Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA TISHIO; MAKADA WAKE WASHTAKIWA KWA UGAIDI AKIWEMO KATIBU WA CHADEMA MKOA WA DAR ES SALAAM, HENRY KILEWO

KASI ya kuimarika na kushamiri kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kila kukicha kunakotokana na kukubalika kwake kwa wananchi, kumekuwa tishio kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hali ya mambo inaonesha kuwa, kitisho hicho ndicho kinainyima usingizi CCM na serikali yake, hivyo kupanga na kuibua vituko dhidi ya CHADEMA ili kukidhoofisha na kukipaka matope mbele ya wananchi.

Vituko na mikakati hiyo imezidi kushika kasi ambapo safari hii, makada watano wa chama hicho wameshtakiwa kwa kosa la ugaidi, ukiwa ni mwendelezo na sehemu ya mkakati huo kwa kutumia njia mbalimbali.

Kosa kama hilo pia alishtakiwa nalo Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, hivi karibuni, lakini Mahakama Kuu ilimfutia shtaka hilo.

Wakati makada hao wameshtakiwa kwa ugaidi, kosa ambalo halina dhamana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Tundu Lissu na Godbless Lema wamezuiwa kuingia bungeni.

Hata hivyo, matokeo ya kiwewe cha CCM dhidi ya CHADEMA, yamewahi kukipata Chama cha Wananchi CUF kuelekea uchaguzi wa mwaka 2005, baada ya kuonekana ni tishio dhidi ya CCM.

Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Omari Mahita, aliibua tuhuma nzito dhidi ya CUF kuwa waliingiza nchini shehena ya majambia, hivyo ni chama hatari, doa ambalo kwa kiasi kikubwa lilikiathiri chama hicho.

Safari hii, hila hizo zinaelekezwa kwa CHADEMA kinachoonekana ni tishio kwa utawala wa CCM na serikali yake ambapo jana makada wake wameshtakiwa kwa ugaidi.


Walioshtakiwa kwa ugaidi

IMG-20130625-WA0003Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo (pichani), Evodius Justinian wa Buboka, Oscar Kaijage wa Shinyanga, Seif Magesa Kabuta wa Mwanza, Rajab Daniel Kihawa wa Dodoma, jana wameshtakiwa kwa ugaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora mjini.

Watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi kwa kumteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.

Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka mawili wote, la kwanza ni la kufanya ugaidi, na la pili ni kummwagia tindikali Tesha.

Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, ya Tabora mjini, Joktani Rushwera, huku upande wa serikali ukiwakilishwa na Wakili Juma Massanja na Ildefons Mukandara.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Profesa Abdalah Safari, ukiwajumlisha Peter Kibatala na Gasper Mwalyela, uliiomba mahakama hiyo iyafute mashtaka hayo kwa sababu ya kutokuwa na uhai.

Mawakili wa utetezi walidai kuwa mashtaka hayo hayana uhai kwa sababu yamefunguliwa bila ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Ulidai sheria za uendeshaji wa makosa kama hayo hapa nchini zinadai kuwa mashitaka kama hayo yanapofunguliwa ni lazima ridhaa ya DPP iwepo lakini ridhaa hiyo haipo hivyo yatupwe.

Ulitoa sababu ya pili kuwa maelezo hayaoneshi kosa husika ni la kigaidi, tofauti na makosa mengine ya kawaida kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hivyo waliomba yafutwe au yafunguliwe kama kosa la kawaida.

Upande huo wa utetezi ulidai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, inaelekeza kuwa mshitakiwa ashitakiwe katika mahakama yenye mamlaka na hadhi kama ile waliyopelekwa katika maeneo yale walikokamatwa.

Ulidai mawakili waliiomba mahakama itupilie mbali shitaka, kwani washitakiwa kama walikuwa na hatia walipaswa kushitakiwa katika maeneo yao walipokamatwa.

Baada ya hoja hizo, mahakama iliahirisha kesi hiyo na itatajwa tena Julai 8, mwaka huu Tabora mjini.

Hii si mara ya kwanza kwa viongozi au wafuasi wa CHADEMA kufunguliwa kesi zinazohusiana na ugaidi, Machi 18, 2013, Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka manne, yakiwamo ya ugaidi.

Kosa jingine lililowakabili Lwakatare na Ludovick ni kula njama; kosa ambalo pia linawakabili washtakiwa wote, ambalo ni kinyume cha kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na. 21 ya mwaka 2002.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka Denis Msaki, kinyume cha kifungu cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

Katika kosa la tatu, washtakiwa wote wawili wanadaiwa kufanya mkutano wa kupanga kufanya makosa ya ugaidi  kinyume cha kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi.

Wakili wa serikali alidai kuwa washitakiwa wote Desemba 28, mwaka jana walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyara Msaki kinyume cha kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi.

Pamoja na tuhuma hizo, Mei 8, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimfutia mashitaka matatu ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Lwakatare.

Jaji Lawrance Kaduri akitoa uamuzi huo alisema ulitokana na kukubaliana na hoja ya mawakili wa Lwakatare; Tundu Lissu, Peter Kibatara na Mabere Marando na kusema kuwa:

“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama inatoa amri ya kumfutia Lwakatare mashitaka matatu, yaani kosa la pili, tatu na la nne kwa sababu Jamhuri imeshindwa kuonesha maelezo yanayotesheleza kumshitaki Lwakatare kwa kesi ya ugaidi.

“Naamuru jalada la kesi ya msingi lirudishwe Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya mshitakiwa kuendelea kushitakiwa kwa kosa moja la kula njama, ambalo linaangukia katika sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002,” alisema Jaji Kaduri.


KILEO CHADEMA 3

Mbowe, Lissu, wazuiwa kuingia Bungeni

Licha ya kanuni za Bunge kuruhusu vazi la safari suti yenye mshono kama kombati zinazovaliwa na baadhi ya wabunge wa CHADEMA, kwa mara ya kwanza Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe na wenzake watatu jana walizuiwa kuingia bungeni.

Mbowe na Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) walizuiwa na askari kwa madai kuwa wamevalia sera za chama.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni katika viwanja vya Bunge, Lissu alisema walishangazwa na uamuzi huo wakati mavazi hayo wamekuwa wakiyavaa na kuingia nayo bungeni kwa miaka mingi sasa.

Lissu alisema kuzuiwa kwao wanakuchukulia kuwa ni mkakati maalumu wa serikali ya CCM kutaka kuwazima na kuhakikisha hawapati nafasi ya kuingia bungeni ili wasijibu mashambulizi ya tuhuma wazosingiziwa kuhusiana na mlipuko wa bomu jijini Arusha.

“Sisi hali hiyo tulianza kuishtukia tangu asubuhi tulipoingia kwenye eneo la Bunge, kama mligundua kulikuwa na askari wengi sana kila kona kuliko kawaida kana kwamba nchi imepinduliwa. Kinyume cha utaratibu na kanuni, askari wa kawaida wameingiza hadi bungeni.

“Tulipofika wakati wa kuingia ukumbini mimi, Mbowe, Lema na Wenje tuliambiwa haturuhusiwi kwa kuwa tumevaa sare za chama. Tulipouliza nani kawapa maagizo hayo walidai ni uongozi wa juu, yaani Spika wa Bunge,” alisema Lissu.

Aliongeza kuwa kitendo hicho ni kichekesho kwani wakati wote tangu mwaka 2010 Mbowe amekuwa akivalia vazi hilo, achalia mbali wabunge wenzake baadhi ambao mara moja moja nao walikuwa wakivaa suti hizo lakini hawajawahi kuzuiwa.

Hata hivyo, pamoja na uamuzi huo, kanuni za Bunge hakuna mahali zinazuia mbunge kuvaa sare ya chama chake isipokuwa kanuni limeainisha aina za mavazi ya kuvaliwa na wabunge wanawake na wanaume.

Kwa mujibu wa kanuni ya 149 (3)(a) Kwa wanawake na (b) Kwa wanaume inasema: (a) Kwa wanawake;- (i) Vazi lolote la heshima yaani ambalo si la kubana mwili, lisiloonesha maungo ambayo kwa mila na desturi za Kitanzania hayapaswi kuoneshwa na ni refu kuvuka magoti.

(ii) Gauni la kitenge au blauzi inayovaliwa na kitenge au sketi ya rangi yoyote (iii) Kilemba cha kadiri au mtandio (iv) Suti ya kike; au (v) Vazi linalovaliwa wakati wa eda.

(b) Kwa wabunge wanaume;-(i) Suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia; (ii) Vazi la kimwambao yaani ka nzu rasmi na nadhifu, koti, baraghashia na makubadhi au viatu; (iii) Suti kamili ya Kimagharibi ya rangi kadiri isiyomeremeta; (iv) Koti aina ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au (v) Tarbushi na kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti ya imani au mila.


Wasusia kupitisha bajeti

Akizungumzia kuhusu uamuzi wa wabunge wao kutoingia bungeni kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/14, Lissu alisema baada ya kukutana na kujadiliana kwa kirefu hawakuona sababu ya kuingia.

“Tukio la bomu kwa wafuasi wetu jijini Arusha halikuwa la bahati mbaya lakini tumejiuliza ni kwanini Bunge halikuahirishwa walau kwa siku moja kama ilivyo utamaduni ili kushiriki kuomboleza msiba huo,” alisema.

Alisema kuwa pamoja na kwamba kiongozi wao wa kambi, Mbowe na Lema ndio walikuwa wamelengwa kulipuliwa lakini wakarusurika, Spika wa Bunge na Waziri Mkuu hakuna hata mmoja aliyetuma salamu za pole kwa viongozi hao.

“Waliolengwa kulipuliwa ni Mbowe, Lema na James ole Millya, lakini hata risasi zilizowaua wale wafuasi wetu wanne zilikuwa zikielekezwa kwa viongozi wetu.

“Sasa tunajiuliza, Bunge limeona waliokufa Arusha ni Watanzania lakini kwa vile walikuwa kwenye mkutano wa CHADEMA haiwahusu, hivyo kama wanajifanya kama hakuna kilichotokea sisi tunaingia ndani kufanya nini?” alihoji.

Lissu alitaja sababu nyigine kuona siku zote kila unapotokea msiba mkubwa wa wananchi wakati Bunge likiendelea, wamekuwa wakitumwa wawakilishi lakini kwa tukio la Soweto, Arusha Bunge halikutuma mwakilishi.

Alifafanua kuwa sababu kubwa iliyowafanya wafikie uamuzi huo ni kutokana na hatua ya Spika wa Bunge kupindisha ratiba ya Bunge ili kuwanyima nafasi wasijadili bajeti hiyo, hivyo kuhoji wanakwenda kupitisha kitu gani ambacho hawakushiriki.

“Hatukuweza kuwasilisha maoni ya kambi kutokana na tukio la Arusha lakini kulingana na ratiba tulimaliza mazishi Ijumaa tukijua kabisa Jumatatu tungepewa muda wetu wa nusu saa kuwasilisha maoni ya kambi.

“Si hivyo tu, bali hata wale walioomba kuchangia wangepata nafasi ya kuchangia halafu Jumanne bajeti hiyo ingepitishwa kwa mujibu wa ratiba. Lakini kutokana na hofu kuwa tungejibu mapigo kuhusu madai ya Arusha waliamua kufanya mbinu za kutunyima nafasi,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO