JOTO la kupinga marekebisho ya sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2012 limezidi kushika kasi baada ya Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) kutangaza kuiburuza mahakamani Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
Marekebisho hayo yaliyopitishwa na Bunge Aprili 13, mwaka huu na kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete yanabainisha kuwa mwanachama wa mfuko wowote wa hifadhi ya jamii hataruhusiwa kuchukua mafao yake kwa sababu yoyote mpaka hapo atakapofikisha miaka 55 au 60.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo Bisimba, ndiye alitangaza kusudio hilo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwasilisha taarifa ya hali ya ukiukaji wa haki za binadamu katika kipindi cha nusu mwaka (Januari-Juni 2012).
Bisimba alisema kituo chake kipo katika mchakato wa kuiburuza mahakamani Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kitendo chake cha kuwanyima haki wanachama wa mifuko ya Jamii kutochukua mafao yao mpaka watakapofikisha umri wa miaka 55 au 60.
Alibainisha kuwa marekebisho ya sheria hiyo yanakiuka haki za wanachama ambao wamekuwa wakijinyima na kuweka fedha zao katika mifuko hiyo ambayo imekuwa ikizitumia fedha hizo kwenye miradi mbalimbali kwa lengo la kukuza kipato cha mfuko husika.
Bisimba alisema Watanzania wengi hivi sasa wanaishi kati ya miaka 45 hadi 52, hivyo kuwawekea masharti kwamba wachukue fedha zao mpaka hapo watakapofikisha miaka 55 ni kuwanyima haki yao ya kiuchumi na kijamii.
Aliongeza kuwa Tanzania haiwezi kujinasibu kuwa inafuata sheria za kimataifa kwa sababu bado haijafikia utaratibu wa nchi zilizoendelea ambazo hutoa mafao mapema zaidi mara mhusika anapostaafu.
“Sheria hii ilipitishwaje bila kuwashirikisha wanachama wenye haki na fedha zao zitumikeje? Mbona hatujalisikia Bunge likizungumzia jambo hili ambalo sasa linaonekana kuwagawa zaidi wafanyakazi?” alihoji.
Nacho Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), kimepinga agizo lililotolewa na Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), kikisema agizo hilo ni kinyume cha sheria ya mkataba wa wafanyakazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Sudi Madega, alisema kinaunga mkono uamuzi wa kwenda mahakamani kupinga sheria hiyo kulikotangazwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Madega alichanganua kuwa endapo serikali itapitisha agizo hilo bila kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwamo TALGWU, itakuwa imekinzana na sheria za ajira ya mkataba kwa wafanyakazi.
“Makubaliano ya mkataba ni jambo la kuzingatiwa sana, kwa sababu si jambo jepesi, kuingia mkataba na mfanyakazi kwa miaka mitano, baada ya hapo ukamweleza malipo ya kiinua mgongo hadi afikishe umri wa miaka 50 au 60, unamuweka katika wakati gani hapo?” alihoji Madega.
Aidha, alisema kuwa Talgwu hakikubaliani, wala haijaridhishwa na hatua ya serikali ya kubadili mfumo wa sheria ya kazi kwa sababu ni gandamizi na imedhamiria kuwaumiza wafanyakazi wa hali ya chini wakati bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya mishahara midogo isiyokidhi.
Naye wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa, alisema kuna umuhimu wa kuangalia upya sheria iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni kutokana na kuonekana kuwa ni kikwazo kwa wanachama wa mifuko hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Mgongolwa alisema kuwa sheria inatengenezwa ili itumike, ikidhi mahitaji na kufaidisha watumiaji lakini marekebisho yaliyofanywa hivi sasa yanapingwa na watumiaji ambao wamekosa imani nayo.
Alisema ni vema watunga sheria wakaangalia namna ya kuunda sheria nyingine kwa kuwa sheria ya mifuko hiyo imeshindwa kukidhi mahitaji ya watumiaji.
“Sayansi ya sheria ni ile inayowasaidia watumiaji lakini sheria ambayo inaletwa na kushindwa kuwasaidia ni heri hiyo sheria ikavunjwa na kutafuta nyingine itakayofaa,” alisema.
Sheria hiyo pamoja na kuzuia fao la kujitoa na kutoruhusiwa kuchukua mafao yao, mwanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (NSSF) atapata fursa ya kupata mikopo ya nyumba kwa kutumia dhamana ya michango yake kama ilivyoelezwa kwenye sheria ya SSRA.
Mwanzoni mwa wiki SSRA ilitoa taarifa juu ya marekebisho hayo kuhusu kuzuia mafao ya kujitoa yaliyofanyika ili kutimiza lengo na madhumuni ya hifadhi ya jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu maisha ya uzeeni.
Source: Tanzania Daima
0 maoni:
Post a Comment