na Martin Malera, Dodoma
VIJEMBE, kashfa, kejeli na maneno ya kuudhi, jana vilitawala Bunge wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Hali hiyo ilianza juzi kutokana na ushabiki wa kisiasa kwa upande mmoja, na udhaifu wa Mwenyekiti wa Bunge, Steven Mabumba, kwa upande mwingine.
Mvutano na malumbano ya kisiasa vilimfanya Mbumba kuonyesha wazi upendeleo kwa wabunge wa CCM dhidi ya wale wa upinzani.
Mabumba alifikia hatua ya kutoa hata kauli chafu Bungeni dhidi ya Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, akisema mbunge huyo “anawashwawashwa” na kutaka kusimama mara kwa mara kuomba mwongozo.
Baadaye alimtoa nje Mbunge Kasulu Moses Machali (CCM) akidai kuingilia mjadala huo; mbunge huyo alikuwa na kiherehere cha kudandia mambo yasiyomhusu.
Malumbano hayo yaliyoanza tangu juzi na kuendelea hadi jana yalitokana na hoja ya mgomo wa madaktari na jaribio la kuuawa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, ambaye alitekwa nyara katika mazingira ambayo yanailazimisha serikali kuendelea kujitetea kwamba haikuhusika kumteka daktari huyo.
Aliyeanza kuchafua hali ya hewa juzi Bungeni ni Mbunge wa Viti Maalum na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, ambaye alitoa tuhuma dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akisema kinahusika na mgomo wa madaktari na kwamba waliomteka walivaa magwanda yanayoelekeana na nguo wanazovaa wafuasi na wanachama wa CHADEMA.
Hata hivyo, tayari Dk. Ulimboka mwenyewe alishamtambua na kumwambia waziwazi mmoja wa watu ambao aliwatuhumu kumfanyia unyama. Mtu huyo, ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa tume iliyoundwa na jeshi la polisi kuchunguza mkasa huo, ni kigogo katika jeshi la polisi katika idara ya upelelezi wa makosa ya jinai mkoani Dar es Salaam.
Wakati Manyanya akiendelea kuzungumza, Mbunge wa Ubungo (CHADEMA) John Mnyika alisimama kupinga kauli hiyo na kumtaka msemaji athibitishe au afute kauli yake.
Naye Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) Mwigulu Nchemba aliungana na Manyanya kwamba CHADEMA inahusika akitumia kauli kama za Manyanya.
Hoja hiyo ilimtibua Mnyika, akatumia kanuni mbalimbali kuwabana wasemaji (Manyanya na Mwigulu), na kuwataka wathibitishe au wafute kauli zao.
Hata hivyo kauli ya Manyanya imewasikitisha baadhi ya wabunge wa CCM kwa madai kuwa mkuu huyo wa mkoa wa Rukwa alipotoka.
Hali ilivyokuwa jana
Hali ya wabunge kulumbana kwa mambo yasiyo na tija hadi kutoleana lugha kali, iliendelea tena jana kiasi cha ukumbi wa Bunge kuonekana kama uwanja wa mipasho.
Baada ya maswali na majibu, Mnyika aliomba mwongozo wa Spika na kuhoji uhali wa Mwenyekiti wa Bunge, Mabumba, kutumia lugha ya kuudhi kwa wabunge hao.
Mwenyekiti wa Bunge Jenister Mhagama ambaye aliendesha vikao vya Bunge jana, alisema atatolea uamuzi baadaye au siku yoyote atakayoona inafaa.
Mjadala wa jana kuhusu hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, ulivurugika tena baada ya Mbunge Iramba Magharibi (CCM) Nchemba alipoamua kuishambulia CHADEMA.
Nchemba ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akiishambulia CHADEMA, alisoma hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani na kudai kuwa imejaa maneno ya uchochezi dhidi ya walimu.
“Mheshimiwa mwenyekiti, hotuba hii imejaa maneno ya uchochezi. Ukisoma ukurasa wa 36 kuna sehemu inasema walimu wote wa msingi wanafanya biashara shuleni na kuacha kufundisha, jambo ambalo sio kweli.
“Huu ni udhalilidha na upotoshaji mkubwa unaofanywa na CHADEMA kwa kusema walimu wote hawafundishi bali wanafanya biashara,” alisema Nchemba.
Kuona hivyo wabunge wa CHADEMA, walikuja juu, na Mnyika, Sabrina Sungura na Mchungaji Peter Msigwa kwa nyakati tofauti waliomba mwongozo kupinga kauli ya Nchemba kwa madai kuwa anapotosha umma kwa kusoma mstari mmoja badala ya sentensi nzima.
Sabrina alisema katika mwongozo wake kuwa ana ushahidi kuwa walimu wengi, hasa wa shule ya msingi, wanafanya biashara shuleni kutokana na maslahi madogo.
Hata hivyo Mwenyekiti Bunge alipotoa ufafanuzi alimruhusu Nchemba kuendelea kutoa hoja yake, lakini wakati akiendelea alimshambulia Sabrina kwa kumwambia arudi tena darasani kwani hajui kitu, kwani wanapingana na hoja waliyoiandika wenyewe.
Safari hii Mnyika alisimama tena kuomba mwongozo wa kutaka afute kauli yake ya kuudhi kwamba Mbunge wa CHADEMA (Sabrina), arudi tena darasani.
Hata hivyo, Nchemba alifuta kauli hiyo lakini wakati akiendelea na hoja yake alizidi kuishambulia CHADEMA na kumfanya Mnyika asimame tena kuomba mwongozo.
Alipopata nafasi, Mnyika alitoa tuhuma nzito kwa Mwigulu kwamba ni mmoja kati ya mafisadi waliokwapua fedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Wakati akiendelea kushusha tuhuma hizo, Jenister Mhagama, alimtaka Mnyika kuthibitisha tuhuma hizo ndani ya siku saba kwamba Mwigulu ni mmoja kati ya watuhumiwa ufisadi wa mabilioni ya fedha za EPA ingawa Mnyika hakusema Mwigulu alikwapua fedha za EPA.
Baada ya timbwili hilo lililodumu kwa takriban dakika 45, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachaweni, alitumia dakika tano kueleza masikitiko yake kuhusu kile kinachoendelea Bungeni.
Simbachawene ambaye amepata kuwa mwenyekiti wa Bunge alisema kuna uvunjifu mkubwa wa kanuni ikiwa ni pamoja na wabunge kuzungumza bila kuzingatia kanun
Source: Tanzania Daima, 04 July 2012
0 maoni:
Post a Comment