Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Tanzania haiwezi kuiomba radhi Rwanda—Membe

TANZANIA haiwezi kuiomba radhi Rwanda kuhusiana na matamshi aliyoyatoa Rais Jakaya Kikwete mjini Addis Ababa, Ethiopia hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema jana. Alikuwa akitoa majumuisho ya hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/14 bungeni mjini hapa.

Membe alisema siku chache zilizopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda ilimtaka Rais Kikwete kuiomba radhi nchi hiyo, kutokana na matamshi yake kuhusu Rwanda.

Alipokuwa akihudhuria maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika (AU) mwezi uliopita, Kikwete pamoja na mambo mengine, alimtaka Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwa na mazungumzo na vikundi vya waasi nchini humo, katika juhudi za kuleta amani ya kudumu nchini mwake.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda siku chache zilizopita ilisema Rais Kagame hawezi kuwa na mazungumzo na “wauaji” na kumtaka Rais Kikwete aombe radhi kwa kutoa ushauri kama huo.

Jana Membe alisema Rais Kikwete kamwe hawezi kuomba radhi kwa suala la kweli na kwa kutoa ushauri wenye lengo la kuleta amani ya kudumu katika Rwanda.

“Ni wajibu wa serikali ya Rwanda kufanya mazungumzo na maadui. Huu ni ushauri tu kama hawautaki waache.

“Hivi sasa ni miaka 16 tangu mapambano ya waasi nchini humo yaanze… watapigana hadi lini?” alisema.

Alisema wakati wote Tanzania imekuwa ikisisitiza umuhimu wa mazungumzo katika kupata ufumbuzi wa migogoro.

Membe alisema Tanzania imekuwa ikitoa ushauri kama huo hata kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kwa mapigano yanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Alisema baada ya taifa kupeleka askari wake wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kusaidiana na jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa mashariki ya DRC, waandishi wapatao wanane pia watapelekwa ili kukabili propaganda chafu dhidi ya shughuli za askari hao.

Kuhusu mgogoro wa Ziwa Nyasa, Membe alisema hivi karibuni mawaziri wa mambo ya nje na wanasheria wakuu wa nchi mbili za Tanzania na Malawi watakwenda Maputo kutoa ushahidi.

“Kila nchi itatoa ushahidi wake… nina uhakika tutashinda kwa sababu tuna ushahidi sawa na Mlima Kilimanjaro,” alisema.

Bunge lilipitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha

.

Imeandikwa na Mtanzania Jumapili, Juni 2, 2013

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO