Nora Damian
SERIKALI ya China imesema kuanzia mwaka huu itaanza kutoa ufadhili wa Watanzania 100 kusoma nchini humo katika fani mbalimbali.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, kulikuwa na zaidi ya Watanzania 700 nchini humo wanaoendelea na masomo ya elimu ya juu. Akizungumza Dar es Salaam jana, Balozi wa China nchini, Lu Youqing alisema ufadhili huo mpya utakuwapo baada ya Watanzania waliokwenda kumaliza masomo yao na kurejea.
“Tutaendelea kuongeza nguvu katika mafunzo ya raslimali watu kwa kuongeza idadi ya Watanzania kwenda kusoma China,” alisema Youqing.
Balozi huyo alisema hadi sasa uwekezaji wa China nchini umeongezeka na kufikia dola 339 milioni za Marekani na kwamba, wajasiriamali 40 kutoka nchini humo tayari wamewekeza katika miradi mbalimbali nchini. Balozi Youqing alisema miradi hiyo ni uendelezaji wa kilimo cha mkonge, kituo cha kurusha matangazo ya digital cha Star na mradi wa pamoja kati ya Tanzania na China katika uendeshaji meli.
Pia, alisema zaidi ya Watanzania 1,000 wameajiriwa katika mashamba ya mkonge na kwamba, wanazalisha tani 2,000 za mkonge kwa mwaka. Alisema tayari ujumbe wa wataalamu kutoka China unatarajia kuwasili nchini kukagua mfumo wa reli ya Tazara kwa ajili ya matengenezo. Alisema wataendelea kusaidia Tanzania kuendeleza kilimo hasa kupitia sera ya Kilimo Kwanza na ukanda wa kusini wa kilimo.
Source: Mwananchi
0 maoni:
Post a Comment