TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Marakech mjini hapa na wenyeji Morocco, katika mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani.
Hadi mapumziko, Morocco walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Abderazak Hemed Allah dakika ya 37, baada ya yeye mwenyewe kujiangusha kwenye eneo la hatari baada ya kugongana na Aggrey Morris. Morris alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya hapo na Stars wakabki pungufu. Kipindi cha pili Morocco walirejea na moto tena, wakiishambulia zaidi Stars iliyoonekana kudhoofika na katika dakika ya 50 Youssef El Arabi akafunga bao la pili kiulaini baada ya kuwatoka mabeki wa Tanzania na kubaki na kipa Juma Kaseja.
Hata hivyo, shambulizi la kushitukiza liliipatia Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager bao la kwanza dakika ya 61 lililofungwa na Amri Kiemba kwa shuti la mbali kutoka wingi ya kushoto. Kwa matokeo hayo, Stars inabaki na pointi zake sita baada ya kucheza mechi nne, kushinda mbili nyumbani na kufungwa mbili zote ugenini, nyingine ikiwa dhidi ya Ivory Coast.
Lakini Stars inabaki nafasi ya pili mbele ya Morocco yene pointi tano sasa, wakati Ivory Coast wanaongoza kwa pointi zao saba kabla ya matokeo ya mechi na Gambia leo. Picha imedhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
0 maoni:
Post a Comment