Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Makala: Mambo Yakukumbukwa miaka 29 kifo cha Sokoine

100_9811Waziri wa Michezo Mh Mukangala, Mbunge wa Monduli Mh Lowassa, Mbunge wa Simajiro Mh Olesendeka, Mbunge wa Arusha Mjini Mh Lema na mtoto wa Hayati Sokoine, na mbunge wa Viti Maalumu Mh Namelok Sokoine na muaandaaji wa mashindano ya riadha Sokoine Mini Marathoni, Bw Wilhlm Gidabudai wakiwa katika matembezi Monduli Juu jana katika tukio la kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 29 tangu kufariki kwa Edward Moringe Sokoine. Picha na Seria Tumainniel
********************************

Ilikuwa Jumatano ya Aprili 12, 1984 saa 11:30 jioni, siku ambayo Dar es Salaam ilinyesha mvua kutwa nzima. Wakati kipindi cha salaam cha Jioni Njema cha Redio Tanzania (RTD) wakati huo kikiwa hewani, mara matangazo yake yanakatishwa ghafla na wimbo wa taifa unapigwa.

Mara inasikika sauti iliyozoeleka ya Rais Nyerere wakati huo ikisema: “Ndugu wananchi, leo majira ya saa 10 jioni, ndugu yetu, kijana wetu na mwenzetu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine wakati akitoka Dodoma kuja Dar es Salaam, gari yake imepata ajali, amefariki dunia.”

Takribani miaka 29 imepita tangu kufariki kwa, Edward Moringe Sokoine, aliyepata kuwa waziri mkuu wa Tanzania katika vipindi viwili tofauti kabla ya kufariki Aprili 12, 1984.

Sokoine alikufa baada ya kutokea ajali ya gari eneo la Wami-Dakawa, wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro akiwa njiani kurejea Dar es Salaam akitokea mjini Dodoma alikokuwa akishiriki vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kumbukumbuka kila mwaka
Aprili 12 ya kila mwaka, taifa limekuwa likiadhimisha kumbukumbu ya kiongozi huyo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kuendesha makongamano, midahalo, mabonanza, ibada, riadha na upandaji mlima Kilimanjaro.

Katika utawala wa hayati baba wa taifa na rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika eneo la Wami  Sokoine kulijengwa nyumba moja na banda moja linalotumika kama jukwaa lakini kwa sasa majengo hayo yamechakaa, anasema msimamizi wa eneo hilo, Hamis Said Mpandachuri.

Mwananchi ilifika katika eneo hilo na kukuta mnara wa picha ya Sokoine ukiwa umepakwa rangi mpya za manjano, kijani, blue na nyeusi huku chini ya picha yake kukiwa na maneno “Alimtumikia Mungu kwa kuwatumikia watu, sauti ya watu ni sauti ya Mungu”.

Mbali ya mnara huo na majengo yaliyojengwa katika utawala wa serikali ya kwanza, pia liko jengo jipya na la kisasa ambalo linaendelea kujengwa nyuma ya majengo ya zamani. Kwa mujibu wa uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero, jengo hilo ni kwa ajili ya shule ya sekondari ya Sokoine (Sokoine memorial high school), inajengwa kama sehemu ya jitihada za wilaya hiyo za kumuenzi Sokoine.

Mbali na jitihada za halmashauri hiyo, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambacho pia kimebeba jina lake kimekuwa katika mikakati ya kuhakikisha kuwa kinamuenzi kiongozi huyo kwa kila hali. Kassim Msagati ni ofisa mawasiliano wa chuo hicho,  anasema hayati, Edward Moringe Sokoine, alikuwa muhimili muhimu wa kuanzishwa wa chuo kikuu hicho cha kilimo ambacho ni chuo kikuu pekee cha kilimo cha Serikali nchini.

Aprili 12, 1984 bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo hayati Sokoine alishiriki lilipitisha sheria namba 6 ya mwaka 1984 ya kuanzishwa kwa chuo kikuu cha kilimo Morogoro. Hapo kabla chuo hicho kilikuwa ni kitivo cha kilimo cha kilimo na misitu cha chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Msagati, sheria hiyo iliyopitishwa na bunge ilikiidhinisha kitivo cha kilimo cha chuo kikuu cha Dar es salaam kilichokuwa Morogoro kuwa chuo kikuu na kutaka kiitwe chuo kikuu cha kilimo Morogoro.

Lakini chuo hicho kililazimika kubadilishwa jina hata kabla ya jina la awali kuanza kutumika na kuitwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Hii ilitokana na kifo cha kiongozi huyo, muda mfupi baada ya chuo hicho kuidhinishwa rasmi kwa sheria hiyo ambapo utekelezaji wake ulipaswa kuanza mwezi Julai, 1984, ndipo serikali ikakubali kiitwe Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo.

Kutokana na umuhimu huo, chuo hicho kinakila sababu ya kumuenzi Sokoine kwa vitendo na hatua hiyo imekuwa ikichukuliwa kwa kuhakikisha kila mwaka ifikapo Oktoba, chuo huandaa mdahalo maalum wa kumbukumbu ya Sokoine ambapo viongozi mbalimbali wa kitaifa hualikwa.

Historia yake
Kila kiongozi ana historia yake katika uongozi wa kisiasa, kijamii na ofisi za umma.  Edward Moringe Sokoine inaelezwa alishawishiwa awe kiongozi.Kwa mujibu wa mzee Saiguran Kipuyo ambaye amekua pamoja na hayati Sokoine, ni kwamba hayati alishawishiwa kuingia kwenye uongozi.

“Kipindi kile alikuwepo Chifu mmoja akiitwa Edward Barnoti. Vijana tulimuona hatutendei haki wala kusimamia maslahi yetu hivyo tukaamua kumpenyezea mtu wa rika letu kama msaidizi wake,” anasimulia  Kipuyo

Kipuyo ambaye anasema amezaliwa kati ya mwaka 1928-1944 anaeleza kuwa vijana ndio waliokwenda kumchukua Sokoine kwa nguvu kutoka kwenye shughuli zake za kuchunga eneo la Mfereji alikoenda baada ya kumaliza elimu ya msingi katika shule ya kati ya Moringe mjini Monduli.

“Tulimlazimisha kuwa msaidizi wa chifu Mkuu wa Council ya Maasai land akimsaidia Chifu Barnoti na ilipofika kipindi cha uchaguzi wa mbunge tukamlazimisha kuchukua fomu kuchuana na mzee Barnoti, tulifanya kampeni ya chini chini hadi akashinda,” anasimulia

Anasema baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 1965 akiwakilisha jimbo la Maasai Land inayojumuisha wilaya za sasa za Monduli, Simanjiro, Kiteto, Longido na Ngorongoro, Sokoine aliteuliwa kuwa waziri mdogo wa ujenzi kabla kuhamishiwa ulinzi na jeshi la kujenga taifa.

Tabia ya asili ya Sokoine
“Pamoja na Uwaziri Mkuu, Sokoine alikuwa yule yule. Alikuwa na tabia ya kipekee. Alikaa na kuzungumza na watu wa rika zote kuanzia wazee, akina mama, vijana na watoto, alitumia fursa hiyo kujua matatizo yao na kupata maoni kuhusu utatuzi kutoka kwa wahusika wenyewe,” anasema Kipuyo

Waliopeleka majungu kwa Sokoine walifanikiwa?
“Alipopelekewa majungu ya mtu, alimwita anayefitiniwa na kumtaka mpika majungu kusema yote mwenzake akiwepo. Kwa tabia hii alikomesha majungu,” anafafanua.

CCM na Chadema wanasemaje?
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mahojiano maalum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa CCM (UWT), wilaya ya Arumeru, Ester Maleko na Mwenyekiti wa baraza la vijana wa Chadema (Bavicha), mkoa wa Arusha, Ephata Nanyaro  wanakiri Sokoine ni kiongozi aliyekuwa na tunu za kipekee aliyewahi kutokea nchini.

Hakuna kama Sokoine
Kwa upande wake, Nanyaro yeye anasema tangu uhuru, taifa halijawahi kupata kiongozi aina ya Sokoine na Nyerere ambao walipenda nchi na watu wao kwa dhati na kuwa tayari kujitolea nafsi zao kushughulikia matatizo yao.

Baadhi ya nukuu muhimu za Sokoine;
“Ole wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa siasa hana usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na Wananchi peke yake. Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao. Labda tusiwajue. Hawa hatuna sababu ya kuwapa imani, kuwa tutawalinda kama vitendo vyao viovu” - Edward Moringe Sokoine, 26 Machi 1983

“Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi yawe ni chombo cha kulinda haki na maslahi ya walio wengi. Na kamwe hayaruhusiwi kuwa ni chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau maslahi ya walio wengi” - Edward Moringe Sokoine, 1Februari 1977.

Makala haya yameandikwa na Venance George na Peter Saramba; Gazeti Mwananchi

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO