Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

SUGU AKAMATWA; WABUNGE CHADEMA WAZUILIWA KUVAA KOMBATI

Chadema wakienda kutoa maoni ya katibaWabunge na viongozi wa Chadema wakielekea Ikulu kuonana na Rais Kikwete kwa maswal aya Katiba mwaka jana. Mavazi yanayovaliwa sana na watu wa Chadema katika rangi tofauti kama picha inavyoonesha ndio yaliyoibu atafrani Bungeni. Picha ya maktaba.
KATIKA mwendelezo wa kuibana CHADEMA, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ameshikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma jana kwa mahojiano ya saa tatu akidaiwa kuandika ujumbe wa kumkashifu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mbilinyi maarufu kama Sugu anadaiwa kusambaza ujumbe huo kwenye mtandao wa kijamii ukisomeka; “Tanzania haijawahi kuwa na Waziri Mkuu mpumbavu kama Pinda.”

Akithibitisha kuhojiwa kwa mbunge huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema walimshikilia kuanzia saa 8 mchana hadi 10:30 jioni na kisha kumwachia kwa dhamana.

Misime alisema Mbilinyi atatakiwa kuripoti polisi leo asubuhi na kwamba uchunguzi wa tukio hilo ulikuwa ukiendelea.

Mbilinyi anadaiwa kuandika maneno hayo kwenye ukurasa wake wa facebook baada ya Pinda kusema watu wanaokaidi amri ya polisi wapigwe tu, akiitafsiri kauli hiyo kuwa ni upumbavu.

Alipotafutwa na Tanzania Daima Jumatano kuzungumzia tukio hilo, Mbilinyi hakupokea simu yake ya kiganjani ingawa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa CHADEMA, John Mnyika alithibitisha kuwa alipewa dhamana.

Wiki iliyopita katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu kuhusu kauli ya serikali katika vurugu zenazoendelea nchini, Pinda alisema wanaokiuka amri wapigwe tu na polisi.

Alifafanua kuwa anasema wapigwe kwa kuwa serikali imechoka na vitendo vya vurugu. “…Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine…maana tumechoka.”

Kombati za CHADEMA mzozo

Siku moja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na wabunge wenzake watatu kuzuiwa kuingia bungeni juzi, uongozi wa Bunge umesisitiza kuwa kombati zao zinakiuka kanuni.

Mbowe na wabunge wenzake wa CHADEMA, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) walizuiwa na askari kwa madai kuwa wamevalia sare za chama ambazo kikanuni haziruhusiwi.

Uamuzi huo uliibua hali ya sintofahamu kwa wabunge wa CHADEMA kutokana na Mbowe kuvalia vazi hilo mara nyingi tangu aingie bungeni mwaka 2010.

Licha ya kanuni za Bunge kuruhusu vazi la ‘safari suti’ kwa wanaume lenye mshono kama kombati zinazovaliwa na baadhi ya wabunge wa CHADEMA, Tanzania Daima Jumatano limebaini kuwa uamuzi huo unaacha maswali mengi yanayohitaji majibu.

Akizungumzia uamuzi huo jana, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema suti hizo za wabunge wa CHADEMA zilikiuka kanuni ya 149 (3) (b) (i).

Kipengele hicho cha kanuni kinasomeka kuwa inaruhusiwa suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia.

Joel alifafanua kuwa yawezekana huko nyuma wamekuwa wakifanya makosa kwa kuwaruhusu wabunge hao kuingia na suti hizo, lakini sasa kuanzia juzi wameamua kuanza kuchukua hatua ya kuwazuia.

“Zile wanasema sio sare ya chama, lakini wote tunawaona kwenye mikutano na shughuli za chama ndizo zinavaliwa na isitoshe tuliwahi kuwatahadharisha kuwa ziko kinyume na kanuni wasizivalie bungeni ila wamekuwa wakiendelea kuzivaa,” alisema.

Licha ya kanuni hiyo kuwa kimya kuhusu kuvaa sare za vyama bungeni, Joel alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa ni busara ya spika wa wakati huo, Samuel Sitta, lakini haujaingizwa kwenye kanuni kimaandishi.

Tanzania Daima Jumatano lilitaka kufahamu ni kwanini uamuzi huo ukaanza ghafla juzi baada ya wabunge wa CHADEMA kurejea kutoka jijini Arusha, na Joel bila kufafanua alisema: “Kawaulize walipanga nini wakiwa Arusha? Ndiyo maana tukaamua kuchukua hatua.

“Bora tukaonekana tumewaonea kuliko kuendelea kufumbia macho kanuni. Tuwe wawazi kombati zao zina nakshi kupitiliza kwa mujibu wa kanuni. Kwanini wakina Halima Mdee na Vicent Nyerere tuliwaacha wakaingia? Mbona kombati za Zitto zinatofautiana na wengine?”

Alipotakiwa kufafanua kama kweli walishaonywa wasivae kombati hizo bungeni, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa CHADEMA, John Mnyika alisema Joel hajui kanuni za Bunge ndiyo maana amekuwa anampotosha spika na viongozi wa Bunge kufanya uamuzi wa ajabu.

“Wametuzuia juzi kwa sababu ya maelezo ya akina Pinda na Serikali ya CCM, sio kwa sababu ya ukiukwaji wa kanuni za Bunge. Kumekuwa na utamaduni wa hovyo wa kutafsiri vibaya kanuni za Bunge kwa lengo moja tu, kuwadhibiti CHADEMA,” alisema.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alitolea mfano akisema kuwa walizuiliwa kuingia ukumbini na askari polisi wasiokuwa na mamlaka ya kuwazuia kuingia ndani bali walitakiwa wasubiri amri ya spika kuwatoa ukumbini ndipo wawatoe.

“Hayo yote hawezi Joel kufahamu, anafanyia uzoefu alioupata wakati anafanya kazi Makao Makuu ya CCM wakati wa Bunge la chama kimoja,” alisema Mnyika.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kuwa walishangazwa na uamuzi huo wakati mavazi hayo wamekuwa wakiyavaa miaka yote na kuingia nayo bungeni.

Lissu alisema kuwa hatua hiyo waliichukulia kama mkakati maalumu wa Serikali ya CCM kutaka kuwazima kabisa kuhakikisha hawapati nafasi ya kuingia bungeni ili kujibu tuhuma walizosingiziwa kuhusiana na mlipuko wa bomu jijini Arusha.

“Sisi hali hiyo tulianza kuishtukia tangu asubuhi tulipoingia kwenye eneo la Bunge, kama mligundua kulikuwa na askari wengi sana kila kona kuliko kawaida kana kwamba nchi imepinduliwa. Kinyume na utaratibu wa kanuni askari wa kawaida wameingizwa hadi bungeni,” alisema.

Hata hivyo, pamoja na uamuzi huo, kanuni za Bunge hakuna mahali zinazuia mbunge kuvaa sare ya chama chake isipokuwa kanuni zimeainisha aina za mavazi ya kuvaliwa na wabunge wanawake na wanaume.

Kwa mujibu wa kanuni ya 149 (3)(b) kwa wanaume wanaruhusiwa kuvaa (i) suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia;

(ii) vazi la kimwambao yaani kanzu rasmi na nadhifu, koti, baraghashia na makubadhi au viatu; (iii) suti kamili ya kimagharibi ya rangi kadiri isiyomeremeta;
(iv) koti aina ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au
(v) tarbushi na kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti ya imani au mila.

Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO