Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MADAKTARI WAZIDI KUFUKUZWA, KCMC YAWATIMUA 80, WENYEWE WAONYA

WIMBI la kuwafukuza kazi madaktari wanaoendelea na mgomo limezidi kushika kasi baada ya madaktari wapatao 80 kutoka Hospitali ya KCMC, mkoani Kilimanjaro, kuamriwa kuondoka katika eneo la hospitali hiyo.

Katika tangazo lililowekwa katika mbao za matangazo ya hospitali hiyo madaktari hao walitakiwa hadi jana saa nane mchana wawe wameondoka katika maeneo hayo wakiwa wamekabidhi kila kitu kinachohusiana na hospitali hiyo, huku wakitakiwa wakaripoti kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.

Pamoja na kuwataka waondoke, tangazo hilo lisilokuwa na jina au saini ya mtu yeyote zaidi ya kuandikwa kuwa ni maagizo ya utawala liliwataka madaktari hao wasikusanyike au kufanya mkutano wa aina yoyote katika maeneo ya KCMC.

Juzi hospitali za mikoa ya Mbeya, Dodoma na Mwanza ziliwafukuza kazi madaktari hao ambao mpaka jana idadi yao ilizidi 200.

Hata hivyo madaktari wa KCMC walisema hawatarudi nyuma katika kutetea maslahi ya kupatiwa mazingira bora ya kufanyia kazi na kwamba serikali inapaswa kutambua njia sahihi ya kumaliza mgogoro huo siyo kuwafukuza madaktari bali waboreshe mazingira ya kuwahudumia wagonjwa.

CHADEMA yalia na Spika

Wakati Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, akisafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemwandikia barua, Spika wa Bunge, Anna Makinda, kutaka Bunge kujadili sakata hilo.

Mkurugenzi wa Habari na Unezi wa CHADEMA, John Mnyika. ameandika barua hiyo baada ya juzi Spika Makinda kuwazuia wabunge kujadili suala la mgomo wa madaktari kwa madai kuwa suala hilo lipo mahakamani.

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mwenezi wa chama hicho, John Mnyika, na gazeti hili kupata nakala yake, CHADEMA inamtaka Makinda kutumia madaraka yake kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) kuisimamia serikali kuokoa uhai wa wananchi wagonjwa na kuishauri serikali kushughulikia chanzo cha mgomo.

“Izingatiwe kwamba serikali imefungua kesi dhidi ya Chama cha Madaktari (MAT) na haijafungua kesi dhidi ya Jumuiya ya Madaktari na Taasisi zingine katika sekta ya afya; hivyo kufunguliwa kwa kesi hiyo hakuwezi kulizuia Bunge kujadili masuala mengine yanayohusu madaktari na sekta ya afya nchini.”

Katika barua hiyo, Mnyika amemtaka Spika Makinda kutumia mamlaka yake kwa kurejea Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la 2007) Kanuni 5 (1), 37 (7), 53 (1), 114 (3), 114 (17) na 116 kuruhusu Bunge kujadili hoja ya madai ya madaktari ili kuisimamia serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupitisha maazimio ya kuwezesha suluhu ya mgogoro unaoendelea.

Mbunge huyo alisema kuwa aliwahi kumwandikia barua Spika Makinda juu ya hoja hiyo, badala yake Juni 27, 28 na 29 mwaka huu kwa nyakati tofauti, kumetolewa miongozo na majibu ya Spika Makinda, Naibu wake Job Ndugai na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba suala la madai ya madaktari haliwezi kujadiliwa bungeni kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kuingilia kesi iliyopo mahakamani.

Alisema ukiondoa suala la madai ya madaktari ambayo ni kati ya hoja zilizopo mahakamani masuala mengine yanayoendelea si sehemu ya madai yaliyopo mahakamani.

Aliyataja mambo ambayo hayahusiki na kesi iliyopo mahakamani kuwa ni pamoja hali ya hivi sasa ya kudorora kwa huduma katika hospitali za umma na jaribio la mauji ya Dk. Ulimboka.

Alirejea kauli ya Waziri Mkuu bungeni kuwa serikali imejipanga kuziba pengo kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea kwa kupeleka madaktari kwenye hospitali za rufaa kutoka wizarani, kurejesha madaktari wastaafu, kupeleka wagonjwa wa rufaa katika hospitali za jeshi na kupunguza idadi ya wagonjwa wa rufaa kutoka hospitali za wilaya na mikoa.

“Nikiwa mbunge wa Dar es Salaam kwa mkoa wetu pekee hatua hizi hazijaweza kuziba pengo na kwa sasa maisha ya wagonjwa yako mashakani hali ambayo inahitaji chombo chenye madaraka ya kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kuingilia kati,” alisema.

Aidha alisema serikali imetangaza kwenye vyombo vya habari kuwa imeweka mpango wa kuwahamishia wagonjwa katika hospitali binafsi suala ambalo linazua maswali mengi.

“Kama serikali ina uwezo wa kugharamia matibabu katika hospitali binafsi ni kwa nini isitumie fedha hizo kuboresha huduma katika hospitali za umma ikiwemo maslahi ya madaktari, madawa na vifaa tiba masuala ambayo ni chanzo cha mgogoro. Pia, kutumia fedha za umma zilizopitishwa na Bunge kwa ajili ya hospitali za umma kuingiza madaktari toka nje au kulipia hospitali binafsi ni masuala ambayo yanahitaji usimamizi wa kibunge,” alisema.

Kwa mujibu wa Mnyika, wagonjwa wenye hali tete wamehamishiwa katika hospitali za rufaa wengine kutoka hospitali binafsi na wengine kutoka katika hospitali za chini kwa ajili ya kupata huduma toka kwa madaktari bingwa na kwa kutumia vifaa tiba vya hali ya juu zaidi.

Kuhusu jaribio la mauaji ya Ulimboka, Mnyika alisema kuna utata mkubwa kuhusu jaribio hilo.

Alisema uchunguzi unaofanywa na askari polisi pekee hauwezi kuaminika na hivyo Bunge linapaswa kuisimamia serikali kuwezesha uchunguzi huru.

Alimtaka Spika Makinda kutoa idhini kwa mujibu wa kanuni ya 150 (1) ya kutolewa kwa hoja ya kutengua kanuni husika ya 64 (1) (c) kuliwezesha Bunge kujadili Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii.

Pili alimtaka Spika mosi kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni 114 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kutaka kamati husika ya Bunge kukutana kwa dharura na kuishauri wa haraka serikali kufuta kesi iliyoko mahakama kuu kitengo cha kazi au kutafuta suluhu ya nje ya mahakama ili kulipa fursa Bunge kutumia madaraka yake ya kikatiba kujadili na kupitisha maazimio ya kuweza kusuluhisha pande mbili za mgogoro badala ya mahakama ambayo mchakato wake utachukua muda mrefu kukamilika huku wananchi wakiendelea kuathirika.

Tatu; alisema Spika anaweza kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni ya 114 (17) na 116 kuitaka Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kupatiwa na kupitia nyaraka zilizowasilishwa mahakamani, na kuandaa taarifa maalum ya masuala yanayoweza kujadiliwa bungeni bila kuingilia suala lililo mahakamani.

“Nne; Kanuni ya 53 (2) au 47 (1) za Kanuni za Kudumu za Bunge inaweza kutumiwa kwa Waziri husika kwamba suala la namna ambavyo serikali imejipanga kutoa huduma katika hospitali kufuatia mgomo wa madaktari unaoendelea au mbunge yeyote kutoa hoja kuhusu hali kwa sasa ilivyo katika hospitali na sekta ya afya kwa ujumla kufuatia kuendelea kwa mgogoro kati ya serikali na madaktari na masuala hayo yakajadiliwa.

“Izingatiwe kuwa masuala hayo hayahusu mgogoro ulioko mahakamani bali ni ya dharura kwa ajili ya kuepusha madhara zaidi kwa wananchi na nchi kwa ujumla wakati taifa likisubiri taratibu za mahakama kukamilika.

Habari hii imeandaliwa na Martin Marela (Dodoma) na Charles Ndagula (Moshi)

Source: Tanzania Daima, 01 July 2012
Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO