na Happiness Katabazi
RAIS wa Chama cha Madaktari Nchini (MAT) Dk. Namala Mkopi jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, chini ya ulinzi mkali wa polisi akikabiliwa na makosa mawili.
Wakili wa serikali Tumaini Kweka na Lasdiraus Komanya mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba walidai kuwa mshtakiwa ambaye ni Daktari wa Hospitali ya Kijitonyama anakabiliwa na makosa hayo likiwemo la kudharau amri halali ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Wakili Kweka alidai kuwa shtaka la kwanza ni la kudharau amri ya mahakama kinyume na kifungu cha 124 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Alidai kuwa kati ya Juni 26 na 28 mwaka huu, Dk. Mkopi akiwa ni rais wa Chama cha Madaktari alidharau amri halali ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ya Juni 26 mwaka huu, ambayo ilimtaka mshtakiwa huyo kwenda kwenye vyombo vya habari kuwatangazia wanachama wa chama hicho wasitishe mgomo kwani ulikuwa ni batili.
Mahakama hiyo ya Divisheni ya Kazi Juni 22 mwaka huu, ilitoa amri kama hiyo ya kuubatilisha mgomo huo, lakini ilidai kuwa mshtakiwa huyo hakufanya hivyo.
Wakili Kweka alilitaja kosa la pili kuwa ni kuwashawishi madaktari wagome kinyume na kifungu 390 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa Juni 27 mwaka huu, mshtakiwa huyo akiwa rais wa chama hicho aliwashawishi madaktari wasitekeleze amri hiyo ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ya Juni 22, mwaka huu, na matokeo yake madaktari hao wakagoma.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na Hakimu Kahamba alisema ili mshtakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wanaotambulika na serikali ambao watasaini bondi ya shilingi laki tano kila mmoja.
Hata hivyo Wakili wa serikali Kweka aliomba mahakama impatie dhamana mshtakiwa chini ya kifungu cha 148 (c)(6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambacho kinamtaka mshtakiwa ili apate dhamana ni lazima asalimishe hati ya kusafiria mahakamani na asitoke nje ya mkoa bila ruhusa ya mahakama.
Lakini Hakimu Kahamba alisema hicho kifungu kilishabatilishwa na Mahakama Kuu na kwamba yeye atatoa masharti ya dhamana kwa kutumia kifungu cha 148(c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kwani kifungu hicho kinaipa mamlaka ya kutoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa kadri inavyoona inafaa na baada ya kusema hayo aliahirisha kesi hiyo kwa dakika kumi na mshtakiwa huyo akapelekwa kuhifadhiwa katika mahabusu ya mahakamani hapo.
Ilipofika saa 6:50 mchana mshtakiwa huyo aliletwa ndani ya chumba cha mahakama na hakimu Kahamba akasema maneno yafuatayo: “Hatuko hapa kwa ajili ya kukomoana, tuko hapa kwa ajili ya kutenda haki hivyo nampatia mshtakiwa dhamana kwa kutumia kifungu cha 148(c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, na ambaye anaona hajaridhika na uamuzi wake aende mahakama ya juu akakate rufaa,” alisema Hakimu Kahamba.
Mshtakiwa huyo alitimiza masharti hayo ya dhamana na Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6 mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Jana eneo la mahakama hiyo lilifurika madaktari wenzake na ndugu na jamaa wa Dk. Mkopi waliofika kumuona mshtakiwa huyo ambaye aliletwa na askari polisi chini ya ulinzi mkali.
Takriban wiki mbili zilizopita madaktari walitangaza kuanza mgomo kwa madai kuwa wanafanyakazi katika mazingira magumu na kwamba wanaomba masulufi yao yaongezwe.
Wakati huohuo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa taarifa kwa madaktari walio kwenye mafunzo kwa vitendo (interns) imesema imepokea malalamiko kuwa kati ya Juni 23-29, 2012 madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo 372 kati ya 763 katika hospitali mbalimbali nchini, waligoma kutoa huduma kwa wagonjwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari ambayo imesainiwana Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Regina Kikuli, madaktari hao waliogoma walirejeshwa wizarani kwa barua kutoka kwenye mamlaka za hospitali walikokuwa wakifanyia mafunzo kwa vitendo.
Alisema kwa kuwa wizara ndiyo yenye dhamana ya usimamizi wa huduma za afya nchini, na kwa kuwa madaktari hao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika, hivyo wizara imewasilisha malalamiko haya huko ili baraza liwachunguze na kuamua hatma yao kitaaluma.
Pamoja na hilo wizara imetangaza kusitisha posho zao kuanzia Julai 1, mwaka huu, hadi hapo itakapopata taarifa ya uchunguzi wa Baraza la Madaktari.
“Madaktari wengine waliogoma, taratibu za kiutumishi zitachukuliwa na mamlaka ya ajira zao kwa mujibu wa sheria na taratibu husika,” alisema Kikuli.
Chanzo: Tanzania Daima, 11 Julai, 2012
0 maoni:
Post a Comment