na Betty Kangonga na Abdallah Khamis
MKUU wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Kawe (OC CID), David Mapunda, ametoa siri ya kutekwa, kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
OC CID huyo ambaye kwa sasa amelazwa katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) alilazimika kutoboa siri ya kipigo cha Dk. Ulimboka ili aweze kupata matibabu ya majeraha ya ajali ya kugongwa na gari aliyoipata juzi.
Dk. Ulimboka alipookotwa na wasamaria wema katika msitu wa Pande na kufikishwa katika kituo cha polisi Bunju, kilicho chini ya kituo cha Kawe, OC CID huyo anadaiwa kutoa amri ya Dk. Ulimboka kukaa zaidi ya saa tatu ili asipate matibabu ya haraka.
Vyanzo vyetu vya habari vililiambia gazeti hili kuwa mara baada ya kugongwa na gari juzi, kigogo huyo wa polisi alijitahidi sana kukwepa kwenda Muhimbili lakini alijikuta akiishia mikononi mwa madaktari wa taasisi hiyo ya mifupa ya Moi, hivyo aliingiwa hofu ya kutotendewa haki ya matibabu.
Kabla ya kufikishwa Muhimbili, askari huyo alikwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Lugalo na Aghakan, lakini alijikuta anatakiwa kufika Kitengo cha Mifupa cha Moi, Muhimbili, ambako hadi sasa bado anaendelea na matibabu.
Kwa mujibu wa habari hizo kutokana na hofu ya kususiwa na madaktari, polisi huyo alilazimika kuwapigia magoti na kueleza mengi kuhusu kipigo cha Dk. Ulimboka na kwamba yeye hahusiki na sakata hilo.
Mtoa habari wetu alisema kuwa OC CID huyo mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo akiwa na maumivu makali, alisema hahusiki na kipigo cha Dk. Ulimboka na hata siku ya tukio hakuwepo.
Katika hali isiyo ya kawaida, kigogo huyo alijitetea huku akiwa na maumivu makali ya majereha aliyopata.
“Mimi sijahusika kabisa na kutekwa kwa Ulimboka. Jamani msinidhuru. Tena siku hiyo mimi sikuwepo,’ alikaririwa OC CID akisema.
Habari zaidi zinasema kuwa askari huyo aliendelea kueleza mengi na hata alipotakiwa kuchomwa sindano, alionyesha woga na kuuliza anachomwa sindano gani.
Ili kuhakikisha anatibiwa vizuri, kumekuwa na doria za kila mara ndani na sehemu mbali mbali za wodi za MOI hali iliyowafanya madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kulalamikia hali hiyo.
Mbali ya OC CID huyo kuingiwa na hofu ya kulipiziwa kisasi, hofu hiyo pia imewakumba ndugu zake kwani hawana amani na matibabu ya ndugu yao.
Tanzania Daima Jumatano ilipofika katika hospitali Muhimbili, ilishuhudia kuwapo kwa askari polisi wakilinda doria, huku OC CID akiwa amelazwa chumba cha peke yake akiendelea kutibiwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa madaktari wa Muhimbili ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema Mapunda alifikishwa hospitalini hapo juzi akiwa katika hali mbaya na mara baada ya kufikishwa aliomba msamaha kwamba hakuhusika kumteka Dk. Ulimboka.
“Ni kweli jamaa alipokelewa lakini tulishangaa kwani alikuwa akiongea kwa kuweweseka kwamba hajahusika na tukio la kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka na akawa anaomba tusimdhuru,” alisema daktari huyo.
Kwa mujibu wa daktari huyo, kilichowashangaza zaidi ni ulinzi mkali wa polisi aliowekewa mgonjwa huyo huku kukiwa na watu wanaofuatilia kila anayeingia katika wodi namba D aliyolazwa.
Afisa Uhusiano wa Moi, Jumaa Almasi, alisema mgonjwa huyo alifikishwa hospitalini hapo wiki iliyopita akiwa amepata majeraha mwilini baada ya kugongwa na gari.
Kuhusu mgonjwa huyo kumtaja Dk. Ulimboka, Almasi, alisema hawezi kuzungumzia tukio hilo kwani hakuwepo wakati akifikishwa hospitalini hapo.
Kwa Upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kupata ajali kwa OC-CID Mapunda na kuongeza kuwa ajali hiyo aliipata wakati akitekeleza majukumu yake.
Alisema hakuna uhusiano wowote wa tukio la kutekwa Ulimboka na ajali hiyo.
Tangu tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka serikali kupitia maafisa wake wa usalama wamekuwa wakihusishwa kwa namna moja au nyingine.
Kuhusishwa huko kwa serikali hususan jeshi la polisi kunafuatia matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na afisa upelelezi kutoka kituo cha Selanda Bridge katika eneo la Muhimbili, matamshi ya kutatanisha ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova pamoja na kukamatwa kwa mtu aliyedaiwa kuungama kanisani kuwa ndiye aliyemteka na kumtesa Dk. Ulimboka
Source: Tanzania Daima 25th July 2012
0 maoni:
Post a Comment