Na Thehabari.com
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), umetoa mrejesho wa utafiti shirikishi uliofanywa na kikosi cha waraghbishi kutoka mtandao huo katika baadhi ya vijiji kutoka mikoa ya Shinyanga, Mbeya na Morogoro-huku matokeo yakionesha kuibuka kwa changamoto kadhaa katika maeneo yote ya utafiti.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuelezea matokeo ya utafiti, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya alisema miongoni mwa masuala makuu yaliyojitokeza katika utafiti huo shirikishi na uraghbishi ni pamoja na changamoto za uwekezaji na mgawanyo mbaya wa ardhi kwa wananchi hususan Kata ya Mshewe Mbeya Vijijini.
Mallya alisema masuala mengine ni pamoja na ugumu wa upatikanaji wa huduma za maji safi na salama, Ukosefu wa huduma bora za afya, uongozi mbovu na rushwa maeneo mbalimbali, pamoja na unyanyasaji wa wanawake na wasichana karibu maeneo yote yaliofanyiwa utafiti.
Akifafanua zaidi alisema utafiti ulibani kuchukuliwa kwa maeneo ya ardhi yenye rutuba Kijiji cha Mshewe mkoani Mbeya hali inayosababisha wananchi kukosa ardhi ya kutosha kwa kilimo na makazi hivyo kulazimika wao kuwa vibarua katika mashamba ya wawekezaji ili kujikimu kimaisha. Hali hiyo pia imechangia wanaume kulazimika kutoa rushwa ya pesa ili kupata kazi katika mashamba.
"Wanawake na wasichana wamekuwa wakifanya vibarua katika mashamba ya wawekezaji kwa ujira mdogo kati ya shilingi (2,500/- na 3000/- tu kwa siku). Wakati huo huo wanakumbana na ukatili katika ajira hiyo ikiwemo rushwa ya ngono, hali ambayo inasababisha ongezeko la magonjwa ambukizi yakiwemo VVU na Ukimwi.
Alisema licha ya Sera ya Taifa ya Maji kuweka lengo la kupatikana kwa maji katika umbali kwa mita 400; bado maji safi na salama ni changamoto kubwa kwa wakazi wa Kishapu na Mshewe kwani hakuna huduma za maji safi na salama hali inayotishia maisha na afya zao.
"Mfano Kijiji cha Ilota- Mshewe, licha ya uhaba mkubwa wa maji wananchi wanasaka maji katika eneo hatarishi huku wakichangia maji kidogo yasiyo safi na salama pamoja na mifugo. Cha kusikitisha wananchi wamechanga pesa kwa ajili ya maji kwa muda mrefu bila mafanikio. Katika vijiji vya Isoso na Lubaga Kata ya Kishapu, ukosefu wa maji umesababisha wanawake na wasichana kutembea umbali mrefu na mazingira hatarishi ambayo yamesababisha ongezeko la mimba za utotoni, ubakaji kwa wanawake na wasichana na vipigo."
Alisema tatizo hilo limeongeza umasikini wa kipato kutokana kutumia muda mwingi na rasilimali kusaka maji. Kilio chao kikubwa ni kupata vyanzo mbadala vya maji hasa kutoka zi wa Victoria. Aidha aliongeza utafiti ulibainia huduma mbovu za afya kwani katika Kijiji cha Ilota Mkoa wa Mbeya wananchi wamekiri kutokuwepo na zahanati hali inayosababisha wanawake wajawazito kujifungulia majumbani, huku Kata ya Kisaki Morogoro vijijini, tatizo kubwa likiwa ni ukosefu wa dawa na wahudumu wa afya zahanati za vijiji vya Gomero, Station na Nyarutanga licha ya uwepo wa majengo mazuri bila wahudumu, dawa wala vifaa tiba kwa ajili ya uchunguzi. Eneo hilo pia wananchi huchangia gharama kubwa za usafiri wa gari la wagonjwa (shs 70,000) kwenda Morogoro hususan wanawake wanaokwenda kujifungua.
Alisema suala la viongozi kutowajibika na vitendo vya rushwa limejitokeza karibu maeneo yote ya utafiti
ikiwemo uwepo wa usiri wa taarifa za mapato na matumizi, viongozi kutowashirikisha wananchi katika masuala ya maendeleo, viongozi ngazi za vijiji kuruhusu video za ngono kuoneshwa maeneo yao na kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi.
"Unyanyasaji wa kijinsia umejitokeza kama suala mtambuka katika maeneo yote. Mfano tatizo la maji linasababisha vipigo kwa wanawake, ubakaji, elimu duni kwa wasichana, mimba za utotoni na ukosefu wa kipato. Kwa upande wa uwekezaji/ardhi, wanawake na wasichana wamekumbana na rushwa ya ngono, ajira isiyo na staha pamoja na kipato kidogo na kwa upande wa afya, wanawake wamekuwa wakidaiwa fedha na vifaa wakati wa kujifungua na hata kujifungulia katika mazingira hatarishi," alisema Mallya.
Aidha alisema lengo kuu la utafiti huo ilikuwa kujenga mifumo mbadala dhidi ya mfumo dume, uliberali mamboleo na mifumo yote kandamizi, huku akidai maafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuendeleza kampeni ya Haki ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake Walioko Pembezoni ambayo imewezesha kujenga nguvu za pamoja na kuongeza uelewa wa masuala ya kijinsia na ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi mbalimbali hapa nchini na hata nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya akizungumza
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo
Meneja wa Kitengo cha Habari, Lilian Liundi (kulia) akiwa katika mkutano huo
0 maoni:
Post a Comment