Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

SIKIKA WAPINGA SERIKALI KUWANYANG’ANYA LESENI MADAKTARI

na Asha Bani na Irene Mark

WAKATI Shirika lisilo la kiserikali la SIKIKA, likidai kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya Baraza la Madaktari Tanganyika kuwafutia leseni za kutibu madaktari wanafunzi (interns) 319 juzi na kutaka warejeshwe mara moja, Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania (BAHAKITA), linakusudia kuwashitaki mahakamani madaktari waliogoma.

Mkurugenzi wa SIKIKA, Irenei Kiria, alisema kuwa wanamtaka, Dk. Donan Mmbando, ambaye anaongoza baraza hilo kwa niaba ya serikali, kuwarejeshea leseni zao interns haraka iwezekanavyo na kuwarudisha kwenye vituo vyao vya kazi.

Alisema kuwa namna serikali inavyoshughulikia mgogoro wa madaktari, inaonesha wazi kuwa haina uwezo wa kutatua migogoro ya wafanyakazi wake badala yake inatumia hujuma, vitisho na ubabe.

“Mgomo huu unaoendelea wa madaktari nchini ni wa kipekee kwa sababu haujaitishwa na Chama cha Madaktari (MAT) na kwamba unapigania kuboresha huduma za afya kwa wananchi,” alisema Kiria.

Alisema tangu mgomo huo uanze, serikali haijawahi kuwa na nia ya dhati kushughulikia madai ya madaktari zaidi ya kuahirisha mazungumzo, kudanganya umma kuhusu hatua za makubaliano kwamba imetatua matatizo ya huduma za afya.

Kiria aliongeza kuwa pengo la madaktari nchini ni kubwa kufikia takriban asilimia 60, hivyo si busara kuwanyanyasa wale wachache waliokubali kufanya kazi katika mazingira hatarishi kiafya na vitendeakazi duni au haba.

Kwamba kwa mujibu wa tafiti za SIKIKA, hospitali nyingi nchini hazina mashine za kuchunguza maradhi na zilizopo ni mbovu kwa muda mrefu bila jitihada za kutengeneza, mfano X-ray na CT-Scan.

“Mwenyekiti wa Baraza la Madaktari ndiye Mganga Mkuu wa wizara, mwajiri. Hatuna taarifa kama uchunguzi wa kutosha ulifanyika kwa kila intern ushiriki wake katika mgomo kabla ya kufutiwa leseni.

Hivyo, tunahitaji madaktari zaidi kuhudumia wananchi, uamuzi wa kuwafukuza ni kutowajali wananchi, hasa wakati huu ambao viongozi wengi wa serikali hutibiwa nje ya nchi,” alisema.

Hata hivyo, BAHAKITA kwa upande wao wameweka msimamo wa kwenda mahakamani kuwshitaki madaktari waliogoma iwapo litabaini kuwapo kwa vifo vya watu vilivyotokana na mgomo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Baraza hilo, Said Mwaipopo, alisema wamekusudia kufanya hivyo baada ya kuona kwamba madaktari hawataki suluhu wala kusikiliza ushauri wao.

Mwishoni mwa juma lililopita, Mwaipopo akiwa na baadhi ya viongozi wa madaktari walioko kwenye mgomo, alinukunuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akimwomba Rais Jakaya Kikwete akutane nao ili kuzungumzia suala la madaktari ombi lililokataliwa na Ikulu kwa maelezo kwamba hakuna mgomo tena.

Hata hivyo baada ya Ikulu kukataa ombi lao Mwaipopo alizungumza na Tanzania Daima akisema amewashauri viongozi wa madaktari kuandika barua ya kuomba msamaha kwa wananchi, serikali na Rais Kikwete kisha kuweka bayana suala hilo kwenye vyombo vya habari.

Katika majibu yake kuhusu suala hilo, Dk. Edwin Chitage, ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, alikiri kukutana na Mwaipopo akiwa na viongozi wengine na kusema haoni sababu ya kuomba radhi kwa vile kudai masilahi na mazingira bora ya kazi si kosa.

“Wapo wanaosema mgogoro umeisha lakini ukweli si huo, mgogoro bado upo na huu ulianza mwaka 2005 bila dhamira ya dhati ya kutafuta suluhu, utaendelea hata baada ya miaka 10, naomba jamii ielewe hatulazimishi kukutana na mtu muhimu hapa ni dhamira ya dhati kwanza,” alisema.

Lakini katika tamko lao, Mwaipopo aliweka bayana kwamba lengo la kuwaburuza mahakamani madaktari hao ni barua waliyoandika kwa Umoja wa Mataifa (UN) wakiomba ulinzi huku akisisitiza kwamba kitendo hicho ni kuudhalilisha utawala wa Rais Kikwete.

Kuhusu madaktari wanafunzi kunyang’anywa leseni zao, Dk. Chitage alisema hawashtushwi na jambo hilo kwa kuwa walilitegemea.

Afya ya Dk. Ulimboka

Akizungumzia hali ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, ambaye baada ya kutekwa, alipigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande nje ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Chitage alisema anaendelea vizuri.

Dk. Ulimboka aneendelea na matibabu nchini Afrika Kusini. Na Dk. Chitage alisema wanamshukuru Mungu kwamba mwenyekiti wao anaendelea vizuri kila siku afya yake inazidi kuimarika na hata anapozungumza naye kwenye simu anamsikia kwamba amepata nafuu sana

Source: Tanzania Daima, 12 July 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO