na Grace Macha, Arusha
MFANYABIASHARA wa jijini Arusha, Joseph Ngisha (24), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuoa mtoto wa kike (jina limehifadhiwa) akiwa na umri wa miaka minane mwaka 2010 baada ya kumlipia mahari ya ng’ombe wanne kwa wazazi wake.
Aidha baba wa mtoto huyo ambaye kwa sasa ana ujauzito wa miezi mitatu, Lemomomo Olokuto (42) mkazi wa Mto wa Mbu wilayani Monduli, naye anashikiliwa kwa tuhuma za kumuoza mtoto huyo kinyume cha sheria na haki za malezi ya watoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa walimkamata Ngisha, Julai 18 mwaka huu, saa 3:45 akiwa nyumbani kwake pamoja na mtoto huyo maeneo ya Sakina, Songambele.
Alisema kuwa Ngisha alipohojiwa na polisi alikiri kumuoa binti huyo kwa kutoa mahari ya ng’ombe wanne huku akikanusha taarifa zilizotolewa na baba wa mtoto huyo, Olokuto aliyedai kuwa alimuoza mtoto huyo kwa mahari ya ngombe watatu.
Alisema Ngisha alitiwa mbaroni Julai 18 mwaka huu, saa 3.45 asubuhi nyumbani kwake baada polisi kupata taarifa za siri na kumkuta akiishi na mtoto huyo huku akiwa amembebesha ujauzito wenye miezi mitatu.
“Ngisha alianza kumchumbia mtoto huyo baada ya kuacha kunyonya kwa mama yake, alipofikisha umri wa miaka minane aliwafuata wazazi wake na kuwaeleza nia ya kutaka kumuoa,” alisema Sabas.
Hata hivyo mama wa mtoto huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, inadaiwa kuwa hakukubaliana na mpango huo ambapo Ngisha alimdanganya kuwa anakwenda kumpeleka shule.
“Taarifa za Ngisha kuishi na mtoto huyo kama mke ziligunduliwa na majirani kwani mara nyingi alikuwa akimfungia ndani bila mtu kujua huku akiwaeleza baadhi ya jamaa zake kuwa ni mdogo wake,” alisema.
Kwa sasa mtoto huyo yuko chini ya uangalizi wa ofisi ya ustawi wa jamii jijini Arusha, akiendelea na uchunguzi wa afya kuangalia endapo amepata madhara yoyote kiafya zaidi ya hiyo mimba aliyo nayo kwa sasa.
Kamanda Sabas alisema kuwa polisi wanaendelea na upelelezi juu ya tukio hilo ambapo ukikamilika watuhumiwa hao ambao kwa sasa wanashikiliwa na jeshi hilo watafikishwa mahakamani
Source: Tanzania Daima
0 maoni:
Post a Comment