Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CUF wakiri uliberali, wakana ushoga; Wamalizana na CHADEMA bungeni

Mbunge wa Nyamagana(Chadema), ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Ezekia Wenje, akitolewa nje ya Ukumbi wa Bunge na askari wa Bunge huku akionyesha alama ya ‘V’, baada ya wabunge wa CUF kutaka kumpiga, kutokana na hotuba yake waliyodai kuwaudhi wabunge hao. Picha na Emmanuel Herman.


na Edson Kamukara, Dodoma

SIKU moja baada ya vyama vya CUF na CHADEMA kuvurugana bungeni na kusababisha Bunge kuahirishwa mara mbili, hatimaye muafaka umefikiwa kwa viongozi wake kuombana radhi hadharani.

Vyama hivyo viliingia kwenye mtafaruku mkubwa juzi baada ya wabunge wa CUF kuomba mwongozo wakita msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekiah Wenje, aondoe maneno ya kukidhalilisha chama chao kwenye hotuba yake.

Maneno yaliyoleta mtafaruku yalikuwa ukurasa wa nane ambapo katika hotuba hiyo, Wenje alikuwa akielezea itikadi za vyama rafiki vya nje vinavyoshirikiana kuviwezesha na vyama vya CCM, CUF na CHADEMA.

Wenje alisema kwa upande wa CUF, kutokana na itikadi yake ya mrengo wa Kiliberali ambayo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na “kupigania haki ya ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga”.

Kutokana na vurugu hizo baada ya Wenje kukataa kuomba radhi akisema haoni kosa lake na hivyo kukubali kuondoa maneno, Naibu Spika, Job Ndugai, aliliahirisha Bunge mara mbili na kuiagiza Kamati ya Haki, Kinga, Madaraka na Maadili ilijadili suala hilo na kushauri.

Hatimaye jana baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Ndugai alimpa nafasi Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, John Chiligati, ili aeleze kile kilichojadiliwa na kuafikiwa.

Chiligati alisema kuwa walikutana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kama walalamikiwa na upande wa CUF kama walamikaji, alikuwepo mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim.

Alisema kuwa katika utetezi wake, Mbowe alisema kuwa wako tayari kuondoa maneno hayo lakini hawawezi kuomba radhi kwa vile kilichosemwa ni sahihi.

Katika hoja yake ya pili Mbowe alisema kuwa CUF walimtukana Wenje na kumdhalilisha, kuchana hotuba na vurugu zao ziliahirisha Bunge, hivyo akataka mambo hayo yazingatiwe katika mjadala.

“Mbarouk yeye alikiri kuwa CUF ni wanachama wa ‘Liberal International’ lakini hawakubaliani na sera zote za umoja huo. Na isitoshe Tanzania kama nchi ilishatoa msimamo wakati Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alipotoa masharti ya misaada kwa mataifa yanayoendelea kwa kutaka wakubali ushoga.

“Hivyo kama nchi tumekataa! Masoud alihoji kwa nini CHADEMA waliweka maneno hayo kwenye hotuba ili kuwadhalilisha? Anataka waombwe radhi na kuondoa maneno hayo,” alisema.

Chiligati aliongeza kuwa ili kujenga mshikamano ndani ya Bunge waliafikiana kuwa Mbowe kwa niaba ya CHADEMA awaombe radhi CUF, Bunge zima na Naibu Spika na maneno hayo yaondolewe kwenye hotuba.

“Pia CUF kupitia mnadhimu wao, wawaombe CHADEMA radhi kutokana na baadhi ya wabunge wao kutukana, kuchana hotuba yao na vilevile waliombe radhi Bunge na Naibu Spika kwa usumbufu hadi kuahirisha Bunge,” alisema.

Muafaka wapatikana

Baada ya Chiligati kumaliza, Ndugai alimwita mnadhimu wa CUF, Rashid Ali Abdallah, ambaye alianza kwa kuwaomba radhi Naibu Spika na Waziri Bernard Membe kutokana na vurugu hizo kukwamisha mjadala wa Wizara ya Mambo ya Nje.

Alisema kuwa CHADEMA kwa makusudi, kutokujua au kwa bahati mbaya waliweka maneno ya kuidhalilisha CUF, kwamba wao wameweka maslahi ya taifa mbele kukubali kufikia muafaka.

“Kwa kitendo kile wabunge wa CUF walichemka na kutoa maneno ya kashfa, hivyo naomba samahani kwa yote yaliyotokea,” alisema Abdallah na kushangiliwa na wabunge.

Naye Mbowe alisema kuwa katika dhamira ya usuluhishi na kurejesha amani ndani ya Bunge, hana sababu ya kuhoji mambo yote aliyowasilisha Chiligati.

Mbowe pia alimpongeza mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) akisema alialikwa na kamati hiyo kama mshauri na kutoa msaada mkubwa wa kimawazo kutokana na uzoefu wake.

“Katika kikao kile nilitanguliza kusema kuwa ile kauli ya Wenje haikuwa yake pekee bali ni ya kambi nzima kama ilivyo kwa serikali, kauli ya waziri si yake bali ya serikali, hivyo tusikwepe kuwajibika wote,” alisema.

Alisema kuwa CUF walikwazika na maneno hayo potelea mbali yalikuwa na ukweli au hapana, hivyo ni lazima wapate muafaka ili kuonyesha umoja wao kwani taifa ni zaidi ya vyama.

“Kuna mambo mazito ya kujadili na kusuguana ya msingi zaidi ya hili, nipende kuwaomba radhi CUF na Bunge zima. Pia kwako Naibu Spika, tumeahirisha Bunge mara mbili bila sababu ya msingi. Pole kwa usumbufu mlioupata wote, tumetafakari na kuona tulikojikwaa,” alisema Mbowe na kushangiliwa na Bunge.

Ndugai katika kuhitimisha jambo hilo, aliwasihi wabunge kujiepusha na kauli ambazo zinaweza kuudhi wengine na vilevile aliwataka CUF na CHADEMA kuzingatia makubaliano.

Imeandikwa na Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO