kwa kushirikiana pamoja. Kuwapo na meza ya mazungumzo kunawezekana, lakini kila mmoja akiri kwamba kuna tatizo na anaenda kuondoa tatizo,” alisema Maalim Seif.
KUACHANA NA CUF
Maalim Seif alisema hajawahi kufikiria kuunda chama kingine kwa kuwa yeye ni mmoja wa waanzilishi wa CUF na alivuja jasho na viongozi wenzake kukiimarisha chama hicho.
“Nitakuwa msaliti mkubwa sana, sijawahi kufikiria na kuwaza kuunda chama kingine, mimi ni mwana-CUF kindakindaki na nitaendelea kuwa mwanachama kindakindaki," alisema.
UCHAGUZI DIMANI
Maalim Seif alizungumzia uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani visiwani Zanzibar uliofanyika Januari 22 na kudai kuwa "ulitekwa na majeshi" kwa kuwa baadhi ya wapigaji kura walipelekwa kwenye vituo vya kupigia kura na magari ya jeshi.
Maalim Seif pia alisema hawezi kustaafu kwa sasa kwa sababu bado hajatimiza ahadi aliyowaahidi Wazanzibar.
“Ngoja kwanza nipate haki yangu, nikishapata haki yangu, CUF ikaongoza Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa uchaguzi unaokuja na hapo ndiyo nitafikiria, lakini kwa sasa ni lazima tupate haki yetu, niliwaahidi Wazanzibar kuwa nitawatumikia na kupata haki yao, tukishaipata haki na mimi nikawa Rais, na mimi naziona dalili hizo,” alisema.
Imeandikwa na Allan Isack, ARUSHA, Agusta Njoji, DODOMA na Gwamaka Alipipi, DAR
CHANZO: JAMJICHO
0 maoni:
Post a Comment