Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CCM YAJIFUA KIJESHI MKOANI MBEYA; YADAIWA KUUNDA KAMBI KWA MAAGIZO YA MWIGULU..POLISI WAKIRI

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani.



Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija

********************************

HOFU ya vitendo vya kijangili imezuka mkoani hapa baada ya kuwepo kwa tuhuma za kambi tatu zinazoendesha mafunzo ya kijeshi, zikidaiwa kuendeshwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tuhuma hizi nzito zilizotolewa na uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani, zimedai kuwa kambi hizo zimeanzishwa kutokana na agizo la Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba.

Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija alisema kuwa kambi hizo zimewekwa katika shule tatu za sekondari zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM ambako vijana wa chama hicho wanapatiwa mafunzo ya kijeshi.

Mwambigija alisema kambi hizo zilizoko Ivumwe, Itende na Igawilo, zinaendesha mafunzo hayo huku vijana wakisikika wakitamka maneno ya ‘kata kucha’, ‘ng’oa meno’, ‘ingiza chupa’ na mengine yanayotishia usalama wa watu.

“Tumepata taarifa kuwa vijana hao wanatekeleza maagizo yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba. Vijana hao wapo Ivumwe, Itende na Igawilo, wanatamka maneno hatarishi, wakiimba, kata kucha, ng’oa meno, ingiza chupa na mengine hatuwezi kuyataja, ni hatarishi sana,” alisema Mwambigija.

Mwenyekiti huyo alisema wamegundua kuwa hatua hiyo inalenga pia kuwatisha wananchi wasijitokeze katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Iyela jijini Mbeya unaotarajiwa kufanyika Juni 16.

“Baada ya kufuatilia tumeona mwenendo wa mazoezi hayo una lengo la kuwatisha wapiga kura na kuwafanya wananchi waogope kujitokeza siku ya kupiga kura.

“CHADEMA tunataka kuona uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki, na CCM walipewa muda wa kufanya kampeni, hawajafanya kiasi cha kutosha, kwa hali hiyo wasitumie mbinu nyingine ili kuvuruga uchaguzi,” alisema.

Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa Kanda ya Nyanda za Juu, Lucas Mwampiki ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa CHADEMA Mbeya Mjini, alisema kwa kutumia mbinu za kiintelijensia walifika zilipo kambi hizo kushuhudia hamasa na mafunzo waliyokuwa wakipewa vijana hao.

“Mafunzo na matamshi wanayopatiwa vijana hao hayana sura ya uzalendo, na sijawahi kuona wala kusikia chama kikongwe kikiwafundisha vijana wake maneno hatarishi.

“Sisi tumetekeleza wajibu wetu baada ya kugundua kuwa kambi za wenzetu hazina lengo zuri na uchaguzi huu. Nimeongea na RPC, RCO RSO na CID na viongozi wetu wa chama ngazi ya juu ili kuwajulisha kile kinachoweza kutokea,” alisema Mwampiki.

Baadhi ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya walipohojiwa kuhusu kuwepo kwa kambi hizo, hususan muda huu wa kampeni za udiwani, walikiri na kusema wanatekeleza maagizo ya Mwigulu.

Wakiongea kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, viongozi wawili wa CCM walisema kuwa wanajua maelekezo yaliyotolewa kuhusu mafunzo katika kambi hizo, lakini wakasema anayetakiwa kuzungumza ni Mwigulu mwenyewe.

“Kambi zipo, lakini kwangu binafsi sielewi vijana waliowekwa kambini wanafundishwa nini, maana huko sijafika bado,” alisema mmoja wa viongozi hao.

Alipotafutwa kwa njia ya simu, Mwigulu hakuweza kupatikana kwa vile simu yake ilikuwa imezimwa wakati wote. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno, bado ilionekana haijafunguliwa.

Aidha, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya, Boyd Mwabulanga, alisema kuwa tangu kampeni zilipoanza wamegundua kuwepo kwa vitendo visivyoridhisha ikiwemo mbinu za kughushi shahada za kupigia kura.

Mwabulanga alisema kuwa wanawaomba wenzao CCM kuacha kutumia mbinu chafu zenye lengo la kuwaogopesha wananchi na mikakati iliyoandaliwa ya kutumia vyombo vya dola ikiwemo kupiga mabomu ya machozi ili watu waogope na kushindwa kujitokeza siku ya upigaji kura.

Kadhalika, alisema kuna tuhuma kwamba CCM wameanza mbinu chafu za kughushi shahada za kupigia kura maeneo ya Kabwe jijini Mbeya na kumtaja mtu mwenye mashine inayotumika kughushi.

Pia alisema kuwa baadhi ya wajumbe wa nyumba kumi kumi (mabalozi) wa CCM wamenaswa na kufikishwa kwenye vyombo vya usalama, lakini siku ya pili wameshangaa kuwaona wakitamba mitaani hali ambayo inazidisha kiburi na kuonyesha dhahiri CCM wanavyotegemea polisi.

Kauli ya RPC

Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Mbeya, Diwani amekiri kupokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa uongozi wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya Mjini, na kudai kuwa wanafuatilia suala hilo.

“Tumepata habari hizo na tunafuatilia kwa njia na mbinu zetu, na hadi sasa tunajua kuna mafunzo ya vijana wa CCM yanaendelea,” alisema Kamanda Diwani.

Hata hivyo, Kamanda Diwani alidai kuwa wanachojua ni kuwepo kwa mafunzo ya kawaida kwa vijana wa CCM, na ndiyo maana yanafanyika ndani na kwamba hayahatarishi amani na usalama.

“Lakini bado tunawaomba CHADEMA watusaidie kufuatilia na kama watagundua tofauti na haya tunayoyajua hadi sasa, watuarifu.

Kwa sasa hatuwezi kumkamata yeyote kama wanavyotaka tufanye,” alisema.

Tuhuma hizo zinakuja kukiwa na taarifa za kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya kwa makada wa CHADEMA mkoani Arusha kunakohusishwa na kampeni za uchaguzi.

Mapema wiki hii, kundi la vijana wanaoaminika kuwa wafuasi wa CCM walivamia mkutano wa CHADEMA na kuwajeruhi vibaya baadhi ya watu, jambo lililosababisha kuzuka kwa ghasia kubwa.

Chanzo: TANZANIA DAIMA.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO