Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MAKALA: Funga ya Ramadhani ana mazingatio yake

SALAAM alaykum, mpenzi msomaji, Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu na kuneemesha neema kubwa kubwa na ndogo, anatukutanisha katika funga ya Ramadhani ambapo leo hii tukiwa Ramadhani ya Saba, ndani ya kumi la kwanza.

Tunajua yapo mengi ya kutafakari namna tulivyouacha mwezi wa Ramadhani uliopita wa mwaka 1432 Hijiria na kuingia katika 1433 Hijiria.

Na mwenye kumuamini Allah (SW) na siku ya mwisho, basi na amkirimu mgeni wake ambapo kwa huu mwezi maridhiwa wa Ramadhani, hatuna ugeni adhimu kabisa kuliko ujio huu. Ni vizuri kuutumia na jilazimishe kunufaika nao kwa kuutendea haki zake unazostahiki kupewa.

Miongoni mwa haki zake kuu ni:

1) Kufunga Swaumu kwa kujizuilia na vyenye kufuturisha (kufunguza) kuanzia alfajiri inapodhihirika mpaka kuzama kwa jua na kwa kunuia kwa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu (S.W).

2) Kutenda haki ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhan kwa kuukirimu kwa matendo yanayompendeza Muumba wetu kama vile kula daku, kuharakisha kufuturu na kuzidisha kuomba toba (msamaha) kila wakati.

Kwa mujibu wa hadithi kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu 'Anhu) amesema; Amesema Mtume (S.A.W), kuleni daku kwani hakika chakula cha daku kina baraka ndani yake. (Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim)

Pia imepokewa kutoka kwa Sahl bin Sa’ad (R.A), hakika mjumbe wa Mungu (S.A.W) amesema, watu watakuwa bado wapo katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha futari.

3) Kuchuma kutoka kwake mafunzo ya ucha Mungu kwa kukithirisha kisimamo cha usiku, kusoma Koraan, kutoa sadaka, kwenda ‘Umrah, kukaa itikafu, kurejesha haki za watu na kadhalika.

4) Kunufaika na usiku mmoja maalumu wa Ramadhan ambao ni usiku mtukufu kuliko usiku wowote katika mwaka.

Nako ni kuutafuta usiku wa cheo (Laylatul-Qadr), usiku huu ulio bora kuliko miezi Elfu moja, kama ushahidi wa Qoran unavyothibitisha, upo katika siku moja kati siku za mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ingawa zaidi inadhaniwa kuwa katika siku miongoni mwa kumi la mwisho la Ramadhan.

Kutoka kwa Mama ‘Aisha (R.A) amesema; Mtume (S.A.W), utafuteni usiku wa cheo Laylatul-Qadr, katika siku kumi za mwisho za Ramadhaan, (Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim).

5) Kuzisubiria shida zake ndogo ndogo Ramadhani kama vile kutokula mchana, kutofanya tendo la ndoa na uchovu wa kisimamo cha usiku.

Hapa ni kuelewa kwamba ingawa funga ya Swaum ni faradhi kwetu Waislamu, lakini hatuna budi kukiri kwamba subira kubwa yahitajika katika kuitendea haki Ramadhani kwa kutokula na mengineyo.

Hata hivyo, subira hii haiendi bure bila ya malipo kama Alivyosema Allah (S.A.W) ndani ya Koraan.

Enyi mulioamini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni imara, na mcheni Allah ili mpate kufaulu.

(Aal-‘Imraan: 200)

6) Kujiepusha kwa kiwango cha juu zaidi kuliko siku nyenginezo, kumbughudhi mwanaadamu mwenzako kwa kutenda maovu kama vile kusengenya, kufanya israfu ya chakula, kuiba, kuzidisha kulala, kusema uongo na mfano wa hayo.

Amesema Mtume (S.A.W) na yeyote asiyeacha kusema maneno mabaya na vitendo vibaya basi hana haja kuacha chakula chake na maji, yaani hana sababu ya kufunga. (Al-Bukhaariy)

7) Kumuomba Mola maghfirah (mshamaha) kwa kupitia kivuli hiki cha Ramadhan:

Basi atakayefunga Ramadhan kwa imani na kutaraji malipo, atafutiwa madhambi yake yaliyotangulia.(Al-Bukhaariy na Muslim).

Hizo ni baadhi tu ya haki zake Ramadhan, nasi kwa upande wetu tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba tunanufaika na Ramadhani kwani ndiyo sababu ya sisi kuweza kuepuka ghadhabu na adhabu za Allah.

Tunamuomba Mola atujaalie kunufaika na Ramadhan kwa haki yake inayotakiwa pamoja na kutuwezesha kuyatenda yale yote aliyoyaamrisha yeye Muumba na kutufundisha Mtume wetu Muhammad (S.A.W).

Kwa hali hii ni lazima makundi ya Waislamu, vijana kwa wazee, wanawake kwa wanaume, matajiri kwa masikini, weusi na weupe, wagonjwa kwa wazima kutambua kuwa sasa mgeni wetu mtukufu Ramadhani ameingia na huu ni wakati muafaka wa kukaa kitako na kuipangia mikakati Ramadhani yetu.

Mgeni ameshafika mlangoni na ameshabisha hodi kwa nguvu zote, basi mfungulieni mlango na mumtandikie zulia la upendo na ukarimu akae.

Huu ndiyo mwezi wa Ramadhani ambao ndani yake kuna fadhila nyingi na matunda yake mtakuja kuyaona mbele ya Muumba. Kuna mazingatio makubwa katika Swaum hapa duniani kama vile kujua hali za mafakiri na masikini, kulikausha tumbo na kulifanya kuwa na afya zaidi na mengineyo zaidi.

Source: Hassan Rashid; Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO