SIKU moja baada ya Mkurugenzi wa Mambo ya Katiba wa CHADEMA, Tundu Lissu kufichua njama zinazofanywa ili kutengeneza ushahidi wa uongo kwa ajili ya kuutumia katika kesi ya ugaidi inayomkabili Wilfred Lwakatare, baadhi ya wahusika wameanza kuvurugana.
Kwa mujibu wa Lissu, njama hizo zinafanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama na ujasusi ili kutumia ushahidi huo mahakamani dhidi ya Lwakatare ambaye ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA.
Alisema kuna baadhi ya vijana wa CHADEMA wa Idara ya Ulinzi na Usalama wanaopewa fedha na kuahidiwa kufundishwa namna ya kuzungumza katika kesi hiyo ya Lwakatare.
Lissu alisema kuna baadhi ya vijana wakiongozwa na Saumu Mulugu ambaye alifukuzwa kazi CHADEMA mwanzoni mwa mwaka jana, wamepokea fedha kutoka kwa kigogo mmoja wa CCM (jina linahifadhiwa) ili kufanikisha mpango huo.
Jana gazeti hili lilimnasa Saumu akiwa anawasiliana na wenzake, huku akiwatuhumu baadhi yao kuwa ndio waliovujisha siri kwa Lissu.
Vile vile alionekana akiwasiliana na kigogo mmoja wa CCM ambaye alikuwa akimwita ‘mkuu’ huku akimsomea baadhi ya taarifa zilizoandikwa magazetini jana kuhusu kuvuja kwa siri zao.
Saumu akiwa katika grosari maarufu kwa jina la Kwa Kimaro jirani na eneo la Benki Kuu ya Damu Salama Mchikichini jijini Dar es Salaam, alisikika akiwalalamikia wenzake kwa kumsaliti na kuvujisha mkakati wao kwa Lissu.
“Kwanini mmelikisha siri zetu kwa Lissu hadi amejua tulikutana katika hoteli ya kifahari na Mwigu? Sasa nitawaonesha, maana laki tano zenu ninazo mimi. Siwapi bali nitazitumia kujilinda,” alitamba.
Saumu ambaye alikuwa akizungumza kwa sauti kubwa ya ghadhabu kupitia simu, aling’aka: “Nyie kwanini mmeniuza kwenye ishu ambayo tumeipanga wote?”
Baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa ‘mkuu wake’ aliendelea kupiga simu akimlalamikia mtu ambaye hakumtaja, kuwa alikuwa amezima simu yake makusudi kwa kuwa ndiye alivujisha siri zao kwa CHADEMA.
“Mimi sitakubali na nimehakikishiwa na bosi wetu kuwa huyo aliyetusaliti tutatumia wale askari kumwekea hata unga. Haiwezekani fedha tumepokea za kwanza, za pili na tatu kwanini tuuzane dakika za mwisho?” alidai Saumu huku akiendelea kugida bia yake.
Huku akihaha huku na kule, Saumu alikuwa akiwapigia simu baadhi ya madereva wa CHADEMA makao makuu na kuwaomba simu za baadhi ya watu, na hata wakati mwingine kuwafokea akidai ndio waliofichua siri hiyo.
Hata hivyo, baada ya kutilia shaka nyendo za chanzo chetu kudaka siri zake, ghafla alitokomea na kuzima simu zake mara moja kwani hata alipotafutwa baadaye hakupatikana.
Katika madai yake, Lissu alisema hadi sasa vijana hao wameshapewa sh 400,000 ili wakubali kwenda kufundishwa jinsi ya kuzungumza mahakamani kuwa CHADEMA ni chama cha kigaidi, kwamba Lwakatare alipanga mikakati ya kigaidi.
“Awali walipewa 400,000, wakapewa tena 300,000, pia wakapewa 35,000 mara mbili. Na fedha zote hizi walikuwa wanapewa kwa njia ya M-Pesa,” alisema Lissu.
Alidai kuwa Saumu ndiye anayeratibu mpango wote kati ya Jeshi la Polisi na vijana hao wa CHADEMA kwa kuwarubuni kwa fedha.
Alisema vikao baina ya vijana hao wa CHADEMA na Saumu vimewahi kufanyika mara kadhaa katika moja ya hoteli maarufu nchini juu ya mambo ya kwenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari au mahakamani kwenye kesi ya Lwakatare.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba hakupatikana kuzungumzia tuhuma hizo kama anahusika nazo kwa namna yoyote.
Chanzo: Tanzania Daima
0 maoni:
Post a Comment